Makala
Yanayoathiri maumbile ya siri ya mwanamke
Mbeya. Baadhi ya wanawake wenye umri kati ya miaka 18 mpaka 35 wako hatarini kiafya kutokana na matumizi ya kemikali, vidonge na vitu vinavyotengenezwa kwa njia asili sehemu zao za siri.
Vitu hivyo ni pamoja na vidonge mbalimbali vinavyochakatwa viwandani kwa bidhaa asili maarufu ‘yoni’, ugoro, shabu na hata wengine kuweka limao wakiwa na malengo ya kurejesha maumbile ya sehemu zao za siri, wakilenga kuongeza mvuto, joto na kuondoa ukavu wakati wa kujamiiana.
Tofauti na matarajio yao, wataalamu wa afya wanasema matumizi ya vitu hivyo huathiri maumbile ya nyama za uke, hivyo kusababisha mtumiaji kupata madhara kiafya.
Miongoni mwa madhara ni kuharibu mji wa mimba, saratani ya viungo vya uzazi, ikiwemo kizazi, shingo ya uzazi na saratani ya uke, UTI sugu, maumivu makali wakati wa kujamiiana na kuathiri uzalishaji chembe chembe za damu zinazozalishwa ukeni.
Uuzwaji holela
Bidhaa zinazotajwa kuleta athari soko lake limepamba moto, hasa mitandaoni. Matumizi ya shabu ni makubwa katika baadhi ya maeneo nchini, hasa jijini Mbeya kwa imani iliyojengeka kuwa hurejesha maumbile na nyama ya uke.
Matumizi hayo yametajwa mahususi kwa mwanamke anapopata mpenzi mpya au ambaye mwenza wake husafiri, hutumia shabu kwa lengo la kujenga uaminifu ndani ya mahusiano.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa mwezi mmoja kwa baadhi ya wauzaji na watumiaji wa kemikali hizo, wamedai shabu hukaza nyama za uke na ongezeko la joto.
Mmoja wa wauzaji (jina linahifadhiwa) anasema wateja wake wakubwa ni kwenye maeneo ya starehe, vilabu vya pombe za kienyeji na kwenye mikusanyiko ya watu.
“Soko la shabu siyo siri ni kubwa na sasa mahitaji yameongezeka, kuna wakati tunaishiwa na tunakozipata huadimika, hii biashara ina mapato ya chapchap,” anasema.
Anasema awali wakati zikitumika kama tiba ya jino, tumbo, kiungulia na upele, bei yake ilikuwa Sh500 kwa kipande, lakini sasa imepanda na kuuzwa kati ya Sh1,000 mpaka 2,000 kulingana na wingi wa mahitaji ya mteja husika.
“Shabu ni jiwe lenye asili kama chumvi ya mawe, tofauti yake yenyewe ni nyeupe kama chaki, tunauza kwa kupasua vipande vipande, lakini mteja akinunua hulazimika kusaga na kuiloweka kwa maji baridi kabla ya matumizi,” anasema mwanamama huyo.
Akielezea matumizi yake, anasema maji hayo hutumika kunawia sehemu ya siri na matokeo yake hugandisha uteute wa asili na huleta ukavu na kuongeza joto.
Wanawake wafunguka
Mfanyabiashara wa vileo eneo la Ikuti, Kata ya Iyunga jijini Mbeya, Anastazia Noel anakiri kushuhudia baadhi ya rafiki zake wakitumia shabu, malimao na ugoro kuweka sehemu zao za siri.
“Kwa mfano limao linatumika sana kwa wanawake wanapokuwa hedhi ili kukata damu kwa muda, lengo ni kutaka kufanya ngono na wanaume ambao sio wao rasmi,” anasema Anastazia.
Anasema kwa sasa wapo wafanyabishara wengi wanatembeza ugoro, shabu kwenye maeneo ya baa, grosari na kwenye vilabu vya pombe za kienyeji, hasa nyakati za jioni.
Anasema wateja wao wakubwa ni mabinti na wanawake wa rika la kati ya miaka 18-35.
Hata hivyo, wakati Mwananchi linapiga stori na dada huyo jioni katika eneo lake la biashara, likaonana na wanawake waliokuwa wanafanya biashara hiyo.
Walikuwa wamebeba vikapu, ndani yake vilikuwa na makopo yaliyohifadhiwa bidhaa hizo.
Naye Riselaiza Ayoub, mkazi wa Mji wa Makambako amekiri kutumia shabu miaka kadhaa iliyopita. Hata hivyo anasema alikumbana na changamoto ya maumbile yake kulegea na kukosa mvuto.
“Hali hiyo imenipa shida sana, mwanamume alikata mawasiliano kwa kunituhumu kuwa na mahusiano nje kutokana na mabadiliko ya maumbile yangu ya uke kuwa tofauti,” anasema na kuongeza;
“Maji ya shabu ukioshea maumbile husinyaa, huwa makavu na joto kali, mwanamume akiingia anapata starehe, lakini akirudia awamu nyingine maumbile huwa tofauti na wingi wa utelezi.” Riselaiza anasema kuna umuhimu wa elimu kutolewa kwa makundi rika kwa sababu kuna uwezekano mkubwa kukawa na wagonjwa wengi wa saratani baadaye zitokanazo na matumizi ya vitu visivyotakiwa katika sehemu za siri.
Yoni, pipi
Mbali na shabu, baadhi ya wanawake pia hutumia vidonge viitwavyo yoni, ambavyo huuzwa mitandaoni.
Vidonge hivyo vilivyotengenezwa China, huwekwa sehemu za siri kwa saa kadhaa eti huondoa majimaji na uchafu kwenye sehemu hizo.
“Nimewahi kutumia. Unaweka ukeni na kukaa nacho saa 6 mpaka 8 kisha unakiondoa na kinatoka na uchafu na majimaji. Nilifanya hayo yanayoelezwa lakini tangu hapo najikuta kama sipo sawa kabisa katika maumbile yangu, ili uwe vizuri ni mpaka uvitumie, nahisi vimeniharibu,” anasema Aneth (si jina lake halisi).
Licha ya yoni, vipipi vya kuongeza uwezo na hamu, haya yote yakizidi kushamiri mitandaoni, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kuwa wanawake wanazichangamkia pipi hizo zinazodaiwa kusaidia kuongeza uwezo, hamu ya kushiriki tendo la ndoa na kumfurahisha mwanamume.
Pipi hizo zenye rangi nyeupe mithili ya maji, hivi sasa ni habari ya mjini, kuanzia mitandaoni hadi katika maeneo yenye mikusanyiko ya wanawake na huuzwa kati ya Sh5,000 hadi Sh10,000.
Athari
Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, George Roimamu anakiri kuwepo kwa changamoto ya kupokea baadhi ya wagonjwa wanawake waliopata athari za matumizi ya kemikali, hususan tumbaku, malimao na shabu.
Anasema wanawake wa kati ya miaka 18 mpaka 35 hupata madhara na kubainika kuwa na tatizo la saratani ya shingo ya kizazi, maambukizi katika njia ya mkojo na nyama za asili za uke kulegea.
Ametaja madhara mengine ni kuua bakteria wanaolinda mfumo wa njia za uzazi na chembechembe za damu kuzalishwa tofauti na utaratibu wake.
“Kitu chochote chenye kemikali hakipaswi kuingizwa ukeni, kinaleta madhara makubwa kwa wanawake ambao baada ya miaka 10, matokeo hasi hujitokeza na hujikuta wakitumia gharama kubwa za matibabu,” anasema.
Dk George anataja madhara mengine ni pamoja na wanaobeba ujauzito wakijifungua huchanika, wakishonwa vidonda huachia na kutokauka, kukosa hamu ya tendo la ndoa na mahusiano kuvunjika.
“Wapo wanaofika kueleza ukweli ndoa zimeharibika kutokana na matumizi ya kemikali ukeni na hata wakishika ujauzito wanapojifungua huchanika kutokana na nyama ya uke kutoimarika.
Dk George anasema asilimia kubwa wanaokumbwa na kadhia hiyo ni wale wenye umri miaka 18 mpaka 35, huku madhara kiafya huibuka wakifika umri wa zaidi ya miaka 25 mpaka 45. Hata hivyo, anaonya wanawake kuachana na matumizi ya kemikali kwa kuwa siyo rafiki kiafya na huleta madhara makubwa kwa siku za baadaye.
Sababu sehemu za siri kulegea
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Ali Said anasema sehemu za siri za mwanamke zina bakteria walinzi hivyo, kutumia dawa na kemikali inaweza kuwaua bakteria hao na kuacha sehemu hizo zikiathiriwa kutokana na kukosa ulinzi wa kutosha.
“Uke ulivyoumbwa tayari una bakteria ambao kazi yao ni ulinzi, hivyo usafi wake unahitaji maji pekee, hakuna haja ya kuweka sabuni za kemikali, dawa wala mvuke wa maji ya moto, ni hatari sana kiafya,” anasema.
Daktari huyo anaeleza kuwa hakuna dawa ambayo imethibitishwa kuwa ina uwezo wa kumwongezea mwanamke hamu au nguvu ya kushiriki tendo la ndoa, kinachofanywa na wafanyabiashara hao ni kutafuta pesa.
“Hata mimi nimewahi kuzisikia hizo pipi na vitu vingine, lakini siwezi kuzungumzia, ninachofahamu mapenzi ni mawasiliano, mkiwasiliana utajua mwenzio anataka nini na wewe unataka nini, mtafika mahali pazuri.”
“Kama hamzungumzi ni vigumu kufurahia tendo, ndio hapo inapokuja kwenye kutafuta dawa na njia nyingine ambazo zinaweza kumuweka mtumiaji hatarini na kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi, huenda vitu kama hivi vinachangia,” anaongeza. Hilo linaelezwa pia na Dk Berno Mwambe, anayesisitiza mapenzi yanahusisha hisia na homoni, hivyo kutumia dawa na kemikali hakusaidii kwenye viungo vyao vya uzazi, bali huishia kuwaletea madhara kiafya watumiaji.
“Unaweza ukaweka dawa au ukafukisha ukaishia kuvimba, kubabuka na kuungua. Pia kwa kuweka vitu vya aina hiyo unaweza kupata maambukizi, yakiwamo fangasi, miwasho. Ukijihisi una shida yoyote sijui ukavu, maumivu wakati wa tendo ni vema kwenda hospitali ukapate ushauri wa kitaalamu na tiba na siyo kuweka vitu ukeni,” anasema Dk Mwambe.
Kuhusu tatizo la kulegea uke, mtaalamu huyo anasema mazoezi ndiyo tiba inayoweza kusaidia kuviweka viungo hivyo katika mwonekano wa kuvutia na salama.
“Ili kuimarisha misuli inayozingira uke, wanawake wanashauriwa kujaribu mazoezi ya sehemu ya chini ya tumbo (pelvic) ya sakafuni au ya kegel yanayoweza kusaidia kuboresha na kuimarisha misuli na uwezo wa kupata shauku ya kushiriki tendo hilo,” anasema Dk Mwambe.
Mamlaka zinasemaje?
Akizungumzia suala hilo, Meneja na Uhusiano na Mawasiliano kwa umma wa TMDA, Gaudensia Simwanza anakiri kuna changamoto ya udhibiti wa uuzaji wa dawa katika mitandao ya kijamii.
“Nashindwa kuzizungumzia dawa hizo kwa kuwa sina uhakika kama zipo kwenye kundi la dawa tunazosimamia sisi, maana inaweza kuwa ni dawa zinazoangukia kwenye tiba asili, ila wito wetu dawa hazitakiwi kuuzwa wala kutumiwa kiholela, wananchi wawe makini,” anasema Simwanza.
Kwa upande wake, Mfamasia katika Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Ndahani Msigwa anasema, “Hizo pipi hatuzifahamu na inawezekana kuna vitu vingi vinatumika, lakini kwa kuwa havijaja ofisini na kuvithibitisha basi mtu atakuwa anatumia kwa uamuzi wake na maisha yake.”