Connect with us

Kitaifa

Rais Samia ataka utafiti rasilimali watu sekta ya afya

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Afya ikamilishe utafiti wa kitaifa, unaoangalia hali halisi ya rasilimali watu katika sekta ya afya Tanzania ili kupata takwimu za nguvu kazi iliyopo ndani na nje ya vituo vya tiba na hatimaye kukabiliana na upungufu uliopo.

Rais Samia pia ameiagiza Ofisi ya Waziri Mkuu kuimarisha kamati ya uratibu ya kisekta kuhusu rasilimali watu katika kada ya afya inayojumuisha Wizara za Afya, Tamisemi, Utumishi, Fedha na sekta binafsi.

Ametoa maagizo hayo leo Julai 31, 2024 aliposhiriki kilele cha kumbukizi ya tatu ya urithi wa hayati Benjamin Mkapa.

Kumbukizi hiyo ilitanguliwa na kongamano la siku mbili lililojadili changamoto ya rasilimali watu katika sekta ya afya Tanzania na hatua za kuchukua.

“Naielekeza Wizara ya Afya kubainisha hali halisi ya wataalamu wa afya nchini, tungependa kufahamu nguvu kazi iliyo nje ya mfumo wa ajira na ile iliyo ndani ya vituo vyetu vya afya,” ameagiza.

“Waziri Ummy (Mwalimu-Waziri wa Afya) ameniambia hapa kwamba mmejipanga kufanya vikao vya mabaraza ya kitaaluma ili kuja na majibu ya nguvu kazi iliyo nje na mahitaji halisi ya ndani. Masilahi ya watumishi tutaenda nayo polepole, katika hili niseme tunathamini kazi yenu na tunajua ugumu wake, tutaangalia masilahi yenu,” amesema.

Rais Samia amesema Taasisi ya Benjamin Mkapa imejitofautisha na zingine kwa kuwekeza katika rasilimali watu kwenye sekta ya afya.

Amesema majengo na dawa pekee hayana uwezo wa kutibu, hivyo wataalamu wa afya wanahitajika na inachukua muda mrefu kuwaandaa.

“Unahitaji miaka sita kumwandaa daktari mmoja na daktari bingwa miaka tisa hadi 12, lakini pia unahitajika uzoefu. Hivyo kumpoteza mtumishi mmoja ni hasara kubwa kwa Taifa,” amesema.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ambaye ni msarifu wa taasisi hiyo, amesema BMF imejielekeza katika kuboresha nguvu kazi ya sekta ya afya.

Amesema wametoa ajira mpya 1,050 za watumishi wapya wakati wakimalizia kutathmini aina ya watumishi wa afya kuanzia ngazi ya msingi hadi ngazi za juu, ili kuziba mapengo yaliyopo na kuendana na huduma zinazohitaji.

Huku akimpongeza Rais Samia kwa hatua anazochukua katika kuboresha huduma za afya, Dk Mwinyi amesema suala la afya halikwepeki.

Amesema wananchi wa Zanzibar wanapozidiwa huvuka maji kufuata huduma upande wa Bara.

Katika hitimisho na maazimio, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema miongoni mwa mambo yaliyoibuka katika kongamano hilo ni uzalishaji wa madaktari, wauguzi, wafamasia, wataalamu wa maabara na kukosekana kwa ajira.

“Madaktari na wataalamu tunazalisha wengi kupitia vyuo vyetu na hatuwapi ajira, lazima tutatue changamoto hii. Tutakaa na mabaraza ya wanataaluma wakiwemo MAT (Chama cha Madaktari Tanzania ), wafamasia, wauguzi, maabara tukubaliane njia bora ya kudhibiti watumishi wa afya ambao wapo barabarani,” amesema.

Takwimu za hivi hivi karibuni, zinakadiria kuwa zaidi ya madaktari 5,000 waliohitimu na kuwa na sifa za kuajiriwa, wanaendelea kusota mtaani kwa kukosa ajira rasmi, huku wakiwa wametumia zaidi ya Sh450 bilioni kusomea fani hiyo.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi