Connect with us

Kitaifa

Serikali yatangaza ajira 11,015 za walimu, omba hapa

Dodoma. Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi 11,015 kwenye kada ya walimu kwa halmashauri nchini.

 Tangazo hilo lililotolewa jana Julai 20, 2024 na kusainiwa na Kaimu Katibu wa Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa niaba ya Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya za Serikali za Mitaa.

Ofisa Uhusiano wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Baraka Samson amethibitisha kufunguliwa maombi hayo baada ya tarehe ya mwisho iliyotolewa kuwasilisha maombi ya ajira za sekta ya afya kukamilika.

Julai 7, 2024 ofisi hiyo iliwatangazia Watanzania wenye sifa na uwezo wa kujaza nafasi 9,483 katika sekta ya afya, mwisho wa kutuma maombi ilikuwa Julai 20, 2024.

Katika tangazo hilo lenye kumbukumbu namba JA/9.259/01/B/14, mikoa hiyo na nafasi katika mabano ni Njombe (62), Mtwara (153), Dodoma (85), Shinyanga (115), Songwe (101), Iringa (56), Manyara (78), Tabora (116), Singida (110), Tanga (113), Kagera (133) na Katavi (99).

Mingine Rukwa (76), Simiyu (120), Mara (173), Geita (90), Ruvuma (140), Kigoma (129), Dar es Salaam (19), Pwani (68), Arusha (116), Mwanza (134), Morogoro (129), Kilimanjaro (124), Mbeya (217) na Lindi (95).

Nafasi nyingi za ajira hizo zinaonekana kwa walimu wa ngazi za shule za awali, msingi na sekondari, huku masomo ya hisabati na sayansi yakiongoza kwa nafasi nyingi.

Pia katika nafasi hizo walimu wa mafunzo ya elimu ya amali wamepewa nafasi za ajira katika baadhi ya halmashauri wakati ambapo Sera ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Mwaka 2023 ikiwa imeanza kutekelezwa nchini.

Tangazo hilo limetaja miongoni mwa masharti ya jumla ni waombaji wote wa nafasi hizo wawe ni raia wa Tanzania wenye umri usiozidi miaka 45 isipokuwa kwa wale tu walioko kazini serikalini.

“Waombaji waliostaafishwa katika utumishi wa umma hawaruhusiwi kuomba isipokuwa kama wana kibali cha Katibu Mkuu Kiongozi,” inaelezwa katika tangazo hilo.

Kwa mujibu wa tangazo hilo mwisho wa kupeleka maombi ambayo yanatakiwa kutumwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa ajira ni Agosti 2, 2024.

Tangazo hilo la ajira limetolewa wakati takwimu za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zikionyesha Tanzania ina upungufu wa walimu 271,025 kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi sekondari.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Tamisemi, Zainab Katimba katika kipindi cha kati ya mwaka 2020/21 hadi mwaka 2022/23, Serikali iliajiri walimu 29,879 wakiwemo 16,598 wa shule za msingi na 13,281 wa sekondari.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi