Kitaifa
Sh87 bilioni zatumika miradi ya maji Mtwara
Mtwara. Zaidi ya Sh87 bilioni zimetumika mkoani Mtwara katika ujenzi wa miradi saba ya maji, ambayo baada ya kukamilika kwake itawanufaisha wananchi zaidi ya 600,000.
Miradi hiyo inajumuisha mradi mkubwa wa Makonde wenye thamani ya Sh84 bilioni.
Akizungumza mara baada ya mradi huo kuzinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa, Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Mtwara Primy Damas amesema miradi hiyo inafanya upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Mtwara kuwa asilimia 74 ambapo awali ilikuwa 67.
Amesema kuwa miradi hiyo saba, miwili imetembelewa lakini mitano imezinduliwa na Mwenge wa Uhuru na tayari wananchi wameshaanza kupata huduma hiyo.
“Malengo ya kitaifa ya upatikanaji wa maji unatakiwa ufikie asilimia 85 hadi kufikia 2025 ambapo mpaka sasa tuko asilimia 74 na bado tuna miradi mingine inajengwa ikiwemo mradi wa Makonde Newala, ambao utawahudumia wananchi 600,000 mijini na vijijini na miradi mingine itaongeza asilimia za upatikanaji wa maji katika mkoa wetu wa Mtwara,” amesema Damas
Kwa upande wake, Meneja wa Ruwasa Nanyumbu Saimon Mchucha, amesema kuwa mradi huo utahudumia wakazi 3,565 sawa na ongezeko la asilimia mbili ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Nanyumbu.
“Unajua chanzo cha maji tunachotumia ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 7000 kwa saa katika mkakati wa kuhakikisha chanzo cha maji cha mradi kinakuwa endelevu,” amesema Mchucha.
Naye Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike, amesema kuwa mradi huo unaenda kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji katika vijiji viwili vya makome A na B.
“Mradi huo umefikia asilimia 70 na unatarajia kuhudumia wananchi wapato 1,584 kati ya hao 858 wanatoka kijiji cha Makome na 726 wanatoka katika kijiji cha Makome B, ambao ulianzishwa kwa lengo la kusogeza na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara”
Naye Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Tandahimba Antideus Mchunguzi amesema kuwa zaidi ya vijiji saba vinatarajia kunufaika katika katika kata ya Mkundi wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara.
Amesema kuwa mradi huo utanufaisha zaidi ya wananchi 10,000 kwa kuwapatia huduma ya maji safi na salama katika mradi wa unaosimamiwa na Wakala wa Maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) ambao umegharimu zaidi ya Sh1.4 bilioni.
Naye Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Masasi Juma Yahaya, amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi na salama na kusogeza maji karibu na wananchi.
“Zaidi ya wakazi 1000 wa kijiji cha Namatunu wilayani Masasi wameipongeza Serikali kwa ujenzi wa mradi wa maji ambao umegharimu zaidi ya milioni 300 ili kusogeza huduma kwa wakazi hao.