Kitaifa
Kufanya mapenzi majini kunavyowaweka hatarini wavuvi kupata VVU
Nyasa. Baadhi ya wavuvi wa samaki na dagaa katika Ziwa Nyasa wilayani Nyasa, Mkoa wa Ruvuma wapo hatarini kupata magonjwa ya zinaa, ikiwemo Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa kushiriki ngono zembe kwenye maji kwa imani kuwa hawataambukizwa VVU.
Wavuvi hao wanadai wanafanya hivyo baada ya mganga wa kienyeji anayefahamika kwa jina la ‘askofu’ kuwaeleza kufanya hivyo husaidia kuondoa nuksi na kuongeza mvuto wa kuvua samaki wengi zaidi.
Uchunguzi mdogo uliofanywa na Mwananchi Digital hivi karibuni umebainika kuwa vitendo vya ngono kwenye fukwe za Ziwa Nyasa vimeongezeka kutokana na imani hiyo, bada ya kupewa dawa za mitishamba na mganga huyo.
Inaelezwa dawa hizo zinazoongeza nguvu za kiume na mvuto wa kimapenzi, wavuvi huzinunua kwa Sh5,000 kwa chupa ya nusu lita na hutumia kabla ya kukutana na wanawake.
Wille Mwangono, mmoja wa wavuvi katika ziwa hilo amesema wavuvi wengi wa kiume hufanya ngono bila kutumia kinga, wakiamini wakifanya ngono kwenye maji huwasaidia kupata mvuto zaidi na samaki wengi.
“Humu kwenye maji ndiyo gesti zetu, tunajifanya tunaogelea kumbe tunafanya mapenzi na hakuna anayegundua,” amesema Mwangono na kuongeza kuwa huwa huwalipa wanawake hao kati ya Sh3,000 hadi 20,000 kulingana na makubaliano.
Zidadu Mbele, mvuvi mwingine naye amekiri vitendo vya ngono kwenye fukwe za ziwa hilo vimeongezeka, huku akirusha mpira kwa wanaume kwamba huwarubuni wanawake wakafanye vitendo hivyo ndani ya ziwa bila kinga kwa madai si rahisi kupata magonjwa ya ngono.
Hata hivyo, Somoye Hamdani, mkazi wa Mbambabay amesema anaamini wanawake wengi hufanya ngono na wavuvi kwa sababu ya hali ngumu ya maisha.
Hata hivyo, ametoa wito kwa Serikali kuwapatia mitaji ili waondokane na biashara ya kujiuza kwa wavuvi.
Mganga mkuu azungumza
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Steven Mbunda amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema tayari Idara ya Afya ya Wilaya ya Nyasa imeweka mikakati ya kutoa elimu kwa wavuvi kwa lengo la kuwaepusha na imani potofu na wazingatie matumizi ya kondomu.
Amesema maeneo ambayo tayari wameyafikia kutoa elimu hiyo ni pamoja na mialo mikubwa ya Chiwindi, Litui, Mbambabay, Ngo’ombo na Liuli.
“Tunaendelea kutoa elimu na kugawa kondomu baada ya kuwaelekeza madhara ya kufanya ngono bila kondomu, ili kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya zinaa na Ukimwi,” amesema Mbunda.
Amesema kati ya Aprili hadi Juni, 2024, watu 83 wamegundulika kuwa na mambukizi ya VVU, wanawake wakiwa 26 na wanaume 57.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Nyasa, Raphael Kalembo amesema wataendelea kushirikiana na wavuvi na viongozi wa dini, ili kuhakikisha wavuvi wanazingatia usalama wa afya zao na kuepuka imani potofu na pia watafuatilia na kudhibiti uwepo wa waganga wanaosababisha imani hizo.