Kitaifa
Kuporomoka jengo Kariakoo si tukio la kwanza, wataalamu wataja vyanzo
Dar es Salaam. Kuporomoka jengo la ghorofa katika mtaa wa Congo na Mchikichi, eneo la Kariakoo leo Novemba 16, 2024 kumeamsha kumbukumbu za matukio mengine ya aina hii nchini, huku wataalamu wakiainisha vyanzo vya matukio hayo na nama ya kuviepuka.
Kwa mujibu wa wataalamu waliozungumza na Mwananchi, ukiukwaji wa viwango vya msingi wa jengo na mabadiliko ya matumizi ya jengo husika ni baadhi ya sababu za kuanguka kwa majengo hayo.
Mwaka 2006 jengo liliporomoka eneo la Chang’ombe, Dar es Salaam na kuua watu wanne. Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa alitoa maagizo watu wawajibishwe kwa uzembe uliojitokeza.
Juni 21, 2008 ghorofa jipya lililokuwa linajengwa mitaa ya Mtendeni na Kisutu lilianguka na kuangukia jengo dogo walimokuwa wakiishi watu.
Machi 29, 2013 jengo la ghorofa 16 katika makutano ya barabara za Zanaki na Indira Ghandi lilianguka na kusababisha vifo vya watu 36, sababu ya kuporomoka ikitajwa kuwa ujenzi usiozingatia utaalamu.
Kutokana na matukio hayo, kampuni ya Design Plus Architects (DPA) ilipewa zabuni ya kukagua majengo Manispaa ya Ilala kuona usalama wake na Novemba 5, 2013, ilitoa ripoti kuwa kati ya maghorofa 90 yaliyokaguliwa, 67 yalikuwa yamejengwa kinyume cha sheria.
Kampuni hiyo ilisema baadhi ya majengo hayo yanaweza kuporomoka kutokana na ujenzi wake kuwa chini ya kiwango.
Nje ya Dar es Salaam, Desemba 19, 2022 watu watano walifariki dunia na wengine tisa walijaruhiwa baada ya kuangukiwa na jengo la ghorofa mbili lililokuwa linaendelea kujengwa, katika Kijiji cha Sembeti, Marangu mkoani Kilimanjaro. Kulikuwa na mafundi na vibarua wapatao 30.
Kwa upande wa Zanzibar Januari 25, 2017 jengo moja katika Mtaa wa Hurumzi, Unguja lilianguka wakati mafundi wakilifanyia ukarabati. Fundi mmoja alifariki dunia na wengine kujeruhiwa.
Kauli ya Profesa Tibaijuka
Kufuatia ajali hiyo, aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), Profesa Anna Tibaijuka, kupitia mtandao wa kijamii wa X ameandika:
“Kwa sheria za mipango miji ilitakiwa viwanja vinne vya ‘high density’ viunganishwe mbele na nyuma kipatikane kiwanja kimoja kikubwa cha kujenga ghorofa imara yenye ‘basement’ kubwa kupaki magari. Ghorofa inayofunguka kwenye mtaa wa mbele na nyuma awali katika awamu ya tatu ushauri huo wa wataalamu wa mipango miji ulishapuuzwa na viongozi kwa presha ya wawekezaji, kwa hiyo maghorofa Kariakoo na kwingineko yanajengwa kiholela kwenye viwanja visivyokidhi vigezo.
“Pamoja na madhaifu ya usimamizi wa ujenzi kiuhandisi ni vigumu majengo kuwa imara bila kuwa na eneo la kutosha kujenga kitako yaani ‘base foundation’ stahiki. “Naendelea kuhimiza kurekebisha kosa hilo. Sasa tunavuna hasara kubwa ya upotevu wa mali, maisha na fursa za ajira na aibu ya kushindwa kusimamia viwango vya ujenzi miaka 63 baada ya uhuru. Naendelea kushauri viwango vya ‘vertical development’ vizingatiwe kuanzia sasa. Tujisahihishe.”
Mtazamo mwingine
Kwa mtazamo mwingine wa kitaalamu, msingi wa ghorofa unapaswa kujengwa kuhimili uzito wa jengo na vitakavyofanyika ndani yake, ikifanyika kinyume chake lazima litaanguka.
Inaelezwa baadhi ya maghorofa yamejengwa kwa matumizi ya hoteli na makazi, lakini yamebadilishwa matumizi na kuhifadhi mizigo, jambo linaloweza kusababisha kuporomoka.
Akizungumza na Mwananchi Novemba 16, 2024, Mhandisi wa Ujenzi, Joseph Rwihura amesema ukiukwaji wa viwango vya msingi wa ghorofa inaweza kuwa sababu ya kuporomoka.
Amesema ujenzi wa ghorofa huanza na msingi unaojengwa kwa uimara kwa kuzingatia idadi ya ghorofa zitakazobebwa na jengo.
“Kama jengo litakuwa na ghorofa mbili, basi msingi utajengwa kwa uimara utakaomudu kubeba ghorofa mbili. Kwa bahati mbaya majengo mengi Kariakoo, misingi yake imejengwa kubeba kiwango fulani cha ghorofa, lakini mahitaji yanasababisha watu wanaongeza ghorofa juu ya jengo,” amesema.
Katika mazingira hayo, amesema msingi huelemewa na hatimaye jengo kuporomoka.
Kubadilishwa matumizi ya jengo ni sababu nyingine akieleza kwa uhalisia wa Kariakoo, majengo mengi yalijengwa kuwa makazi ya watu na hoteli, lakini yanatumika kuhifadhi mizigo zikiwemo mashine na mitambo.
“Jengo lililojengwa kwa matumizi ya makazi, halipaswi kutumiwa kuhifadhi mtambo au mizigo. Ukifanya hivyo linazidiwa uwezo na utafika wakati litaanguka,” amesema.
ERB yatoa neno
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bernard Kavishe amesema kwa taarifa alizonazo jengo hilo limeshatumika kwa zaidi ya miaka 10.
Kwa sababu ya mazingira ya sasa, amesema ni mapema kujua sababu ya kuanguka kwake na hata kujua iwapo limesajiliwa au la.
“Baada ya siku mbili nitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kujua kama ni miongoni mwa majengo tuliyoyasajili au vinginevyo. Nasi tunafanya uchunguzi baada ya muda tutatoa taarifa rasmi juu ya sababu ya jengo hilo kuanguka,” amesema.
Hata hivyo, amesema kwa uzoefu wake sababu za kuanguka kwa jengo hilo, inaweza kuwa msingi dhaifu.
Kavishe amesema jengo hujengwa juu ya ardhi hivyo, ujenzi wake unapaswa kuwa na msingi utakaohimili uzito wa jengo husika, na shughuli zitakazofanyika ndani yake.
“Kabla ya ujenzi wa msingi kunafanyika vipimo vya udongo kujua kama eneo linaweza kuhimili jengo la namna gani, kisha msingi utajengwa kwa uimara unaozingatia uzito wa jengo na matumizi yake,” amesema.
Kavishe amesema jengo pia linapaswa kujengwa kuhimili mazingira ya asili, ukiwemo upepo, tetemeko la ardhi na majanga mengine.
“Kama kuna kimojawapo kati ya hivyo kimekwenda ndivyo sivyo, basi linaweza likadondoka,” amesema.
Uhai wa ghorofa
Msajili huyo amesema jengo la ghorofa huduma kwa miaka hadi 50 bila kuharibika na baada ya hapo, ndipo linaweza kuchoka.
Hata hivyo, umri wa jengo la ghorofa wakati mwingine, amesema unategemea na namna linavyotunzwa.
“Kama kunafanyika mabadiliko ya mara kwa mara katika jengo, unaweza kugusa nguzo kuu au eneo lolote ukaathiri uimara wa jengo na hatimaye likaanguka kabla ya umri wake,” amesema.
Sababu nyingine ya jengo kuporomoka amesema ni mabadiliko ya shughuli za karibu na jengo husika.
Kavishe amesema kama nje ya jengo hakukuwa na mtaro na baadaye ukachimbwa, inaweza kuathiri. Amesema hata ikitokea kumechimbwa handaki ni hatari nyingine kwa usalama wa jengo.
Mhandisi aliyeomba hifadhi ya jina lake kutokana na masharti ya ajira yake, amesema wizi wa saruji na nondo wakati wa ujenzi ni sababu nyingine ya majengo kuporomka.
“Kwa ufupi wanaamua kulipua ilimradi kazi iishe. Jengo linakosa ufanisi ndani ya muda mfupi linaanguka,” amesema.
Pia, amesema vifaa vilivyotumika wakati wa ujenzi wa msingi ni sababu nyingine, akieleza msingi imara wa jengo la ghorofa ni ule unaojengwa kwa mawe mazito na eneo unapojengewa hakupaswi kuwa na asili ya unyevunyevu au chemchem.