Kitaifa
Haya hapa majina waliochaguliwa kujiunga Polisi
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limetangaza majina ya vijana waliochaguliwa kujiunga na jeshi hilo pamoja na tarehe ya kuripoti shuleni.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Jumatatu Septemba 23, 2024 inasema majina ya waliochaguliwa wanatakiwa kuripoti kuanzia Septemba 30, 2024.
“Mkuu wa Jeshi la Polisi anawatangazia vijana wote waliochaguliwa kujiunga na Jeshi la Polisi nchini, wanatakiwa kuripoti Shule ya Polisi Moshi kuanzia tarehe 30/09/2024 hadi tarehe 02/10/2024 kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo.
“Vijana waliofanyiwa usaili Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) na vikosi vilivyo chini ya Makao Makuu ya Polisi wanatakiwa kuripoti Dar es Salaam eneo la Polisi (Barracks) Barabara ya Kilwa karibu na Hospitali Kuu ya Polisi Septemba 30, 2024 kuanzia saa 12.00 asubuhi kwa ajili ya safari ya kwenda Shule ya Polisi Moshi,”inaeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliofanya usaili mikoa ya Tanzania Bara wanatakiwa kuripoti kwa makamanda wa polisi wa mikoa Septemba 29, 2024 saa 2.00 asubuhi kwa ajili ya kupewa utaratibu wa safari ya kwenda Shule ya Polisi Moshi.