Connect with us

Kimataifa

Biden ajitoa kugombea urais, ampendekeza Kamala

Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Joe Biden (81) ametangaza kujitoa kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi utakaofanyika Novemba 2024.

Biden aliyeingia madarakani mwaka 2020, ametangaza uamuzi huo leo Jumapili Julai 21, 2024 huku akimpendekeza Makamu wake, Kamala Harris kupeperusha bendera ya Democratic katika kinyang’anyiro hicho.

Kupitia taarifa aliyoichapisha katika mtandao wake wa X (zamani Twitter) amesema: “Imekuwa heshima kubwa maishani mwangu kutumika kama Rais wenu. Ingawa imekuwa nia yangu ya kutaka kugombea tena nafasi hiyo, naamini ni kwa manufaa ya chama changu na nchi kwa mimi kujiuzulu na kujikita katika kutimiza majukumu yangu ya urais kwa muda wote uliosalia.”

Amesema anatarajia kuhutubia Taifa na kueleza kwa undani sababu ya kujitoa kwake hivi karibuni.

Hata hivyo, tovuti ya Al Jazeera imeripoti miongoni mwa sababu ya kumfanya kukaa kando ni wafuasi wa chama chake cha Democratic kupoteza imani naye ya kumshinda mpinzani wake wa karibu, Donald Trump wa Republican.

“Wafuasi wa Democratic wamepoteza imani naye kutokana na ‘uwezo wake wa kiakili’,” imesema taarifa hiyo.

Wakati mjadala ukishika kasi maeneo mbalimbali duniani juu kutangaza uamuzi huo, Biden amempigia chapuo makamu wake, Kamala Harris kupeperusha bendera ya chama cha Democratic katika nafasi hiyo.

 “Wanademocratic wenzangu, nimeamua kutokubali kuteuliwa na kugombea urais na kuhamishia nguvu zangu zote katika majukumu yangu kwa muda uliosalia wa muhula wangu.

“Uamuzi wangu wa mwaka 2020 ulikuwa kumchagua Kamala Harris kama Makamu wangu wa Rais. Na umekuwa uamuzi bora zaidi ambao nimefanya. Leo namuunga mkono Kamala kuwa mteule wa chama chetu mwaka huu, ni wakati wa kuungana kumshinda Trump,”ameandika Biden.

Awali, Biden alipata shinikizo la kuondoka katika nafasi hiyo kutokana na hali yake ya kiafya kuzorota lakini pia kushindwa kufanya vizuri mdahalo na mpinzani wake wa chama cha Republic Donald Trump.

Wiki iliyopita Biden aligundulika kuwa na Uviko-19 na kulazimika kutengwa hivyo kushindwa kuendelea na kampeni.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi