Makala
Usichukulie poa, kuna faida katika kutandika kitanda
Dar es Salaam. Hivi unajua kuwa, uimara wa saikolojia yako na mtazamo chanya wa maisha, unajengwa na tabia ya kutandika kitanda mara kwa mara?
Kwa taarifa yako, tabia ya kutandika kitanda pekee inakufanya uwe na hali chanya ya kisaikolojia kwa asilimia 25 zaidi ya yule asiyetandika, utafiti wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania cha Marekani unaonyesha.
Kama ulidhani kutandika kitanda ni jambo la hiari, basi fahamu kuna uhusiano wa jukumu hilo na afya yako ya akili, usingizi bora na hata kuifanya siku yako iwe yenye tija.
Muhtasari huo unajenga msingi wa umuhimu wa tafakuri ya leo Septemba 11, 2024, dunia inapoadhimisha Siku ya Kutandika Kitanda.
Hata hivyo, muhtasari huo unagusa sehemu ya maisha ya vijana wengi hasa wanaume ambao aghalabu, kutandika kitanda si moja ya vipaumbele vya maisha yao.
Tabia hiyo ya vijana inathibitishwa na Denis Msangi, mkazi wa Dar es Salaam, anayesema umuhimu wa kitanda kwake ni kupata eneo la kulala, lakini kutandika huja kwa bahati mbaya.
“Labda kama nina ugeni ambao nina uhakika unaingia chumbani hapo nitatandika, lakini natandika pia kwa zile siku ambazo huwa sina kazi nyingine,” amesema.
Kwa Sophia Nello, mkazi wa jijini Mwanza kutandika kitanda ni jambo analolitekeleza kila siku na hufanya hivyo si kwa kujua faida zake kiafya, bali anatandika kuweka unadhifu wa mazingira ya chumbani kwake.
Ilimradi anapata usingizi wakati wa kulala, Hamidu Shafih anaona kutandika kitanda si muhimu, akidokeza kuwa wanaopaswa kuzingatia kutandika ni wanawake.
Usiyoyajua kuhusu kutandika
Kutandika kitanda kila asubuhi ni ishara ya kuanza siku kwa utaratibu na nidhamu. Hoja hiyo iliwahi kusemwa na Mwanasaikolojia, maarufu William McRaven, ambaye pia alikuwa Kamanda wa Jeshi la Marekani.
Katika moja ya hotuba zake, alisema: “Ukitandika kitanda chako asubuhi, umekamilisha kazi ya kwanza ya siku. Itakupa hali ya kujivunia na kukuza hamasa ya kukamilisha kazi nyingine.”
Mbali na McRaven, utafiti uliofanywa na Shirika la Marekani la National Sleep Foundation, umeonyesha wanaotandika vitanda vyao wanaripoti kuwa na usingizi bora kwa asilimia 19 zaidi kuliko wale wasiofanya hivyo.
Nidhamu ya kuandaa mazingira ya kitanda na usingizi huenda sambamba na ubora wa usingizi, jambo linalohusishwa na kuimarisha afya ya mwili na akili.
Kama hiyo haitoshi, kutandika kitanda kunaweza kuonekana kama jambo dogo, lakini ni hatua ya kwanza kuelekea siku yenye ufanisi.
Sio maneno yangu, ni utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Cornell cha New York nchini Marekani, uliobaini watu wanaoanza siku kwa kufanya kazi ndogo kama kutandika kitanda, wana uwezekano wa kuwa na siku yenye tija kwa asilimia 20 zaidi ikilinganishwa na wasiotandika.
Mbali na faida za kisaikolojia, kutandika kitanda huchangia kwenye usafi wa nyumba na mwili. Kitanda kinapoachwa bila kutandikwa, vumbi na wadudu vinaweza kukusanyika kwa urahisi kwenye mashuka na godoro, hali inayoweza kuathiri afya, ikiwemo mfumo wa upumuaji.
Takwimu kutoka American Academy of Asthma, Allergy & Immunology zinaonyesha asilimia 70 ya wagonjwa wa pumu hupata nafuu kubwa wanapotunza vizuri mazingira ya kitanda, ikiwemo kutandika na kufua mashuka mara kwa mara.
Katika kitabu chake maarufu, The Power of Habit, Charles Duhigg anaeleza jinsi tabia moja nzuri inavyoweza kuwa kichocheo cha mabadiliko makubwa kwenye maisha ya mtu.
Anasema: “Kutandika kitanda ni moja ya tabia za msingi ambazo huweza kusababisha mlolongo wa tabia nyingine nzuri.”
Si hivyo tu, kutandika kitanda husaidia pia kupunguza msongo wa mawazo kwa kujenga hisia za utulivu na mpangilio katika mazingira.
Hilo linathibitishwa na utafiti uliochapishwa katika jarida la Personality and Social Psychology Bulletin, unaoeleza watu wenye mazingira yaliyopangwa vizuri, wakiwemo wanaotandika vitanda, walikuwa na viwango vya chini vya msongo wa mawazo kwa asilimia 15 ikilinganishwa na wasio na utaratibu huo.