Makala
Hili hapa tatizo la ufundishaji wa Kiingereza Tanzania
Wakati bado kukiwa na mjadala wa lugha ya kufundishia nchini kati ya Kiswahili na Kiingereza, Watanzania wanakabiliwa na hatari ya kutofaidi fursa za kimataifa kwa kutoelewa lugha ya Kiingereza, huku pia matumizi ya Kiswahili yakiwa njia panda.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalum, mfasiri wa lugha na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Faraja Kristomus anaeleza sababu ya lugha ya Kiingereza kuwa ngumu miongoni mwa Watanzania na njia za kuikuza, sambamba na masuala mbalimbali katika sekta ya elimu.
Swali: Kwa muda mrefu Tanzania tumekuwa na mjadala wa lugha ya kufundishia na mpaka sasa tunatumia Kiswahili wa shule za msingi na Kiingereza kuanzia sekondari hadi elimu ya juu. Hata hivyo, uwezo wa Kingereza hauridhishi kwa wanafunzi, nini sababu?
Jibu: Suala la lugha ya kufundishia kwenye Sera ya Elimu halijawahi kupata majibu kwa sababu inaonekana ni suala la kitabaka kuliko kuwa jambo la kisera.
Tatizo pia wanaofanya uamuzi kwamba tutumie lugha ipi ya kufundishia ni watu wa tabaka fulani, lakini walengwa zaidi ambao ni wananchi wa kawaida hawajazingatiwa.
Kwa mfano, mtoto wa Dar es Salaam ana uwezo wa kumudu Kiingereza zaidi kuliko mtoto wa Kakonko au Kasulu Kigoma huko. Kwa sababu ili umudu lugha, ni lazima uwe na mazingira ya kuizungumza kuanzia ngazi ya ngazi ya familia.
Kwa kawaida lugha huwa ina stadi nne, kati ya hizo, mbili ni stadi za msingi ambazo ni kusikiliza na kuongea.
Kwa mfano, lugha za makabila yetu hizi hatuandiki lakini tunajua kuzungumza na kuongea na stadi za baadaye ni kuandika na kusoma.
Tunashindwa kuongea Kiingereza, kwa sababu tumeshindwa kuimarisha stadi za msingi. Ndio maana kwa wenzetu, ukiwa hauna umilisi wa kutosha wa msingi kwa lugha mama, lugha hiyo inaitwa lugha ya pili au ya kigeni.
Swali: Tatizo la kujifunza Kiingereza ni kubwa kiasi gani nchini?
Jibu: Ukweli ni kwamba Watanzania wengi wanakutana na lugha hiyo kwa nadra sana, tangu wakiwa shule ya msingi mpaka sekondari. Hatuna mazingira ya kumwezesha mtoto kijijini kusikiliza lugha ya Kiingereza ili aweze kuiongea.
Mtoto anaanza kusikia lugha ya kabila lake halafu anakutana na Kiswahili, anakuja kukutana na Kiingereza akifika sekondari na anaambiwa ndio lugha ya kufundishia.
Niliwahi kufanya uchambuzi wa matokeo ya mitihani ya shule za msingi na sekondari kwa wanafunzi wa mijini na vijijini. Ikaonekana kuwa, watoto wa vijijini walifeli zaidi kuliko wa mijini, kwa sababu wa mijini walikuwa na mazingira mazuri ya kujifunza Kiingereza.
Swali: Vipi kuhusu maandalizi ya walimu?
Jibu: Mwalimu anayetakiwa kumfundisha mtoto darasani, unakuta hana umilisi wa lugha na hawezi kuzungumza dakika zote kwa Kiingereza, matokeo yake walimu wengi hata yale masomo anayotakiwa kufundisha kwa Kiingereza wanafafanua kwa Kiswahili.
Mimi sipingi Kiingereza, lakini kwa kuwatendea haki Watanzania walio wengi, sisi watunga sera tuache ubinafsi kwa kudhani kwamba tunatakiwa kutunga sera zinazowanufaisha watoto wa tabaka letu.
Swali: Kwa hiyo tuwe na mwelekeo gani, tujikite kwenye Kiswahili au tuongeze juhudi kukuza Kiingereza kama lugha ya kufundishia?
Jibu: Awali baada ya uhuru Kiingereza hakikuwa shida hata kwa wale walioishia darasa la nane na sababu ni aina ya ufundishaji uliokuwepo. Hatujawekeza vya kutosha kwenye miundombinu ya ufundishaji wa Kiingereza. Sio kuwa na vitabu tu, tunahitaji kumwezesha mtoto kusikiliza ili ajifunze.
Tuna msingi mbovu wa ufundishaji, hivyo tuwawezeshe walimu kumudu lugha, wawe na umilisi nayo. Pili tuwekeze kwenye mifumo ya lugha, kwa mfano tunao uwezo wa kiteknolojia kuwafundisha watoto huko vijijini? Pia tuwe na vitabu vya kutosha.
Ili kuwawezesha walimu, tunaweza kuwa na program za kupeleka walimu nchini Uingereza ili wapewe mafunzo hata ya mwaka mzima, kwanza waimarishe Kiingereza na kupewa mbinu.
Jambo lingine ni kutumia vyuo vya elimu na vyuo vikuu. Tukishafundisha hawa walimu na kuwapa maarifa, uwezekano wa kushirikiana kati ya vyuo vikuu na halmashauri uwepo.
Halmashauri zitenge bajeti, wapeleke walimu kwenye vyuo hata kwa mwezi mmoja. Walimu wakipata mafunzo wataboresha uelewa.
Swali: Nini nafasi ya Kiingereza kwa Tanzania ambayo Kiswahili kimetamalaki?
Jibu: Kiingereza kina ngazi tatu; kwanza kinatumika kama lugha mama, ngazi ya pili ni lugha ya pili.
Mzunguko wa tatu ni wa nje, ni nchi ambazo wanafundisha Kiingereza kama lugha ya kimataifa ili mtu aweze kuwasiliana na watu wa mataifa mengine.
Chukua kwa mfano Ujerumani, Ufaransa, Urusi, Ureno, Japan, China. Nchi hizi zinaweka msisitizo katika ufundishaji wa lugha hiyo, kwa sababu kihistoria hazina ukaribu na hiyo lugha, lakini wanatambua kuwa Kiingereza ni lugha ya kimataifa na hawawezi kuikwepa.
Sasa kwa Tanzania sisi tuna lugha za makabila, halafu tuna Kiswahili kinachotuzunguka, hapo ndipo mtihani tulionao, kwani mtu anaona hahitaji Kiingereza kwa sababu anaweza kutumia Kiswahili.
Profesa Charles Bwenge wa Chuo Kikuu cha Florida, Marekani alifanya utafiti zamani na kueleza kuwa Watanzania wengi wana mwamko mdogo wa Kiingereza kwa sababu awali waliiona kama lugha ya ukoloni.
Kimsingi, tunapaswa kuwahimiza wanafunzi wetu kujifunza Kiingereza na lugha nyingine kwa sababu zitawawezesha kupata fursa za kimataifa.
Kwa kuwa tuna lugha yetu ya Kiswahili, Watanzania wachache sana kwao Kiingereza ni lugha ya pili, kwa hiyo tuongeze juhudi za kukifundisha Kiingereza shuleni na tutumie mbinu za kuifundisha lugha hiyo kama nchi nyingne zinavyofanya.
Swali: Licha ya Serikali kuzindua Sera ya Elimu ya mwaka 2014, haijawahi kutumika kikamilifu, tatizo liko wapi?
Jibu: Mwaka 2014 haikuwezekana kutekeleza sera mpya kutokana na ufinyu wa bajeti na pia sera ile ilitaka elimu ya msingi iwe miaka sita na elimumsingi iwe mpaka kidato cha nne.
Hiyo pia iliathiri uwezo wa Serikali kwa sababu kama ingetekelezwa ilitakiwa waunganishe wanaomaliza la saba na wa darasa la sita wote waende kidato cha kwanza kwa mara moja. Ndio maana wakaona wasogeze mbele.
Sasa wamekuja na maboresho mengine kama marekebisho ya mtalaa. Katika marekebisho haya, wadau tuliona yana kasoro kwa sababu yamejielekeza zaidi kwa wataalamu walionufaika na mfumo uliopo, badala ya kufanya tathmini ya kina zaidi kwa wanufaika wa elimu.
Hakukuwa na ushirikishwaji kwa walengwa walioko vijijini kwa mfano kujua wanahitaji kitu gani kwenye elimu.
Kwa hiyo tungekwenda mbali zaidi kuwa na mchakato shirikishi kwa kuihusisha zaidi jamii ya Watanzania.
Wadau pia tuliona sera ile ilijielekeza zaidi kwenye umri wa wanafunzi kukaa shuleni kuliko mambo mengine.
Ukiangalia utafiti uliofanywa na mashirika ya kimataifa kama Benki ya Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) , watoto wa nchi zinazoendelea hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara wanapoteza muda mwingi shuleni bila kujifunza.
Kwa mfano, ripoti ya Benki ya Dunia ya hivi karibuni, inaonyesha kuwa Tanzania, mtoto anayekaa shule ya msingi miaka saba, ni kama anakaa miaka mitatu tu, kwa sababu walimu hawamalizi mitalaa na silabasi.
Pia kutokana na changamoto za maji na za kiafya, hawahudhurii shuleni. Kwa hiyo ilitakiwa sera mpya ya elimu, izingatie ufundishaji kuliko umri wa mtoto kukaa shuleni.
Swali: Pamoja na changamoto za kisera, baadhi ya mambo yaliyomo yameshaanza kutumika kama vile elimu ya amali. Unaonaje mkakati huu?
Jibu: Mpango wa elimu ya amali sio mbaya ni kitu chema kabisa, lakini changamoto ni utekelezaji wake, kwa sababu inahitaji uwekezaji wa kutosha.
Nchi yetu kwa muda mrefu haikuwa na uwekezaji wa kutosha kwenye shule zetu za ufundi na zile zilizokuwepo kama Iyunga (Mbeya), Ifunda (Iringa) Moshi (Kilimanjaro) na nyinginezo, zilitelekezwa kwa sababu mashine zilizokuwepo zilikuwa za kizamani na hazikuwa na tija tena kwa wakati wa sasa.
Kwa hiyo tulihitaji kuwekeza na sio kusema tu tuwe na shule 300 au ngapi, bali ni kuainisha mahitaji ya hizo shule na kuyatimiza.
Tulio wengi katika taasisi za elimu tuna mawazo ya nadharia zaidi, nadhani kwa kuwa tunao mafundi huko vijijini wenye ujuzi wa kutenda, kama Serikali ingekuwa na nia njema, ingewapa mafunzo ili jukumu lao liwe kumpokea mwalimu aliyemaliza mafunzo darasani kwa nadharia na yeye ashinde na wanafunzi akiwapa mafunzo ya vitendo kwa asilimia 60.
Nyingine kwenye hii programu ya mafunzo, nadhani Serikali ingetenga bajeti ya kutosha kwa mafundi waliopo vyuoni, ili nao wasasishe maarifa yao kwa sababu inaonekana mwalimu akishaajiriwa nafasi ya kuendelezwa inakuwa changamoto.
Jambo la tatu kama unakuwa na chuo cha ufundi, miradi ya ujenzi wa hospitali, shule, barabara, ikiwezekana walimu hao wanaokuwepo kwenye vyuo vya ufundi na wanafunzi wao, tuwahusishe zaidi kwenye hii miradi ili wapate uzoefu na pia Serikali itaokoa fedha kwenye miradi hiyo.
Tunapaswa pia kuongeza thamani kwa mafundi wetu hawa. Tunao mafundi wengi mitaani, lakini ukiangalia bidhaa wanazotengeneza haziwezi kushindana sokoni, hivyo tunapaswa kuwaongezea thamani, ili kama tunatafuta masoko ya nje kuwe na bidhaa zenye ubora.
Swali: Kuna mradi wa uboreshaji wa vyuo vikuu nchini unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (HEET), unatathmini vipi ufanisi wake?
Jibu: Mradi huu ni mkopo wa Benki ya Dunia uliolenga zaidi kuvisaidia vyuo vikuu vya umma katika fani za sayansi, uhandisi na teknolojia na hisabati.
Tungetarajia mradi huu uboreshe mazingira na miundombinu ya vyuo husika. Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, miundombinu iliyopo ni ya muda mrefu, majengo, mifumo ya majitaka vyote ni vya muda mrefu.
Lakini mradi huu unalenga kujenga kujenga vyuo vingine vya pembeni badala ya kuboresha kampasi kuu. Sasa hii imekuwa ni changamoto kwa sababu kutengeneza vyuo vipya itabidi uongeze udahili wakati uwezo ni mdogo matokeo yake huko mbele tutaelemewa.
Nadhani mradi huu wa HEET ungejielekeza zaidi kwenye miundombinu ya ufundishaji kama ofisi, madarasa, maabara na nyenzo za ufundishaji na mazingira ya wanafunzi, kwa sababu vimechoka sana na uwezo wetu wa bajeti za ndani ni mdogo.