Connect with us

Kitaifa

Rita: Bora cheti kiandikwe baba mzazi hajulikani, kuliko jina lisilo asili

Dar es Salaam. Kama una mtoto na hauna uhakika na baba yake halisi au kwa sababu zako hutaki ubini wake utumike kwa mwanao, huna sababu ya kumwandika baba bandia katika cheti cha kuzaliwa.

Kwa mujibu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), kuandika jina la baba asiye wa asili wa mtoto katika cheti cha kuzaliwa ni kosa kisheria.

Badala yake, Rita imeweka wazi, iwapo kuna sintofahamu juu ya baba wa mtoto ni ruhusa katika cheti hicho kuandika baba hajulikani, kuliko kuweka jina la asiyestahili.

Ufafanuzi huo, unakuja katika kipindi ambacho aghalabu wazazi wa kike huandika majina ya wazazi wao (babu wa mtoto), iwapo kuna sintofahamu na wenza wao.

Hata hivyo, kuna ukinzani wa kimtazamo kutoka kwa baadhi ya wananchi, wengine wakiona si muhimu kuandika jina la baba halisi katika cheti cha kuzaliwa cha mtoto, kama hamuhudumii.

Mkazi wa Morogoro, Gadison Jeremiah anasema huu ni mwaka wa sita tangu akose haki ya jina lake kutumika kwenye cheti cha kuzaliwa cha mwanawe, akisema limewekwa la babu mzaa mama.

“Ni mtoto wangu lakini anatumia jina la babu yake, yule mwanamke aliamua kunificha kuhusu mimba, alikuja kuniambia baadaye eti kwamba sikuwa namuhudumia wakati hakunishirikisha,” anasema.

Tukio kama hilo, limemtokea Selemani Sayi, anayeishi mkoani Geita, akisema naye alifichwa kuhusu mimba na mtoto alipozaliwa jina lililoandikwa ni la baba mlezi.

“Alienda kwa yule mwanaume akiwa na mimba yangu changa, alipojifungua alimpa jina la huyo mwanaume, baada ya muda waligombana yule mwanaume akafahamu mtoto si wake, ikabidi amrudishe kwangu.

“Nikimuangalia kweli nafanana naye kila kitu, nimempokea lakini akitumia majina ya yule bwana tayari, hilo limefanya nimchukie zaidi mzazi mwenzangu,” anasema.

Uamuzi wa kuacha kuandika majina ya wazazi halisi katika vyeti hivyo, Janeth Zakayo ambaye binti yake Gladness Zakayo (sio jina lake halisi) anasema unatokana na kukosana na wanaume wao kunakosababisha na huduma duni.

“Nilikuwa mwanafunzi wakati huo, alinikataa nikailea mimba kwa shida, nilipojifungua sikutaka hata kumsikia hadi leo mwanangu hamfahamu baba yake, nimempa jina la babu yake ambaye ni baba yangu mimi,” anasema.

Kauli ya Rita

Ukiachana na ugomvi wenu na mzazi mwezako, Ofisa Usajili wa Rita, Joseph Mwakatobe anasema ni kosa kisheria kuandika jina la mtu asiye baba wa asili wa mtoto katika cheti cha kuzaliwa.

“Hata kama humpendi, mmegombana hamko pamoja tena, lakini huyo ndiye baba halisi wa mtoto, hasira zenu zisimfanye mtoto akose haki yake ya kutambuliwa,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Mwakatobe, kuliko kumpa ubini usio asilia ni bora kwenye cheti cha kuzaliwa kuandikwe baba mzazi hajulikani.

“Inaruhusiwa pale kwenye eneo la baba mzazi, inaandikwa ‘Un Known’ (hajulikani) lakini sio kuandikwa majina ambayo si ya baba asilia wa mtoto,” anasema Mwakatobe.

Anasema mama hawezi kupata mtoto bila baba na baba hawezi kusema nina mtoto bila mama na hata mtoto hawezi kuwa na baba wawili au mama wawili, labda yule ambaye ameasiliwa, lakini kinyume na hapo haiwezekani.

Anasema katika sheria ya mtoto, ana haki ya kutambuliwa na ni kosa kutompa majina halisi ya baba yake asilia.

“Mtoto ana haki ya kumjua baba yake ni nani?  hata kama baba huyo alimkataa, mama anamjua huyo baba na ikitokea mama akambadilisha baba asilia ukampa mwingine ambaye si asili yake ni makosa kisheria,” anasema.

Anasema baba pia hawezi kumkataa mtoto wake, hilo pia ni kosa kama yeye kweli ndiye alitungisha huo ujauzito.

“Huna haki ya kumkataa mtoto kama wewe ndiye uliyemleta, huyo mtoto hakutaka kuja mwenyewe duniani, furaha ya watu wawili ndiyo ilisababisha huyu mtoto kuwepo, yeye hakuomba, si sawa baba kumkataa, sheria ipo wazi na inawalinda hawa watoto,” anasema.

Anasema inapotokea malumbano ya wazazi wawili, ni kosa kukataa kulea mtoto wako na ni kosa kumpa jina la baba mwingine mtoto.

“Mama anapojaza fomu hospitali baada ya kujifungua anakuwa na mazingira ya kutambua haya anayoyafanya na kuna sehemu atasaini kwamba alijaza akiwa na akili timamu na ana haki ya kushitakiwa endapo atakuwa amekwenda kinyume,” anasema.

Anasema ikitokea jina la baba upande wa mama na wa mtoto yanafanana basi ofisa anayechukua maelezo atahoji kwa kina ili kujua undani wa hicho kilichotokea.

“Ni nadra kwamba jina la baba yako na la mzazi mwenzako yafanane, wapo wengine wakibanwa sana wanasema baba wa mtoto alimtelekeza hivyo amempa jina la babu, hii si sawa, kama baba amemkataa mtoto, kwenye cheti andika Hajulikani.”

“Pia kuna mazingira, mtoto ameokotwa, wazazi wake hawajulikani, zile nafasi za majina ya wazazi zitaachwa wazi kwamba hawajulikani, baadaye huko zitajazwa na watu watakaomuasili na kupewa majina ambayo yatamuendeleza hadi mwisho,” anasema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi