Connect with us

Kitaifa

Dosari zipatiwe ufumbuzi kuelekea uteuzi wa wagombea

Dar es Salaam. Uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27, 2024, unatoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wa ngazi ya mitaa, vijiji, na vitongoji.

Mchakato huu ni muhimu kwa kuwa unaimarisha utawala wa kidemokrasia na kuleta uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi.

Hata hivyo, kuelekea uteuzi wa wagombea Novemba 8, 2024 kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kuathiri mwenendo mzima wa uchaguzi na uwakilishi wa haki.

Mojawapo ya changamoto zinazolalamikiwa na baadhi ya vyama ni kutokuwapo kwa baadhi ya maofisa wa uchaguzi wakati wa urejeshaji wa fomu, mchakato uliofikia tamati Novemba mosi.

Ili kuhakikisha uchaguzi unaenda vyema ni vyema vyama, wagombea na maofisa wa uchaguzi kuhakikisha kanuni na sheria zinafuatwa.

Viongozi wa vyama vya siasa wana jukumu la kuongoza na kudhibiti mchakato huu kwa njia yenye kujali masilahi ya wananchi na maendeleo ya nchi.

Mbinu na hatua ambazo zinapaswa kutumiwa na viongozi wa vyama vya siasa ili kufanikisha uchaguzi wa serikali za mitaa kwa amani na utulivu ni ushirikiano na mawasiliano ya wazi, na si hizi za kibababishaji zinazopalilia mgawanyiko.

Viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kuanzisha na kudumisha ushirikiano mzuri na wadau wote wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), mashirika ya kiraia, na wawakilishi wa Serikali.

Mawasiliano ya wazi na ya mara kwa mara yatasaidia kupunguza kutokuelewana na migogoro inayolalamikiwa na inayoweza kutokea.

Kila chama kinapaswa kushirikiana na wadau wengine kutoa maoni na mapendekezo juu ya taratibu za uchaguzi na kuhakikisha kuwa haki za wagombea zinaheshimiwa na wahusika wasikilize na kufanyia kazi.

Mbali ya vyama, wagombea wanapaswa kufahamu taratibu za kuwasilisha malalamiko, katika hili ni muhimu kuhakikisha mwongozo na kanuni za uchaguzi zinafuatwa.

Wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi kwa upande wao wana jukumu la kuhakikisha hawawi chanzo cha kuvuruga uchaguzi, wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Ile dhamira ya kuimarisha demokrasia na utawala bora nchini iliyoonyeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia falsafa ya 4R, si tu  inapaswa kutekelezwa, bali inapaswa kuonekana inavyotekelezwa.

Falsafa hiyo inahusisha mageuzi ya kiutawala na kisiasa ili kuhakikisha Tanzania inaendeshwa kwa misingi ya haki, uwazi, na uwajibikaji.

Kwa muktadha wa uchaguzi wa serikali za mitaa, 4R za Rais Samia zina uhusiano wa moja kwa moja na suala la kuhakikisha unakuwa huru na wa haki kwa maana ya kuwepo maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya pale wadau walipobomoa baada ya kuhitiliafiana.

Kwa jamii inayozingatia falsafa hiyo, tusingetarajia kuona aina malalamiko tunayoyasikia au la, kama yangekuwepo tungesikia majibu yake na suluhisho la haraka.

Mbali na hilo, matarajio ya wengi ni kuona kuna maridhiano hasa katika kipindi cha mvutano wa kisiasa. Katika uchaguzi wa serikali za mitaa, maridhiano yanahitajika ili kuhakikisha vyama vya siasa, wapigakura na wadau wengine wanashiriki kwa amani na katijka uwanja ulio sawa.

Kwenye hali ya kisiasa iliyotulia, maridhiano ni sharti la msingi kwa uchaguzi huru, kwani inaruhusu kila mshiriki kujieleza bila hofu ya kubaguliwa wala kushambuliwa.

Ustahimilivu

Vilevile, mifumo ya kisiasa inapaswa kuweka mazingira ya kuhimili changamoto na kushikilia misingi ya demokrasia, hata katika mazingira magumu.

Hapa tunazungumzia watu binafsi, taasisi za uchaguzi, vyama vya siasa na vyombo vya usalama, ili kuhakikisha kuwa vinaweza kusimamia uchaguzi kwa njia huru na ya haki.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa, ustahimilivu wa kila upande na kila mdau ni muhimu sana.

Ni lazima Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) iwe na uwezo wa kusimamia uchaguzi kwa njia isiyoegemea upande wowote, kuhakikisha kuwa taratibu zote zinafuatwa na kushughulikia malalamiko au changamoto zozote zinazojitokeza.

Hii ni pamoja na kuimarisha mafunzo kwa maofisa wa uchaguzi ili watekeleze majukumu yao kwa weledi bila upande wala kuamrishwa na mtu au mamlaka yoyote.

Ustahimilivu pia unahusisha nia na uwezo wa vyombo vya usalama kuwalinda wapigakura na wagombea wakati wa uchaguzi.

Katika historia ya Tanzania, kuna nyakati ambazo uchaguzi wa serikali za mitaa umekumbwa na vurugu na vitisho, hasa katika maeneo yenye ushindani mkubwa wa kisiasa. Kupitia 4R, tunaona umuhimu wa vyombo vya usalama kutekeleza wajibu wake kwa njia isiyopendelea upande wowote, kuhakikisha kuwa wananchi wanapiga kura kwa uhuru na kwa amani, kura zao zinalindwa na maamuzi yao yanaheshimiwa.

Mageuzi

Uchaguzi ni si jambo jipya, umekuwepo na umekuwa kama wa kihistoria. Bahati mbaya hata malalamiko tunayosikia sasa yamekuwepo pia kwa miaka mingi, hivyo 4R katika eneo hilo inaangazia umuhimu wa kufanya mageuzi ili kuhakikisha uchaguzi huu na ule ujao unakuwa huru na wa haki.

Mageuzi haya yanahusu kuboresha mfumo wa uchaguzi na sheria zinazohusiana na uchaguzi ili kuondoa vikwazo vinavyoweza kuvuruga utekelezaji wa kidemokrasia.

Mathalani, mabadiliko yamefanywa ili kuhakikisha wapigakura wanavifikia vituo vya kupigia kura kwa urahisi zaidi na kwamba, taarifa kuhusu wagombea zinapatikana kwa wananchi kwa uwazi, kura zinahesabiwa na kulindwa na matokeo yanatangazwa na kuaminika.

Mageuzi haya pia yanahusu kuimarisha mifumo ya kiufundi inayotumika katika uchaguzi, kama vile uandikishaji wa wapigakura kwa njia ya elektroniki, kuhakiki na ikiwezekana upigaji kura wa kidijiti.

Mfumo huu unasaidia kuhakikisha kila raia aliye na sifa anapata fursa ya kupiga kura na kupunguza uwezekano wa udanganyifu au dosari zinazoweza kuvuruga matokeo ya uchaguzi.

Aidha, mageuzi katika utoaji elimu ya uraia na haki za kupiga kura yanachangia kuongeza idadi ya wapiga kura, hasa katika maeneo ya vijijini ambako uelewa wa mchakato wa uchaguzi unaweza kuwa mdogo.

Katika eneo hili pia kuna umuhimu wa elimu ya uraia kama njia ya kuwawezesha wananchi kuelewa haki zao na umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kujenga upya

Sehemu ya nne ya 4R ni kujenga upya ambayo inahusu kuimarisha hadhi ya Tanzania kimataifa kupitia uchaguzi huru na wa haki.

Rais Samia ametambua kuwa dunia inaitazama Tanzania kama moja ya mifano ya demokrasia barani Afrika na kwamba, kuendesha uchaguzi wa serikali za mitaa kwa uadilifu ni hatua muhimu ya kudumisha sifa hiyo, tofauti na ambavyo iliwahi kuiona huko nyuma.

Sifa njema ya Tanzania katika masuala ya uchaguzi ni muhimu kwa sababu inavutia uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa.

Uchaguzi ambao unafanyika kwa uwazi na kwa kufuata sheria unatoa ishara kwa jamii ya kimataifa kuwa Tanzania inaweza kuheshimu misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.

Hii inachangia kuimarisha uhusiano wa kimataifa na kuvutia misaada ya maendeleo ambayo inaweza kusaidia kuboresha maisha ya wananchi.

Hii inajumuisha kuhakikisha kuwa, kuna ushiriki wa kutosha wa waangalizi wa kimataifa na wa ndani, ambao wanaweza kuthibitisha uwazi na haki ya mchakato wa uchaguzi.

Hali hii ina uhusiano wa moja kwa moja na suala la kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa unakuwa huru na wa haki.

Kwa ufupi ni kwamba kupitia maridhiano, Rais Samia ameleta umoja na utulivu wa kisiasa, ambao ni muhimu kwa uchaguzi ulio huru.

Ustahimilivu umeimarisha taasisi za uchaguzi na vyombo vya usalama, kuhakikisha kuwa vinaweza kusimamia uchaguzi kwa haki na uadilifu.

Mageuzi yameongeza uwazi na ushiriki wa wananchi na sifa njema imeweka msingi wa Tanzania kuendelea kuheshimiwa kimataifa kama nchi inayothamini demokrasia.

Kupitia utekelezaji wa 4R, Rais Samia anajenga msingi imara wa demokrasia nchini, kuhakikishe uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika kwa njia ya haki na kuwa matokeo yake yanawakilisha matakwa halisi ya wananchi.

Ni kupitia uchaguzi huru na wa haki, Tanzania itaendelea kuwa na viongozi wa mitaa wanaochaguliwa kwa ridhaa ya wananchi na wanaowajibika kwa maendeleo ya jamii zao.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi