Connect with us

Kitaifa

TCU yafungua dirisha udahili masomo elimu ya juu

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kufunguliwa kwa dirisha la kwanza la udahili kuanzia Julai 15 hadi Agosti 10, 2024, ikiwataka wahitimu kuomba moja kwa moja kwenye vyuo wanavyopendelea.

Tangazo hilo linawahusu jumla ya wahitimu 111,056 waliofaulu mtihani wa kidato cha sita mwaka 2024 pamoja na wenye stashahada na wengine wenye sifa zinazofaa, ikiwamo kozi ya cheti inayotolewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), pia wanaruhusiwa kuomba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Julai 15, 2024 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amewataka wahitimu kupitia mwongozo wa uombaji wa shahada kabla hawajaomba.

“Ili kuelewa usahihi na programu zilizoidhinishwa, waombaji wanapaswa kupitia kwa makini Mwongozo wa Uombaji wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2024/25,” amesema.

Tangazo la TCU limekuja siku mbili baada ya Baraza la Mitihani la Taifa la Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya mwaka 2024, ambapo jumla ya watahiniwa 113,536 kutoka shule na wa binafsi walifanya mtihani wa kidato cha sita.

Kati ya watahiniwa 104,454 waliosajiliwa kutoka shule 103,812 (asilimia 99.39) walifanya mtihani. Mwaka 2023, watahiniwa 96,319 walifanya mtihani.

Miongoni mwa watahiniwa binafsi 9,082 waliosajiliwa, 8,387 walifanya mtihani, na 695 hawakufanya.

Takwimu za hivi karibuni za Necta zinaonyesha ongezeko kidogo la kiwango cha ufaulu ikilinganishwa na mwaka uliopita.

TCU imesisitiza taratibu za uombaji zinaelezwa na vyuo husika, si TCU.

Vigezo na sifa za programu inapatikana kwenye tovuti za vyuo na kwenye miongozo ya udahili ya TCU.

“Tunawahimiza waombaji kuelewa vizuri miongozo ya TCU na maelekezo ya vyuo kabla ya kuwasilisha maombi,” ameshauri Profesa Kihampa.

Waombaji wamehimizwa kutembelea tovuti za vyuo kwa taratibu sahihi za maombi na taarifa za kina za programu.

Amewataka pia wahitimu wenye vyeti vya mitihani vya kigeni kuwasilisha Necta kwa Elimu ya Sekondari au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa ulinganifu wa diploma kabla ya kuomba udahili.

“Pata taarifa kupitia tovuti ya TCU, portali za vyuo zilizoidhinishwa na matangazo ya vyombo vya habari ya TCU,” Profesa Kihampa aliongeza.

TCU pia imetoa onya dhidi ya mawakala wadanganyifu. “Wasiliana moja kwa moja na vyuo kwa maswali yanayohusiana na udahili. Kuwa makini na epuka mawakala feki,” amesema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi