Connect with us

Makala

Tamu, chungu za teknolojia kwa watoto

Dar es Salaam. Maendeleo katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) imeenda kubadilisha nyanja mbalimbali za maisha yetu, ikiwemo uchumi, siasa, jamii na nyinginezo.

 Awali kabla ya maendeleo hayo watu walikuwa wakipashana habari mbalimbali kupitia barua, redio na televisheni, mambo yamebadilika sasa kupitia vifaa vya kielektroniki vilivyounganishwa na intaneti, kama vile simu na kompyuta, sasa watu wanaweza kuwasiliana, kupata taarifa mbalimbali.

 Maendeleo hayo ya teknolojia yamewafikia pia watoto, kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii wanaweza kuwasiliana na kujifunza mambo mbalimbali kupitia tovuti.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Watoto (Unicef) kwa kushirikiana na wizara hiyo mwaka 2022 ulionyesha kuwa, watoto 67 katika 100 wenye umri wa miaka 12 – 17 wanatumia bidhaa za mawasiliano, ikiwemo simu janja, kompyuta mpakato na runinga (janja) zenye intaneti.

Utafiti umebainisha kuwa simu na vifaa vingine vya kielektroniki wanavyotumia watoto hupatiwa na wazazi bila kujua madhara wanayokumbana nayo watoto.

Hivi karibuni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema matumizi yasiyofaa ya teknolojia yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa ukatili dhidi ya watoto mitandaoni.

 Anasema hali hiyo inatokana na wazazi kushindwa kusimama kikamilifu na kufuatilia matumizi ya vifaa vya Tehama wanavyowapatia watoto wao.

 “Utafiti umeonesha kuwa watoto wanne katika 100 waliotumia mitandao walifanyiwa aina mojawapo ya ukatili mtandaoni, ikiwemo kulazimishwa kujihusisha na vitendo vya ngono, kusambaza picha na video zenye maudhui ya kingono bila ridhaa yao na kurubuniwa kujihusisha na shughuli za kingono kwa kuahidiwa fedha au zawadi nyingine,” anasema.

Waziri huyo anabainisha kuwa watoto na kundi la vijana balehe wameingizwa kwenye uhalifu (panya road), ujambazi na usafirishaji haramu wa binadamu na matumizi ya dawa za kulevya).

Vilevile muda unaotumika zaidi wa vifaa hivyo ni nyakati za usiku, muda unaoongeza madhara zaidi kwa kuwa watumiaji wengi wanashindwa kumudu majukumu ya shughuli za kuanzia asubuhi na siku nzima, hivyo huathiri maendeleo yao shuleni.

“Matumizi yaliyopitiliza yamesababisha uraibu (ulevi) kwa watumiaji ambapo muda mwingi hutumika kwenye mitandao kuliko kazi zenye tija,”anasema.

Kauli ya Dk Gwajima inaungwa mkono na Yahaya Othman, ambaye ni baba wa watoto wanne anayesema kuwa kutokana na watoto kutokujua matumizi sahihi ya mitandao, kumekuwa kukishuhudiwa vitendo vya kikatili kwa watoto kupitia mitandao.

“Watoto wamekuwa wakirubuniwa mitandaoni na kujikuta wakianzisha mahusiano na watu ambao wakati mwingine hawawafahamu na baadaye kuwataka kutuma video au picha za utupu.”

Anasema baadaye picha na video hizo hutumiwa kuwatisha na kuwaamuru kutoa pesa au kufanya vitu viovu, jambo linaloweza kuwapelekea kupata changamoto za kisaikolojia.

Naye Sakina Ibrahim, ambaye ni mama wa mtoto mmoja anasema kutokana na baadhi ya wazazi kutokuwa na utaratibu wa kuangalia kile anachokifanya mtoto katika mitandao, hujikuta wakiingia katika tovuti ambazo haziendani na umri wa mtoto husika.

Pia anasema baadhi ya wazazi kushindwa kudhibiti matumizi sahihi ya mitandao kunapelekea watoto kutumia muda mwingi, hivyo kuwafanya kupata uraibu.

“Kuna haja ya wazazi kuwa makini na matumizi ya vifaa mbalimbali vya teknolojia kwa watoto ili kuwaepusha na kuingia katika ukatili mitandaoni pamoja na uraibu mitandaoni,”anasema.

Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa teknolojia, Emannuel Masoko anasema teknolojia inazidi kuendelea kukua kwa kasi, matumizi yake hayaepukiki hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari ili athari zake zisiwaathiri watoto.

Masoko anasema kukua kwa teknolojia kumerahisisha mambo mbalimbali, ikiwemo njia za usomaji.

Anasema awali watoto wakitaka kupata rejea mbalimbali wakati wakijifunza, iliwalazimu kwenda maktaba, lakini sasa kupitia mtandao wanaweza kuzipata rejea hizo kwa urahisi.

“Pamoja na masomo, pia wanaweza kujifunza stadi mbalimbali za maisha, ambazo ni muhimu katika ukuaji wao,” anasema.

 Masoko anasema ili kuwaweka watoto salama, hakuna budi wazazi kutokuwa nyuma katika masuala ya teknolojia ili waweze kuwafunza na kuwaongoza watoto juu ya matumizi sahihi ya mitandao.

 Anasema ni vyema wazazi kutenga muda wa kujifunza namna ya kutumia vifaa mbalimbali vya teknolojia, ikiwemo matumizi ya simu janja, vishkwambi pamoja na kompyuta mpakato.

 Pia kufahamu mitandao mbalimbali inavyotumika pamoja na programu tumizi ili waweze kufuatilia matumizi ya mitandao kwa watoto wao.

“Pia unaweza kupakua baadhi ya programu tumizi ambazo zitakusaidia kufuatilia matumizi ya mitandao ya mtoto wako,” anasema.

Vilevile anasema mzazi akishakuwa na uelewa kuhusu teknolojia, ni rahisi hata kuwafundisha watoto kuhusu matumizi sahihi ya mitandao pamoja na tahadhari wanazotakiwa kuchukua.

Mfano wa tahadhari hizo ni pamoja na kutotoa taarifa zao binafsi kwa watu wasiowafahamu, ikiwemo majina yao, taarifa za familia, anuani na nyinginezo, kwani zinaweza kuwasaidia wahalifu wa mitandaoni kuwafikia.

 Naye Mkurugenzi wa taasisi ya kutetea haki za watoto ya Green Kids and Youth Foundatio, Vaileth Mwazembe anasema teknolojia ya habari na mawasiliano ina manufaa makubwa si kwa watoto pekee, bali hata watu wazima, kwani imerahisisha mambo mengi.

 Anasema kulindwa kwa mtoto dhidi ya ukatili ni jukumu la kila mtu katika jamii na si wazazi na walezi peke yake, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika.

“Kutokana na umuhimu wa maendeleo haya ya teknolojia, ni muhimu watoto kuhakikisha wanatumia mitandao katika matumizi sahihi na kujiepusha na yale yanayoweza kupelekea unyanyasaji wa kimtandao, ikiwemo utumaji wa taarifa au picha kwa mtu wasiyemfahamu mtandaoni,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kulinda watoto la Save the Children, Angela Kauleni anasema wazazi, walezi wanapaswa kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya mitandao kwa watoto na vijana, ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili mitandaoni.

 Pia alitoa wito kwa watoto ambao wanakutana na ukatili huo wasikae kimya, wahakikishe wanatoa taarifa kwa wazazi au walezi wao ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wahusika wa vitendo hivyo.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi