Kitaifa
Mbinu ya kubaini bidhaa bandia yatajwa
Dar es Salaam. Wakati Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) ikiendelea kupambana na bidhaa bandia, imetaja mbinu ya kuzibaini huku ikiwataka wafanyabiashara wauze bidhaa halisi kwa kuwa hazina ushindani na zile bandia.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano Julai 17 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), William Erio wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kilele cha Wiki ya Kudhibiti Bidhaa Bandia Duniani.
Kilele cha wiki hiyo yenye kauli mbiu, “Kudumisha Uhalisia wa Kulinda Ubunifu wa Maendeleo ya Kiuchumi Nchini,” kitafanyika kesho Alhamisi Julai 18 2024 Mlimani City jijini Dar es Salaam, huku kikiwa na maonyesho mbalimbali za wajasiriamali na viwanda vidogo vidogo.
Akizungumzia mbinu ya kujua bidhaa bandia, Erio amesema ni pamoja na kuuzwa kwa bei ya chini tofauti na bei husika zilizopo katika maduka mengine.
Amewataka wananchi kuziacha bidhaa bandia, badala yake wanunue halisi kwenye chanzo kinachoeleweka, “tuhakikishe Taifa letu halina bidhaa bandia.”
Mbali na wanunuaji wa bidhaa hizo, amewataka wafanyabiashara waunge mkono suala la kupambana na bidhaa bandia.
“(Wafanyabiashara) wahakikishe wanatuunga mkono kwa kuacha kuagiza bidhaa bandia, na utajuaje kama hii bidhaa ni bandia au hapana, nenda kanunue katika chanzo kinachoeleweka na uagize kwa mfanyabiashara anayeeleweka na anayetambulika katika nchi yake, kwa maana hiyo hautaleta bidhaa bandia hapa nchini,” amesema Erio.
Amesema bidhaa bandia katika uchumi zinadhorotesha biashara na zinafanyika katika mifumo isiyokuwa rasmi, “kwa maana hiyo kuna ukwepaji wa kodi kwa kuwa zinapita kwenye njia zisizo rasmi na ubora wake ni wa chini, hivyo kuwa na matatizo mengi.
“Wale wanaofanya bashara halali hawawezi kushindana na bidhaa bandia kwa kuwa bidhaa bandia bei yake ni ya chini, lakini pia inaathiri uwekezaji, nchi yetu imekuwa ikihimiza wawekezaji kutoka nje waje Tanzania kwa kuwa ni sehemu nzuri ya kuja kuwekeza,”amesema.
Amesema, “wale wanaokuja kuwekeza nchini wakikutana na bidhaa halisi inasaidia katika kuboresha uwekezaji.”
Hata hivyo, amesema tume hiyo inahitaji kuungwa mkono kutoka kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo wanachama wake ni wadau wa bidhaa nchini.
“Wakati mwingine unaweza kukuta mtu analalamikia pensheni ndogo kumbe ananunua bidhaa bandia ambazo zinaisha kwa muda mfupi halafu anatakiwa anunue tena. Kwa hiyo hawa ni wadau muhimu katika vikao vyao wawaeleze wanachama wao madhara ya biadhaa bandia.”
Mmoja wa wadau wa bidhaa bandia, Zuberi Jafar amesema elimu bado inahitajika kwa jamii kuhusu uelewa wa bidhaa bandia, kwa kuwa wengi wao hawawezi kuzitofautisha na zile halisi.
“Ukienda Kariakoo kununua simu ya aina fulani, muuzaji atakwambia hiyo ni simu halisi kwa kuwa anavutia biashara yake, ndio maana kila siku watu wanalalamika simu zao haziingii chaji,’ amesema Jafar.
Husna Hamis, mmoja wa wateja wa bidhaa mbalimbali nchini amesema unaponunua bidhaa halisi inamudu kwa muda mrefu hadi utakapoamua ubadilishe mwenyewe.
Ametolea mfano sinki la choo, amesema amenunua miaka mingi lakini ukiliona kama jipya kwa kuwa ni bidhaa halisi.