Connect with us

Kitaifa

BoT yaondoa hofu uhaba fedha za kigeni

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewaondoa hofu wananchi kuhusu upatikanaji wa fedha za kigeni huku ikisema imeimarika katika kipindi cha Julai hadi Septemba, mwaka huu.

Imesema kuimarika huko kulikwenda sambamba na msimu wa shughuli za utalii na mauzo ya mazao ya kilimo na biashara nje ya nchi.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alisema jana jijini hapa kuwa kutokana na mwenendo huo, kasi ya kuporomoka kwa thamani ya shilingi ilipungua hadi kufikia asilimia 10.1 kwa mwaka unaoishia Septemba 2024, kutoka asilimia 12.5 kwa mwaka ulioshia Juni 2024,” alisema.

 

 

Alibainisha kuwa akiba ya fedha za kigeni iliongezeka kufikia dola za Marekani milioni 5,413.6 mwishoni mwa Septemba kutoka dola za Marekani milioni 5,345.5  Juni, mwaka huu na kwamba kiasi hicho kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa zaidi ya miezi minne.

Tutuba alisema hali hiyo inatarajiwa kuimarika kutokana na ongezeko la bei ya dhahabu kwenye soko la dunia, shughuli za utalii na mauzo ya bidhaa asilia kama korosho, tumbaku, kahawa na pamba.

Pia alisema mauzo ya mazao ya chakula hususan mahindi na mchele kwenda nchi jirani, pia yanatarajiwa kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

“Kupungua kwa uagizaji wa mbolea na kupungua kwa bei za bidhaa za mafuta ya nishati kunatarajiwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni na matakwa ya kisheria kuhusu kunukuu na kufanya malipo ya ndani kwa shilingi ya Tanzania yanatarajiwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni nchini na kuongeza ufanisi wa sera ya fedha,” alisema.

Alisema mpango wa ununuzi wa dhahabu katika soko la ndani kwa kutumia Shilingi ya Tanzania utaongeza akiba ya fedha za kigeni.

 

RIBA YA BENKI

Gavana Tutuba alisema Kamati ya Sera ya Fedha ya BoT imeamua riba ya benki ya asilimia sita iliyodumu kuanzia Aprili mwaka huu iendelee kwa robo mwaka itakayoishia Desemba, mwaka huu.

Aidha, alisema sababu zilizochangia riba ya Benki Kuu (CBR) kwa robo ya mwisho ya mwaka 2024 kubaki asilimia sita kuwa ni pamoja na kukua kwa uchumi nchini na duniani huku ikitarajiwa kuwapo na ongezeko la upatikanaji wa fedha za kigeni.

“Uamuzi huu ulitokana na matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kuwa chini ya lengo la nchi la asilimia tano. Kamati pia inatarajia uchumi kuendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha, sambamba na kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi duniani na hapa nchini,” alisema.

Alisema uchumi wa dunia unatarajiwa kuendelea kukua sambamba na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha na kutokana na hali hiyo, Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia wanakadiria uchumi wa dunia kukua kwa asilimia 3.2 na asilimia 2.6, mtawalia mwaka 2024.

Mwenendo huo, alisema unatarajiwa kuchagiza shughuli za uzalishaji hapa nchini na mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kupungua, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi sambamba na kupungua kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mafuta na mbolea.

“Katika robo ya mwaka inayoishia Desemba 2024, bei za mafuta ghafi zinatarajiwa kuwa kati ya dola za Marekani 72 hadi 82 kwa pipa, kutokana na ongezeko la uzalishaji. Hali hii inatarajiwa kupunguza ongezeko la mfumuko wa bei na mahitaji ya fedha za kigeni nchini kwa kuwa bidhaa za mafuta huchangia takriban asilimia 20 ya bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje ya nchi,” alisema.

 

 

KUKUA UCHUMI

Tutuba alisema katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, uchumi ulikua kwa asilimia 5.6, huku shughuli za ujenzi, kilimo, fedha na bima, na usafirishaji zikichangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji huu.

“Kwa mujibu wa viashiria vya awali, uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 5.8 na asilimia 5.6 katika robo ya pili na ya tatu ya mwaka 2024, mtawalia na unatarajiwa kuendelea kukua katika viwango hivyo katika robo ya mwisho wa mwaka,” alisema Tutuba.

Hata hivyo, alisema kuendelea kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi nchini kunatokana na maboresho katika biashara na uwekezaji, ikiwamo yanayoendelea kutekelezwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

“Uzalishaji katika shughuli za kilimo unatarajiwa kuongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na matumizi ya pembejeo (mbolea na mbegu bora), viwatilifu na uwekezaji katika miradi ya umwagiliaji, shughuli za ujenzi na usafirishaji zinatarajiwa kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, alisema.

 

MIKOPO CHECHEFU

Gavana Tutuba alisema mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka kwa kasi ya kuridhisha ikiwa ni takriban asilimia 17.1 kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2024 na ubora wa rasilimali za benki umeongezeka ambapo uwiano wa mikopo chechefu ulipungua hadi asilimia 3.9 mwezi Agosti 2024, kutoka asilimia 5.1 katika mwezi kama huo mwaka 2023.

 

DENI LA TAIFA

Alisema Deni la Taifa limefikia dola za Marekani milioni 37,721.6, sawa na asilimia 46.9 ya Pato la Taifa (GDP), ambalo ni chini ya kigezo cha mtangamano wa kiuchumi cha ukomo wa asilimia 60 kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Aidha, alisema uwiano wa deni kwa Pato la Taifa, kwa thamani halisi ya sasa (NPV) ulikuwa asilimia 36.4 mwaka 2023/24, chini ya kigezo cha mtangamano wa kiuchumi cha ukomo wa asilimia 50 kwa EAC.

Pia alisema kupungua kwa athari za mitikisiko ya kiuchumi duniani nakisi ya urari wa malipo ya kawaida inakadiriwa kupungua hadi kufikia asilimia 3.2 kutoka 4.4 kwa kipindi kama hicho mwaka 2023.

“Mwenendo huu ulitokana na ongezeko la mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi, hususan utalii, dhahabu, tumbaku na korosho. Nakisi ya urari wa malipo ya kawaida inatarajiwa kuendelea kuimarika na hivyo kusaidia kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni nchini,” alisema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi