Kitaifa
Sababu tatu kupanda nauli za boti Dar-Zanzibar
Unguja. Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA), imetaja sababu tatu za kupandisha bei ya nauli ya boti za mwendokasi zinazofanya safari zake kati ya Unguja na Dar es Salaam.
Nauli hiyo imeongezwa katika huduma hiyo kwa daraja la kawaida kutoka Sh30,000 hadi Sh35,000.
Sababu hizo ni kuongeza kwa gharama za mafuta, matumizi ya Dola ya Marekani, kuongezeka kwa gharama za matengenezo na utawala, ambapo mchakato wa kupandisha ulianza Juni hadi Septemba 2024.
Mara ya mwisho kupanda kwa nauli hizo ilikuwa Mei 19, 2022, ambapo ilipanda hadi Sh30,000 kutoka Sh25,000 iliyodumu kwa miaka saba, licha ya bei ya mafuta kupanda na kushuka kwa nyakati tofauti.
Nauli hizo mpya zilizoanza kutumika hivi karibuni zimewaweka wakati mgumu watumiaji wa usafiri huo wasiokuwa na taarifa kuhusu kupanda kwa gharama hizo. Baadhi yao waliofika katika kituo cha kukata tiketi walijikuta wakipigwa na butwaa baada ya kuelezwa na watoa huduma kuhusu ongezeko hilo.
Hivi karibuni Mwananchi lilishuhudia mmoja wa abiria, aliyekuwa na mpango wa kusafiri kwenda Zanzibar kutoka Dar es Salaam, kujikuta katika mazingira magumu baada ya kueleza ana Sh30,000 ya nauli na hana taarifa za nauli mpya.
“Naomba unisaidie naongeza Sh3000 jumla Sh33,000 sina Sh2000 nisaidie,” aliomba abiria huyo, hata hivyo mtoa huduma (mkatisha tiketi), alimueleza haiwezekani.
Hata hivyo, bei za Unguja kwenda Pemba zimebaki zilezile ya Sh35,000. Meli kubwa nauli zake ni Sh20,000 daraja la chini na daraja la kati Sh25,000
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Novemba 6, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa ZMA, Mtumwa Said Sandar amethibitisha kupanda kwa nauli hizo, akisema kampuni za boti hizo zilifuata taratibu zote kwa kuwasilisha maombi yao katika mamlaka husika.
“Juni, 2024, ZMA ilipokea maombi ya kufanya mapitio na kupandisha bei za tiketi kutoka kwa kampuni zenye boti za mwendo kasi zinazofanya safari zake kati ya Zanzibar na Dar es Salaam, ili kuendana na uhalisia wa gharama za uendeshaji ikilinganishwa na bei halisi za abiria zinazotozwa kwa sasa.
“Katika kuyafanyia kazi mapendekezo hayo, Serikali kupitia mamlaka zake zote muhimu ilianza kufanya mazungumzo na wamiliki wa kampuni hizo,” amesema Sandar
Kwa mujibu wa Sandar, walifanya uchambuzi wa kina hoja za msingi zilizowasukuma kuwasilisha maombi ya kuongeza bei ya tiketi ili kuangalia namna bora ya mapendekezo yao na uhalisia uliokuwepo katika uendeshaji.
Sandar amesema katika mapendekezo ya kuongeza bei ya tiketi yaliyowasilishwa na kampuni hizo yaliegemea kwenye baadhi ya hoja za kuongezeka kwa gharama za bei ya mafuta.
Amesema kampuni zilieleza bei ya nauli kwa tiketi ya Sh30,000 kwa daraja la chini ilitangazwa mwaka 2022 ambapo kwa wakati huo bei ya mafuta ilikuwa ni Sh2,500 ikilinganishwa na mwaka huu 2024 ambapo imekuwa Sh3,020 kwa lita.
Amefafanua ongezeko hilo limesababisha gharama za uendeshaji kuongezeka kwa asilimia 21 na bei ya tiketi imeendelea kubakia ileile.
Sandar amesema kampuni za usafiri baharini kwa kawaida zimekuwa zikilipa kodi, kununua vifaa pamoja na kufanya matengenezo ya vyombo vyao kwa kutumia Dola ya Marekani badala ya Shilingi ya Tanzania.
Kwa mwaka 2022, Dola ilikuwa sawa na Sh2,330 ambapo kwa mwaka huu 2024, Dola moja ni sawa Sh2,850 katika soko la kawaida ambayo hufanya ongezeko la asilimia 22 ya uendeshaji.
“Kampuni zimekuwa zikilipa kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Dola badala ya Shilingi za Kitanzania jambo linalosababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji.”
“Sababu nyingine ni kuongezeka gharama za matengenezo na utawala. Kampuni zililalamika kuongezeka kwa gharama za matengenezo ya vyombo kwa kipindi hiki ambacho Dola imepanda ikilinganishwa na bei ya abiria kubakia kama ilivyo kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita,” amesema.
Amesema Serikali ilizijadili hoja hizo pamoja na kuzifanyia uchambuzi taarifa zote za kifedha za uendeshaji za kampuni hizo na kubaini kwa kiasi haziendani na bei halisi iliyokuwa ikitozwa hapo awali ya Sh30,000.
“Kwa kuzingatia matokeo hayo Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Zanzibar iliridhia kuruhusu kupandishwa nauli za boti za mwendokasi kutoka Sh30,000 hadi Sh35,000 kwa daraja la chini,” amesema Sandar.
Sandar amesema nauli kwa madaraja mengine zinaendelea kuwa kama zilivyokuwa awali.
Licha ya jitihada za Mwananchi kuwatafuta wamiliki wa boti hizo, lakini katika ofisi zao za utoaji wa huduma wa tiketi na usafirishaji mizigo wameweka tangazo kwenye mbao za matangazo, linalowataarifu abiria kuhusu kupanda kwa nauli hiyo.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza maeneo mengine ambayo wananchi wanatumia usafiri wa majini kutoka sehemu moja kwenda nyingine ikiwemo katika maziwa, nauli hazijapanda.