Connect with us

Makala

Hizi hapa mila za ajabu barani Afrika

Je, umewahi kusikia mila ya kuiba mke kwenye sherehe au mila ya kupima urijali wa bwana harusi na mila ya kupigwa ili uoe, hizo ni baadhi ya mila, tamaduni na desturi za kipekee zinazopatikana ndani ya Bara la Afrika.

Utamaduni, mila, na desturi za makabila mbalimbali ndani ya Afrika ni hazina inayowasaidia Waafrika kudumisha utambulisho wao, kuimarisha mshikamano wa kijamii, na kuhifadhi urithi wa kizazi hadi kizazi.

Mila hizi za kipekee, pia hutumika katika kuboresha maisha kwa nyanja zote za afya, uchumi, hadi uhusiano wa kijamii na zimekuwepo kwa vizazi vingi.

Hata hivyo, baadhi ya mila hizo sio tu zinashangaza, zipo zinazoenda hata kinyume na utu wa wanajamii. Makala haya yanaangazia baadhi tu ya mila za ajabu barani Afrika.

Mila ya kuiba mke usiku – Wodaabe, Afrika Magharibi

Kabila la Wodaabe, linalopatikana kaskazini mwa Nigeria, kusini mwa Cameroon, na Chad, lina mila ya pekee inayojulikana kama “kuiba mke.”

Katika sherehe za kimila, jamii ya Wodaabe hujumuika kwenye ngoma za usiku, ambapo wanaume wanaruhusiwa kumchagua mwanamke yeyote wa jamii yao na kumpeleka kustarehe naye kwa usiku mmoja.

Kitendo hiki hakijalishi ikiwa mwanamke ameolewa au la, ilimradi mwanamke huyo asiwe na pingamizi na achague kuridhia tendo hilo.

Mila hii, ambayo inaonekana kinyume na taratibu za ndoa za jadi, inaendelea kufuatwa na jamii hii licha ya changamoto za kisasa.

 

Kupima urijali wa bwana harusi – Banyankole, Uganda

Kabila la Banyankole nchini Uganda lina mila inayohusisha kipimo cha urijali wa bwana harusi.

Pia, mila hiyo inampa shangazi jukumu la kuhakikisha kwamba binti anayeingia umri wa miaka minane,  anaitunza bikra yake.

Binti anapochumbiwa, pia shangazi anabeba jukumu lingine la kushiriki tendo la ndoa na bwana harusi mtarajiwa ili kuhakikisha kuwa ni rijali na ana uwezo wa kumridhisha mke wake.

Mila hii inaonekana kuwa ya ajabu kwa jamii nyingi duniani, lakini ni muhimu katika jamii ya Banyankole kwa kuwa inatoa uhakika wa ndoa yenye mafanikio.

Katika hali hii, baadhi ya wazee wa kabila hilo wanaamini kwamba si lazima shangazi aingiliwe kimwili, bali anapaswa kupewa nafasi ya kusikiliza na kutazama kinachoendelea wakati wanandoa hao wanaposhiriki katika tendo la ndoa.

Pia, mila nyingine nchini Uganda zina utaratibu wa kusikiliza kwa siri tendo la ndoa la bwana na bibi harusi baada ya harusi, kuangalia kama kila kitu kiko sawa.

 

Kuruka kundi la ng’ombe – Hamar, Ethiopia

Katika jamii ya Hamar nchini Ethiopia, vijana wanaotaka kuingia katika utu uzima na kufuzu kuwa watu wazima,  hupitia jaribio maalumu la kuruka kundi la ng’ombe.

Ng’ombe hao hupangwa katika mstari huku kijana akivua nguo zote na kuruka juu yao akiwa uchi.

Jaribio hili linafanyika mbele ya jamii nzima na ni ishara ya kuwa tayari kuanza maisha ya kifamilia.

Vijana wanaofanikiwa kuruka kundi la ng’ombe hupongezwa na marafiki zao wa kike, ambao hucheza ngoma na kufurahia tukio hilo la kihistoria.

Hii ni moja ya mila muhimu kwa jamii ya Hamar, ambayo inaunganisha ujasiri wa kijana na heshima ya kuanza maisha mapya.

 

Kipigo ili  kuoa – Fulani, Benin

Katika jamii ya Fulani nchini Benin, wanaume ambao wanataka kuoa hupitia jaribio la kimwili linalojulikana kama “Sharo.”

Katika jaribio hili, mwanaume anatakiwa kuvumilia kipigo kutoka kwa wazee wa jamii kabla ya kupewa ruhusa ya kuoa.

Jaribio hili linaonekana kuwa na lengo la kupima uvumilivu wa mwanaume na uwezo wake wa kukabiliana na changamoto za ndoa.

Endapo mwanaume atashindwa kuvumilia kipigo hicho, harusi huvunjwa na inakuwa aibu kubwa kwake na familia yake.

Mila hii, ingawa inaonekana kuwa ya kikatili kwa mtazamo wa nje, ina lengo la kumfanya mwanaume kuwa na uwezo wa kuvumilia changamoto za maisha ya ndoa.

 

Mazishi ya siri – Chewa, Malawi

Katika kabila la Chewa nchini Malawi, mila za mazishi ni za kipekee na zenye siri kubwa.

Sherehe za mazishi zinahusisha utaratibu unaojulikana kama “Nyau,” ambapo watu huvaa kifaa maalumu na kufunika nyuso zao wakati wa mazishi.

Utaratibu huu inaaminika unalenga kuzuia mawasiliano ya moja kwa moja na roho za wafu.

Pia, mwili wa marehemu huoshwa kwa maji maalumu, na maji hayo hutumika kuandaa chakula ambacho huliwa na watu wote waliopo katika mazishi.

Mila hii inaendeshwa kwa siri kali na inaaminika kuwa ni njia ya kuwaaga marehemu kwa heshima kubwa, huku ikilinda jamii kutokana na madhara yanayoweza kuletwa na roho za wafu.

 

Maziko ya usiku kwa Mfalme – Zulu, Afrika Kusini

Kwa jamii ya Zulu nchini Afrika Kusini, mazishi ya kifalme yanafanywa usiku na yanahusisha wanaume pekee kutoka familia ya kifalme.

Mfalme Goodwill Zwelithini, aliyefariki dunia kwa Uviko-19, alizikwa usiku kwa mujibu wa mila za jamii ya Zulu.

Kwa mujibu wa mila hizo, maziko ya mfalme yanatakiwa kufanyika faragha na usiku ikiwamo kuhudhuriwa na wanaume maalum tu.

Sherehe hizi zina lengo la kulinda heshima ya kifalme na kuhakikisha kuwa mfalme anapewa heshima ya mwisho kwa njia ya kimila.

 

Mazishi ya kuketi – Wabukusu, Kenya

Katika jamii ya Wabukusu nchini Kenya, mila za mazishi ni tofauti na zile zinazojulikana katika sehemu nyingi duniani.

Wakati wa maziko, marehemu huzikwa akiwa ameketi, kichwa kikiwa kinaelekea mbali na boma.

Pia, mavazi ya marehemu kama viatu na shati lazima vilegezwe kabla ya kuzikwa.

Hili lilionekana wakati wa janga la Uviko-19, ambapo maofisa wa afya walikuwa wakizika watu haraka bila kufuata mila hizi.

Baada ya kuona ishara za laana katika ndoto zao, wazee wa Wabukusu waliamua kufukua baadhi ya miili na kuizika kwa kufuata mila zao za jadi.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi