Connect with us

Kitaifa

Ujenzi nyumba za wahudumu wa afya Peramiho waboresha huduma

Songea. Kukamilika kwa ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya wa zahanati ya Kijiji cha Mdunduwaro, Peramiho mkoani Ruvuma, kumewarahisishia wananchi kupata huduma kwa wakati na kuokoa maisha ya wajawazito.

Kabla ya kuwepo nyumba hizo zilizojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), wahudumu wa afya waliishi mbali na ilipo zahanati hiyo, hivyo kusababisha kukosekana kwa huduma kwa baadhi ya siku.

Akizungumzia ujenzi wa nyumba hizo leo Desemba 24, 2024 msimamizi wa zahanati hiyo, Agustino Luhoga amesema kabla ya ujenzi huo huduma zilitolewa kwa muda mfupi.

Amesema ulifika wakati huduma zilikwama kutolewa kutokana na wahudumu kutokuwepo.

Luhoga amesema mgonjwa alilazimika kukodi usafiri ili kumsafirisha mhudumu awahi zahanati hiyo kutoa huduma.

“Baadhi ya wajawazito na wagonjwa walikuwa wanapoteza maisha wakiwa njiani kufuata huduma, lakini kwa sasa watoa huduma wapo hapa, hatuna haja ya kusafiri kwenda mbali, tunashukuru kwa kukamilika kwa ujenzi wa miradi hii ya nyumba za wauguzi na waganga,” amesema Luhoga.

Mtendaji wa kijiji hicho, Zawadi Mlapone amesema mradi wa ujenzi wa nyumba hizo, kisima cha maji na matundu manane ya vyoo umesaidia kuboresha huduma za afya kwenye zahanati hiyo.

Amesema kabla ya kupata nyumba ya waganga wananchi walikuwa wanapata shida ya kupata huduma za afya hasa usiku.

“Wananchi tunashukuru sana na ombi letu kubwa kwa Serikali na Tasaf tusaidiwe gari ya wagonjwa,” amesema.

Awali, Mratibu wa Tasaf Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Hosana Ngunge amesema mradi huo ulianza mwaka jana baada ya kuibuliwa na kuombwa na wananchi.

“Mradi huu umegharimu Sh179 milioni zilizotumika kujenga nyumba mbili za wafanyakazi wa kituo, matundu manane ya vyoo, kuchimba kisima kirefu cha maji na ujenzi wa kichomea taka,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mwalimu Hassan Mtamba amesema kwa sasa Tasaf inatekeleza mradi wa stendi ya mabasi na Zahanati ya Mdundwaro.

Amewataka watumishi wa Serikali, kusimamia vema miradi na fedha zinazotolewa kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi