Kitaifa
Hatima nafuu ya maisha mikononi mwa wabunge
Dodoma. Unaweza kusema hatima ya maisha ya Watanzania kwa siku 365 zijazo kuanzia Julai mosi, mwaka huu ipo mikononi mwa wabunge, ambao leo wanaanza kujadili mapendekezo ya Bajeti ya Serikali.
Wabunge wanaanza mjadala wa bajeti ambayo tayari imeibua vilio vya kodi na tozo katika bidhaa na huduma kutoka miongoni mwao na kwa wadau wengine mbalimbali.
Pia, kikokotoo cha wastaafu, madeni ya makandarasi wa ndani na kilimo cha umwagiliaji ni miongoni mwa maeneo ambayo wananchi wanatarajia kuwaona wawakilishi wao wakiyashikia bango na kuishauri vilivyo Serikali, ili kutokusababisha ugumu wa maisha.
Utaratibu unaotumika hapa nchini ni Serikali kuwasilisha bajeti yake bungeni, wabunge huijadili na kutoa maoni kabla ya kupiga kura ya mwisho, kwa ufupi wawakilishi hao wa wananchi ndio wenye mamlaka ya kuifanyia marekebisho, kuipitisha au kuikataa.
Bajeti hiyo ya Sh49.35 trilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ilisomwa bungeni Juni 13 mwaka huu na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na kupokewa kwa hisia tofauti, hususan katika suala la ongezeko la matumizi ya Serikali.
Pia, kuna ongezeko la kodi katika baadhi ya maeneo, hali inayoelezwa na wataalamu kuwa inaashiria kutakuwa na maumivu kwa wananchi na ugumu wa kufanya biashara, endapo marekebisho hayatafanyika.
Akizungumzia wajibu wa wabunge katika mjadala huo unaoanza leo hadi Juni 26, Mhadhiri msaidizi wa benki na fedha katika Chuo kikuu Ardhi (ARU), Aziz Rashid alisema wawakilishi hao wanalo jukumu la kuhakikisha bajeti inaakisi uchumi wa jumla.
“Ukiangalia bajeti iliyowasilishwa bungeni, sehemu kubwa ya fedha za maendeleo zinaelekezwa kwenye miradi mikubwa ya kimkakati, ambayo kwa sehemu kubwa inatekelezwa na wageni na wazawa hawanufaiki nayo moja kwa moja,” alisema.
Alisema kuna haja ya Bunge kusisitiza manufaa ya wazawa katika bajeti ya Serikali ili fedha za miradi ya maendeleo zianze kunufaisha Watanzania hata kabla ya mradi wenyewe kukamilika.
“Matumizi ya Serikali yanatakiwa kunufaisha wananchi kupitia mnyororo mzima wa thamani,” alisema Rashid.
Aliongeza, ili kukuza uchumi huo wa jumla ni vyema pia Serikali ikawa na bajeti inayolinda uzalishaji wa ndani na kama kuna mahitaji yoyote ya kisera ya kuongeza uzalishaji huo, Serikali haina budi kuyafanyia kazi.
Bajeti iliyowasilishwa ina pendekezo la tozo mpya ya Sh382 kwa kila kilo moja katika gesi asilia inayotumika kwenye magari (CNG), ambayo mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Ernst & Young (EY), Joseph Sheffu alisema kuna haja ya wabunge kuiangalia upya kwa kuwa tozo hiyo inaifanya gesi hiyo kuuzwa Sh1,932 kwa kilo kutoka Sh1,550 za awali.
“Katika tozo hiyo mapato yanayolengwa siyo mengi, kwa kuwa wanaotumia CNG kwenye magari ni wachache na kwa ongezeko hili la gharama huenda kasi ya wanaobadilisha mifumo vyombo vyao ili vitumie gesi ikapungua kwa kuwa nishati hiyo inakuwa kama mafuta. Serikali ingesubiri kwanza watu wawe wengi, ndipo tutoze,” alisema Shefuu.
Mfumuko wa bei
Kwa upande mwingine, Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee alisema mfumuko wa bei mara zote huwa unachangiwa na ongezeko la bei za nishati ya kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Gesi asilia tunazalisha nchini na tuna udhibiti nayo, ikiwamo kuipangia bei. Kampeni ya matumizi ya gesi asilia na bado haijashika kasi sana na magari yanayotumia yako kwenye mikoa michache sana ikiwamo Dar es Salaam, hata magari ya Serikali si yanayotumia gesi,” alisema.
“Kilichotakiwa ni kuongeza nguvu kwenye kampeni ya matumizi ya gesi asilia ili kupunguza gharama za uzalishaji na maisha kwa Watanzania, kuliko inavyofanyika,” alisema.
Kikokotoo mwiba
Katika hatua nyingine, Mdee, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), alisema kinacholiliwa na wafanyakazi si asilimia, bali ni fomula inayotumika kupata mapato ya mwisho ya mfanyakazi.
“Serikali imeongeza asilimia ya kikokotoo kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40 kwa wafanyakazi wa Mfuko wa Umma wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF) na asilimia 35 kwa wastaafu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), hoja hapa si asilimia, ni fomula (kikokotoo), sijui kama umenipata?
“Fomula ya mafao ya kustaafu kwa malipo ya mkupuo zamani ilikuwa inagawanywa kwa 540, lakini fomula mpya na ambayo ndiyo inalalamikiwa, inagawanywa kwa 580. Hapo utaona kugawa kwa 580 malipo yanakuwa madogo, lakini ukigawa kwa 540 malipo yanakuwa makubwa, hiyo ndio hoja na si asilimia (ambayo imeongezwa),” alisema Mdee.
Madeni ya makandarasi
Wabunge pia watalazimika kuibua hoja madeni ya makandarasi wa ndani yanayodaiwa kufikia takriban Sh1.8 trilioni, ambayo wengi wao wameigusia kwenye michango yao ya bajeti ya wizara za kisekta.
Akizungumzia hilo, Mdee alisema tatizo ni kuwa kwenye mapendekezo ya Bajeti ya Serikali hakuna mpango uliobainishwa wa kulipa madeni hayo.
“Makandarasi wa ndani wengi wanafilisika kwa kuwa mitaji yao waliikopa benki, na vilevile wanaihitaji kwa matumizi yao. Hawa wamekuwa wakitoa huduma kwa Serikali, bahati mbaya madeni yao hayana riba hata wadai kwa miaka 20, watalipwa kilekile wanachodai.
“Tofauti na makandarasi wa nje, wao ukichelewa kuwalipa, riba inaongeza deni. Wao ukichelewa kuwalipa wala hawahangaiki, wanajua riba inaongezeka,” alisema.
Alisema tatizo lingine litakaloibuka ni fedha za Mfuko wa Barabara ambazo zipo kisheria, kuelekezwa kwenye matumizi mengine.
Mbali na hayo, Peter Olumi, mfanyabiashara jijini Dodoma alisema wabunge wanatakiwa kuishauri Serikali kupanua wigo wa walipa kodi kwa kuwaingiza wamachinga katika utaratibu wa kulipa kodi, kwa kuwa mapato yao yamekua na wengine hata kuwazidi wafanyabiashara.
“Sasa hawa watu (wamachinga) wajengewe mioyo ya kulipa kodi kuongeza wigo wa walipakodi ili kutowabana walewale (wachache). Maana hawa wa kati, wao wanabakia pale kwa sababu kila kodi ikija inawalenga wao na wafanyabiashara wakubwa,” alisema.
Olomi alisema kilio chao ni kundi la wamachinga, wakiwemo wanaofanya biashara ya bodaboda, nao waanze kuchangia katika uchumi kwa kulipa kodi na hivyo kuwapunguzia mzigo wafanyabiashara wengine, hasa wa kati.
Aidha, Olomi alisema halmashauri zinatakiwa kutenga maeneo maalumu ya kufanyia biashara ili kuepusha kufanyia biashara kila mahali kwenye miji mikubwa.
“Nimetoka Nairobi (Kenya), nimeona kuna nidhamu ya kipekee sana. Ningeshauri masoko ya usiku yawepo na zile barabara za kufungwa nyakati za weekend (mwisho wa juma) zirudishwe ili kujenga nidhamu ya kutofanya biashara kwa kutembeza,” alisema.
Umwagiliaji uvaliwe njuga
Ushauri mwingine kwa wabunge umetoka kwa Daudi Mwaka, mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Zabibu, kuwa wajikite katika kuongeza kilimo cha umwagiliaji kwa sababu kitawafanya wakulima kuongeza uzalishaji badala kutegemea misimu ya mvua.
“Wabunge wasimamie fedha zilizotengwa kwa ajili ya umwagiliaji kwa kuhakikisha zinatumika ipasavyo na matokeo yanaonekana,” alisema.
Alisema licha ya uzalishaji, mkazo zaidi unatakiwa katika eneo la masoko kwa kuhakikisha kuwa mkulima anapozalisha anauza alichozalisha baada ya kukiongeza thamani ili kupata bei nzuri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mstaafu wa Kanda ya Ziwa wa Chama cha Wafugaji, Tanzania, Charles Malangwa, aliipongeza Serikali kwa kusikiliza kilio cha wafugaji kwa kuanzisha Wakala wa Mifugo nchini na kutenga fedha kwa ajili ya chanjo za mifugo.
Hata hivyo, aliwataka wabunge kujikita katika kubadilisha maisha ya wafugaji kwa kuwahimiza kulima malisho kwa ajili ya mifugo yao.