Makala
Uteuzi wa Dk Nchimbi na hekaheka za urais 2030

Dar es Salaam. Uteuzi wa Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu mwaka huu umewasha taa ya kijani ya mbio za urais mwaka 2030.
Dk Nchimbi ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM alipendekezwa na Mgombea Urais wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa chama uliohitimishwa jana Jumapili, Januari 19, 2025.
Hiyo inatokana na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kumwomba Rais Samia apumzike ombi ambalo lilikubaliwa. Uamuzi huo umepokelewa kwa mitizamo tofauti na wadau wakiona Dk Nchimbi anayesifika kwa siasa za kimkakati ni turufu kwa CCM.
Hii itakuwa ungwe ya kwanza kwa Rais Samia kuwania urais. Aliingia Ikulu Machi 19, 2021 baada ya kuapshwa na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuchukua nafasi iliyokuwa imeachwa wazi na mtangulizi wake, John Magufuli.
Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam. Makamu wake, Samia kwa mujibu wa Katiba akaapishwa kuwa Rais. Naye akamteua Dk Mpango ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango kuwa Makamu.
Rais Samia akiwaeleza wajumbe wa mkutano mkuu maalumu baada ya Dk Mpango (68) kuomba kupumzika alishauriana na marais wastaafu Jakaya Kikwete, Ali Mohamed Shein na Aman Abeid Karume kuona nani ni mtu sahihi na wakamwona Dk Nchimbi.
“…jina moja hilo ndilo nimelipeleka kamati kuu na wao wamelikubali, nalileta kwenu jina la kijana wenu Dk Emmanuel Nchimbi,” alisema Rais Samia huku ukumbi ukilipuka kwa shangwe.
Baada ya uteuzi huo, mijadala imekuwa maeneo mbalimbali ikiwemo mitandaoni na hata wasomi waliozungumza na Mwananchi juu ya uteuzi huo na mbio za urais mwaka 2030 ambapo Rais Samia atakuwa amemaliza muda wake Kikatiba.
Moja ya mambo yanayoweza kumbeba Dk Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya ni kuaminiwa. Taarifa sahihi ndani ya CCM zinathibitisha yeye ni mmoja kati ya vijana wanaoaminiwa mno na chama hicho ‘vijana wa chama,’ wenye msimamo wa kuitetea CCM muda wote, walio tayari kufanya lolote kwa ajili ya chama chake na waliokulia ndani ya CCM.
Kuaminiwa huku na ‘mabosi’ ndani ya chama, kunamfanya awe na turufu mkononi. Lakini yote haya yanachagizwa na uaminifu wake, katika wizara zote alizopita.
Pili, dhana ya ‘ujana’ inambeba. Dk Nchimbi ni mmoja wa wanasiasa waliopikwa kuanzia ujana ambao wanaonekana kuifahamu CCM na amewahi kuiongoza UVCCM na hivyo anajua mahitaji ya vijana ndani ya CCM na ndani ya nchi.
Jambo jingine linalompa nguvu, ni bahati. Dk Nchimbi ni mtu mwenye bahati. Miaka yote aliyokaa ndani ya CCM amekuwa mtu wa kupanda ngazi tu, kutoka kuongoza UVCCM hadi kuwa mkuu wa wilaya hadi kuwa mbunge hadi kuwa naibu waziri wa wizara mbili tofauti hadi kuwa waziri kamili na Balozi.
‘Safari kuelea 2030’
Baadhi wasomi wamezungumzia uteuzi wa Dk Nchimbi wakisema ni mtu sahihi kutokana na uzoefu wa kwenye siasa.
Hata hivyo, wengine wamesema uamuzi unaweza kumsafirishia njia za kuwania urais mwaka 2030 huku baadhi wakieleza pamoja na Dk Nchimbi kuwa mtu sahihi lakini uteuzi huo unalenga kuvunja mtandao wa makundi ya ndani ya chama hicho tawala.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Aviti Mushi ni bora ameteuliwa Dk Nchimbi ni kiongozi hodari na huenda akawa Rais ajaye wa Tanzania.
“Ndiyo maana huenda akaukwaa urais na CCM wamefanya vizuri sana kumweka yeye, ana sifa zote zinazotakiwa. I hope (nina matumaini), atafanya vizuri na baadaye akishika usukani atafanya vizuri zaidi, bado kijana mwenye umri na nguvu.
“Ni mtu mwenye kuleleta mawazo tofauti, licha ya kipindi cha nyuma kuwekwa kando, atachagiza zaidi pale alipoishia Dk Mpango,” amesema Dk Mushi.
Mchambuzi mwingine wa siasa, Ramadhan Manyeko amesema kwa kipindi fulani Dk Nchimbi amekuwa akitajwa kuwania urais, hata aliporudishwa nchini baadhi ya watu walibashiri hivyo kwa muda fulani.
“Dk Nchimbi ana ndoto za kuwa rais, kwa ishara ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza, kuna uwezekano mkubwa baada ya Rais Samia kumaliza muda wake huenda akawa yeye ni kama vile anaandaliwa,” amesema Manyeko.
Kuhusu kuteuliwa ugombea mwenza, Manyeko amesema:”Nchimbi anaonyesha ana busara, hana jazba anakaribiana na mtangulizi wake (Dk Mpango), ingawa hakuwa mwanasiasa.
“Kumbuka Balozi Nchimbi aliwahi kuwa mwenyekiti wa UVCCM Taifa, kwahiyo anakifahamu chama na siasa, lakini pia ni mwanadiplomasia.Ataleta mageuzi makubwa na mzoefu kwenye siasa za Tanzania, atakuwa mshauri mzuri kwa rais,” amesema.
Moja ya kiongozi mwandamizi mstaafu wa CCM aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema: “Uteuzi huo wa Emmanuel una sura mbili kama Makamu wa Rais, lakini kulikuwa na swali nani kumrithi Samia 2030 na nilijua tunaanza kumwona mwakani baada ya uchaguzi lakini sasa tunaanza kumwona Dk Nchimbi kama mrithi wa nafasi hiyo.”
Kiongozi huyo amesema: “Emma huyu ni mwana mtandao na mikakati. Kijana wa chama. Lakini kwenye siasa kuna mambo mengi yanatokea, unapanga hili linatokea hili kwa hiyo wacha tusubiri kuona.”
Mhadhiri mwingine, Dk Faraja Kristomus amesema inawezekana yanayosemwa kuhusu Dk Nchimbi kuwania urais ikawa kweli kwa sababu mikakati mingi ya vyama inakuwa siri hasa kuelekea katika chaguzi.
“Si unakumbuka Rais Samai alisema jana kwamba amenong’ona na wazee wastaafu kuhusu jina la mgombea mwenza, sasa hatuwezi kujua lingine waliongo’na ni lipi? Na walinongo’na na kuwaza hadi kufika wapi?
“Inawezekana wana mikakati inayoelekeza hadi mwaka 2030, lakini kwa upande mwingine naona ni kama jambo la mkakati wa kuua makundi pia.Kwa sababu tulikuwa hatuna uhakika kama makundi yale ndani ya CCM ya mwaka 2015 yamekwisha au yanaendelea kuwepo,” amesema Dk Kristomus.
Amefafanua kitendo cha Dk Nchimbi kuwa katibu mkuu, kisha kuteuliwa kuwa mgombea mwenza, huenda ni mkakati wa kuua hayo makundi, akikumbushia kwamba Hayati Edward Lowassa aliondoka na wanachama na kurudi nao.
“Miongoni mwa nguzo ya Lowassa, Dk Nchimbi alikuwa mmoja wao na alikuwa mshirika mkubwa wa kambi hiyo, Rais aliyepita alijaribu kukabiliana na kambi hiyo sidhani kama alifanikiwa.
“Kumbuka Rais Samia ni matokeo ya Hayati Magufuli, hivyo ni kama anatuliza maumivu ya kambi ya pili ili ifurahi kidogo, lakini tusisahau siasa zetu zina kura za kikanda, ukiwa makamu mwenyekiti anatoka kanda ya ziwa na mgombea mwenza anatoka nyanda za juu kusini, unaweka uwiano sawa,” amesema Dk Kristomus.
Suala hilo la ukaribu na Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu na miongoni mwa makada zaidi ya 30 wa CCM waliojitokeza kuomba ridhaa ya chama hicho kuwania urais mwaka 2015.
Hata hivyo, Kamati Kuu ya CCM chini ya Kikwete ilikata jina la Lowassa na wagombea wengine. Hata hiyo, kamati kuu ililikata jina la Lowassa na wagombea wengine. Dk Nchimbi, aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba na Adam Kimbisa waliokuwa wajumbe wa kamati kuu walitoka kupinga uamuzi huo.
Dk Nchimbi, Kimbisa na Sophia walikuwa wanamuunga mkono Edward Lowassa ambaye baada ya kukatwa alitimkia Chadema ambako alipitishwa kuwania urais na kuitetemesha CCM.
Hata hivyo, baada ya mgombea urais kupatikana, Dk Nchimbi alijitokeza hadharani na kueleza kama chama kimefanya uamuzi, mtu akiendelea kuupinga, huo ni usaliti.
Machi mwaka 2017, akiwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Dk Nchimbi alikumbwa na msukosuko ndani ya CCM, akapewa onyo kali na adhabu ya kutogombea nafasi yoyote kwa kipindi cha miaka minne.
Adhabu hiyo ilitokana na kilichoelezwa na CCM kuwa, ni usaliti katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Dk Nchimbi ni nani?
Dk Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya. Elimu yake ya Msingi aliianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 – 1986.
Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi kutoka wilayani Songea ni askari mstaafu wa Jeshi la Polisi na wakati anastaafu alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara.

Mzee John Nchimbi
Mzee Nchimbi pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia kundi la majeshi na baadaye katibu wa CCM wa mkoa. Alikoma kushiriki masuala ya kisiasa mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.
Dk Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Sekondari Uru kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990.
Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika kilichokuwa Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).
Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).
Dk Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.
Alisoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya benki na fedha.
Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003–2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Dk Nchimbi amemuoa Jane na wana watoto watatu.
Mbio za ubunge
Dk Nchimbi alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM. Ilipotimu mwaka 2005, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu.
Dk Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.
Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini. Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009.
Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa Chadema na kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii Dk Nchimbi akipoteza takriban ushindi wa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro.
Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Rais Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013 kwa shinikizo, baada ya ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, iliyoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli juu ya “Oparesheni Tokomeza”.
Wakati watu wengi wanadhani Nchimbi aling’olewa uwaziri kwa shinikizo la Bunge, ukweli ni kuwa aliondoka kwa shinikizo la vikao vya CCM.
Ripoti ya kamati ya Lembeli ilieleza wazi kuwa anayepaswa kuwajibishwa ni waziri mmoja tu (Dk Mathayo David, aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) lakini “party caucas” ya CCM ikawaangushia mzigo wengine watatu akiwamo Dk Nchimbi.
Lembeli aliwahi kukaririwa akisema: “Ripoti ilimtaja Dk Mathayo na sababu tulitoa mle ndani. Hao wengine watatu si kamati, ni mambo ya hukohuko kwenye party caucas. Ndiyo maana mara ya mwisho nilikwenda pale nikasema kuwa (Khamis) Kagasheki (Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, anaonewa.”
