Dar es Salaam. Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive (Jiji), Janeth Mgaya amejitoa katika kesi inayomkabili Amina Ramadhani na wenzake 17, baada ya upande wa utetezi kudai amekuwa akiwatolea maneno ya ukali na kuwafokea mawakili hao pamoja na wateja wake.
Amina na wenzake 17 wanadaiwa kuwa Juni 14, 2024 maeneo ya Sinza Mori, walitenda vitendo visivyo vya heshima kwenye sehemu za umma, huku wakiwa wamevaa mavazi ya ovyo kwa ajili ya ukahaba.
Wakili wa utetezi, Peter Madeleka amedai leo Juni 26, 2024 kuwa jana alimwandikia barua Hakimu Mgaya kuwa ajitoe kusikiliza kesi hiyo, ili haki itendeke.
“Mheshimiwa tumekuandikia barua Juni 25, 2024 ujitoe katika kesi hii, unaonekana ni mkali na unatufokea kama wanao, tumeona haututendei haki, hii tunaomba ujitoe,” amesema Madeleka.
Akitoa uamuzi wa suala hilo, Hakimu Mgaya amesema Juni 25,2024 kabla ya kesi hii kuja kwa hoja za awali aliandika barua kuwa wateja wake walitozwa Sh300,000 kwa ajili ya dhamana, hivyo nijitoe na leo hii wakili Madeleka amekuja na hoja nyingine kuwa mimi nina hasira sitafanya haki, ili mtu ajitoe lazima asifungane upande wowote,”amesema Mgaya.
Katika uamuzi huo, amesema Madeleka ameshindwa kuonyesha sheria inasemaje, kwani amezungumza maneno matupu kama debe, hivyo mahakama inakatazwa kusikiliza maeneo matupu bila ya na ushahidi.
Mgaya amesema jukumu la utawala ni kuwa mtu anayetenda haki hatakiwa kufungamana na mtu yeyote, hivyo Katiba ya Tanzania inasema kila Mtanzania ana haki ya kusikilizwa na kujitoa lazima mtu ajiridhishe si kuongea ongea kama debe.
“Aliyoyasema Madeleka hayana pa kusimamia kulingana na mimi, mahakama inataka hakimu isiendeshwe na mtu mwenye maneno matupu,” amesema Hakimu huyo.
Pia alisema haoni shida kuendelea katika kesi hiyo kwa sababu hana haja ya kuendelea na watu wasiofuata utaratibu wa kisheria na kusema anarudisha jalada hilo kwa mfawidhi hadi atakapopangiwa hakimu mwingine kusikiliza kesi hiyo.
Kesi imeahirisha hadi Julai 2, 2024 kwa ajili ya kutajwa.
Mbali na Amina washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Aisha Iddi, Mariana Sia, Mwajuma Hamza, Mariamu Hassan, Najma Hamisi, Sabrina Gabriel, Mariam Kitamoga na Elizabeth Michael.
Wengine ni Rosemary John, Recho Kindole, Lobi Daudi, Diana David, Jackline Daniel, Mwajuma Bakari, Jenifa John, Zainabu Hamisi, Recho Bakari.
Wakati huohuo, shahidi wa kwanza, ofisa wa kituo cha polisi Mburahati, Peter Mpozi katika kesi inayowakabili washtakiwa watano ameieleza mahakama hiyo jinsi walivyowakamata washtakiwa hao wakiwa pembezoni mwa barabara inayotoka Tiptop kuelekea mtaa wa Madizini Manzese.
Inadaiwa Juni 14, 2024 maeneo ya Tiptop washtakiwa hao walitenda vitendo visivyo vya heshima kwenye sehemu za umma, huku wakiwa wamevua mavazi ya ovyo sehemu ya umma Kwa ajili ya ukahaba.
Washtakiwa hao ni Mwazani Nassoro, Mariam Mkinde, Mwanaidi Salilum, Faudhia Hassan na Tatu Omary.
Mpozi akiongozwa na Wakili wa Serikali, Mwasiti Ally mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Rachel Kasebele amedai Juni 16, 2024 akiwa kazini aliitwa na mkuu wa kituo, Edward Masunga kuna malalamiko ya wakazi wa eneo la Tiptop ikifika saa 3 usiku wasichana na wanawake ambao wanavalia nusu utupu wanajipanga katika barabara hiyo.
Amedai washtakiwa hao wamekuwa wakijipitisha katika maeneo hayo kwa lengo la kuwashawishi wanaume kwa ukahaba.
“Hizi taarifa zilimfikia mkuu wa wilaya ya Ubungo, amemuagiza mkuu wa kituo azifanyie kazi ndipo aliunda kikosi kazi waliovalia kiraia kwa ajili ya kufika eneo hilo ili wachunguze,” amedai Mpozi.
Ameieleza baada ya uchunguzi walibaini ni kweli watu hao wanafanya vitendo hivyo na waliwakamata wakiwa askari polisi watano, wakiwemo wawili wa kike.
Juni 17, 2024 walifika eneo hilo saa 9:30 usiku waliwakamata washtakiwa hao wakiwa karibu na baa ya Tiptop wakijihisisha na ukahaba wakiwa wamevalia nguo ambazo vitovu, mapaja na tumbo vikiwa wazi.