Makala
Hivi ndivyo neno ‘dollar’ lilivyozaa daladala
Miji bila daladala hainogi, walijua hilo? Na kwa nini kusiwe na daladala wakati ni ngumu kwa kila mwanamjini kumiliki kipando chake?
Kwa lugha ya vijana isiyo rasmi, usafiri wa daladala ndio mpango mzima, maana haubagui mtu, ni wewe, miguu na pesa yako, hata kama usafiri wenyewe baadhi ya nyakati unakengeuka misingi ya utu.
Tuyaache hayo, tunataka kukueleza asili ya neno daladala kama lilivyobuniwa na wakazi na abiria katika mji wa Dar es Salaam miaka ya zamani.
Ni hivi; miaka hiyo sarafu ya shilingi tano ambayo pia ilijulikana kwa jina la ‘gwala’ kwa waliokosea kutamka dala, thamani yake ilikuwa sawa na dola moja ya Marekani.
Kwa sababu hiyo, sarafu hiyo ikapewa jina la dala, ikiwa ni neno lililokopwa kutoka neno dollar la Kimarekani.
Kilichotokea makondakta walipokuwa wakiita abiria, maarufu kama kupiga debe, walikuwa wakitamka nauli ya mabasi yao kuwa ni dala, au daladala. Huo ukawa mwanzo wa usafiri huo maarufu kuitwa kwa jina la daladala na kusambaa kila kona ya nchi baadaye.
Historia kwa mujibu wa mwenyeji wa mkoa huo, Khamis Mataka, inaonyesha kwa Dar es Salaam daladala zilianza kama usafiri usio rasmi.
Ni sawa na kusema daladala za enzi hizo, hasa magari aina ya Combi, zilikuwa zinaiba ruti.
Aina hiyo ya usafiri ilikuja kurasimishwa baadaye na ndipo watu binafsi walipoanza kuingiza mabasi, yakiwamo ya aina ya coaster.
Awali biashara hiyo ilikuwa imehodhiwa na mabasi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA. Shirika hilo lilikuwa na mabasi makubwa ya kawaida na yale marefu aina ya Ikarus ambayo kwa kuchukua idadi kubwa ya abiria, wakazi wa Dar es Salaam waliyabatiza jina la kumbakumba, likibeba kila aliye kituoni!
Ujio wa mabasi ya watu binafsi hasa magari aina ya coaster miaka ya katikati ya 1980, ukaleta ahueni na nafuu ya ugumu wa usafiri.
Kwa raha ambayo abiria walikuwa wakiipata katika mabasi haya ukilinganisha na mabasi ya Uda na mengineyo yaliyokuwa yamechakaa, watumiaji hawakusita kuyabatiza mabasi jina la ‘vilakshari’, wakimaanisha angalau yalikuwa mabasi yanayowapa raha abiria wake.
Hapo ndipo kwa wale watu wa zamani watakumbuka kibwagizo cha wimbo kisemacho: ‘Kilakshari, kilakshari Pugu Kariakoo’’.
Kwa usafiri wa mikoani ambao mabasi yake hayakuwa na stendi maalumu ukitoa ya Kisutu, iliyokuwa maalumu kwa mabasi ya mikoa ya kaskazini, huduma hiyo ilikuwa ikitolewa na mashirika kama Moretco, Coretco, Kamata na mabasi mengineyo.