Makala
Kama ni goli, hili la CCM ni la Tik-Taka

Katika soka, goli linalofungwa kwa Tik-Taka huhesabiwa miongoni mwa magoli bora na ya viwango na uamuzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kuteua wagombea wake wa urais wa Tanzania na wa Zanzibar, unafanana na goli hilo.
Katika mkutano mkuu maalum wa CCM uliomalizika jana Jumapili, Januari 19, 2025 jijini Dodoma, wajumbe walifanya uamuzi wa kihistoria, wa kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan kupeperusha bendera yake katika nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu 2025.
Lakini Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) nayo ikamchagua Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kuwa mgombea urais katika uchaguzi huo, huku Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akichaguliwa kuwa mgombea mwenza.
Kwanini nasema ni sawa na goli la Tik-Taka, ni kwa sababu mbili kubwa, moja ni kama imezima vuguvugu la makada waliokuwa wamejipanga kumpinga Rais Samia asiwe mgombea pekee ‘automatikali’ kama ulivyo utamaduni wao ndani ya CCM.
Ingawa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na ile ya CCM ya mwaka 1977 zinatambua urais ni miaka mitano mitano, lakini CCM kina utamaduni iliyojiwekea wa Rais kuhudumu kwa vipindi viwili mfululizo.
Rais Samia aliyekuwa makamu wa Rais, aliingia kushika wadhifa huo kupitia ibara ya 37(5) kushika wadhifa wa kiti cha urais baada ya mtangulizi wake, John Magufuli kufariki dunia Machi 17, 2021 akiwa ndio ameanza tu mhula wa pili.
Ibara ya 40(4) inasema kama makamu wa Rais atashika kiti cha urais kwa muda wa wa unaopungua miaka mitatu, ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara mbili lakini ameshika miaka mitatu au zaidi, ataruhusiwa kugombea mara moja tu.
Pamoja na utamaduni huo ulioasisiwa kwa miaka mingi, safari hii lilijitokeza kundi ndani ya CCM lililokuwa likiendesha kampeni za chini kwa chini za kutaka Rais Samia asipewe nafasi ya kugombea muhula wa pili bila kupingwa ndani ya CCM.
Kundi hili ndio lililokuja na hoja kuwa hii ni awamu ya tano inayomaliza muda wake (2015-2025) na sio awamu ya sita na ndio lilikuja na hoja kuwa kwa vile urais wa Samia haukupitia kura za maoni, basi safari hii ashindanishwe na wengine.
Wala jambo hili si siri kwani Rais Samia mwenyewe akiwaapisha mawaziri aliowateua huko Ikulu, alifichua siri kuwa wapo mawaziri wake walioanza mbio za kuusaka urais uchaguzi mkuu 2025, na akawataka waache mara moja.
Lakini aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka akiwa Unguja Kaskazini huko Zanzibar Agosti 2022 kwenye kongamano, alisema wao CCM watamalizana na Rais Samia 2030 kama utamaduni wao ulivyo.
Januari 2024 akiwa huko Ruangwa, Mkoa wa Lindi tena mbele ya aliyekuwa makamu mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana, Waziri Mkuu aliitaka CCM kutoa fomu moja tu ya urais 2025, kauli ambayo ameirejea mara katika hotuba zake maeneo mengine.
Lakini kwenye mkutano mkuu wa 10 wa CCM Jijini Dodoma, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alimweleza Rais Samia asisikilize porojo za watu kuwa kuna kijana au mzee atagombea urais 2025 akisema ni upuuzi na hamuoni atakayegombea.
Hayo yote yanathibitisha kulikuwa na kundi ndani ya CCM lilikuwa limejipanga vilivyo kumkabili Samia 2025, lakini kwa uamuzi wa mkutano mkuu wa CCM kumteua yeye na Dk Mwinyi hata kabla ya Bunge kuvunjwa, ni goli la Tik-Taka.
Kwa hiyo uamuzi uliofanywa na wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa CCM mwishoni mwa wiki ni kama ‘surprise’ (tendo la kushtukiza) fulani ambalo limeliacha kundi hilo kama limemwagiwa maji na hawaamini kilichotokea.
Kilichofanywa na wajumbe kina faida kubwa sana, mojawapo ni kwamba wamezima ‘uasi wa utamaduni’ wao, lakini sasa wana nafasi ya kujipanga vizuri kuelekea 2025 kwa kuwa hakuna jambo la hatari tena miongoni mwao.
Lakini watambue hii haina maana kundi hilo linaweza kusalimu amri moja kwa moja, bado linaweza kuwa na athari kama litasusa na kuamua kuwa adui wa ndani ya CCM maana ndoto zao zimezimwa kikatili sana.
Nilitangulia kusema goli hili ni kama la Tik-Taka kwa sababu mbili na moja nimeileza kwa kirefu sana, ila sababu ya pili ni kuwa wamevitangulia vyama vya upinzani hatua kadhaa mbele kwani ile kuteua tu wagombea ni goli la kisigino.
Kwa sababu gani, kwa sababu kuanzia sasa, jina la Samia, Dk Mwinyi na Balozi Nchimbi yataendelea kutajwa vinywani mwa watanzania na kutumia fursa hiyo kusahihisha pale ambapo umma utakosoa zaidi, hiyo pekee ni kampeni tosha.
Itapendeza upinzani nao wakija na “surprise” yao kabla ya Bunge kuvunjwa.
Daniel Mjema
