Kitaifa
CCM yaomboleza kifo kada wa Chadema, yatoa agizo kwa Polisi
Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimetoa pole kwa Chadema kutokana na kifo cha mjumbe wa sekretarieti, Ali Kibao huku kikilitaka Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wake katika uchunguzi wa tukio hilo.
Mwili wa Kibao ambaye alikuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema uliokotwa maeneo ya Ununio Tegeta, jijini Dar es Salaam. Kisha ulichukuliwa na kupelekwa mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Mwanyamala kuhifadhiwa.
Kibao anadaiwa jioni ya Ijumaa Septemba 6, 2024 maeneo ya Kibo Complex Tegeta akiwa safarini na basi la Tashrif akitoka Dar es Salaam kuelekea mkoani Tanga alishushwa kwenye gari hilo la kuchukuliwa na watu wasiojulikana majina yao wala wanapotokea.
Leo Jumapili 8, 2024 akiwahutubia wananchi wa Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjaro, Mkoa wa Manyara katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Getini, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla ameanza kutoa salamu za pole kwa Chadema na familia ya Kibao kutokana na kifo cha kada huyo.
“Nitoe pole kwa Chadema kwa kumpoteza mmoja wa wajumbe wake wa sekretarieti, nimekuwa nikifuatilia toka asubuhi, sisi ni vyama vya siasa linapokuja suala la ubinadamu, siasa unaweka pembeni.
“Nawapa pole kwa msiba huu mzito wa Kibao, niwaombe Jeshi la Polisi likatimize wajibu wake wa kuendelea na uchunguzi ili tupate taarifa baada ya uchunguzi, katika hili sisi ni vyama vya siasa ni binadamu, utu ndiyo maana nimesimama kwa heshima kubwa kwa niaba CCM natoa pole,” amesema Makalla.
Uchunguzi wa kitabu wa mwili wa Kibao umekwisha kufanyika, mwili umeshakabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za maziko yatakayofanyika kesho saa saba mchana mkoani Tanga. Pia majibu ya uchunguzi wa mwili huo yanatarajiwa kutolewa kesho Jumatatu.