Connect with us

Makala

Watumiaji soda, juisi hatarini kupata shinikizo la juu la damu

Dar es Salaam. Wanywaji wa soda, juisi za kusindikwa viwandani na vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) wako katika hatari ya kupata shinikizo la juu la damu, imeelezwa.

Kwa wanywaji wa bia, ingawa hakuna kiwango maalumu kilichowekwa katika miongozo ikiwamo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwamba ni kiasi gani cha kunywa kwa siku, wanashauriwa kutumia kiasi kidogo kulingana na afya ya mnywaji kuepuka kupata maradhi hayo.

Kwa wagonjwa wa shinikizo la juu la damu, wenye shida ya moyo au changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza wameshauriwa kutotumia bia.

Hayo yamebainishwa leo Mei 16, 2024 na Ofisa Lishe kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Husna Faraji, wakati wa utoaji huduma ya matibabu bure mkoani Dar es Salaam katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani.

Amesema unywaji wa vinywaji hivyo unachochea shinikizo la juu la damu.

“Vinywaji vyenye sukari nyingi kama vile soda, juisi na energy vinasababisha mtumiaji kuongezeka uzito haraka, pia vina kemikali nyingi zinazosababisha kushusha kinga ya mwili. Kunywa kila siku si salama,” amesema.

Husna amesisitiza watu kufanya mazoezi angalau ya kutembea na wanaoweza kuogelea wafanye hivyo, na kuzingatia lishe sahihi.

Gharama za matibabu

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Hospitali ya Dar Group, Baraka Ndelwa amebainisha changamoto kwa wagonjwa wengi kushindwa kumudu gharama za matibabu ya ugonjwa wa shinikizo la juu la damu.

Amesema gharama za matibabu ni kubwa na wagonjwa wengi hushindwa kumudu, hivyo wanapotoa huduma bure inasaidia wengi.

“Kuanzia vipimo hadi matibabu ni gharama, wagonjwa wengi kiuchumi hawako vizuri, hivyo huduma kama hizi inakuwa ni changamoto kwao,” amesema.

Kwa mujibu wa Husna gharama ni kati ya Sh2 milioni hadi Sh6 milioni kutegemea na aina ya tatizo.

Dk Ndelwa amesema mkakati wa Serikali wa kuhakikisha bima ya afya kwa wote inapatikana huenda ukasaidia katika utoaji huduma.

Leo Mei 16, 2024 na kesho Mei 17, kwa mujibu wa Dk Ndelwa wanatarajia kuwahudumia wagonjwa 500.

Baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma wamesema wanapopata mahali pa kufanya vipimo na kupata dawa bure inakuwa nafuu kwao.

Omary Seif, mkazi wa Buza amesema aliposikia kuna huduma hiyo inatolewa aliwahi kutokana na maumivu anayoyapitia ya presha tangu mwaka 2020.

“Ikipanda hata kuona nashindwa, huwa nafanya kliniki Muhimbili, niliposikia JKCI Hospitali ya Dar Group wanatoa matibabu bure leo sikupata usingizi,” amesema.

Faraja Suleiman, mkazi wa Gongo la Mboto amesema kuna nyakati anakwama kutibiwa kutokana na kutokuwa na bima ya afya hivyo kushindwa kumudu gharama za matibabu.

“Nina presha ya kupanda muda mrefu, ambacho nimejitahidi ni kuishi kwa kuzingatia miiko. Gharama za matibabu ni kubwa,” amesema.

Dk Ndelwa amesema tatizo la shinikizo la juu la damu ni kubwa nchini na linaendelea kuwa kubwa kwa kuwa ugonjwa huo na kisukari yanaambatana na mtindo wa maisha.

Amesema katika bia kinachopatikana ni sukari.

“Mfano mtu amekula wali na maharage mchana, kisha akaenda kunywa bia, hiyo ni kwamba anaenda kula chakula kingine, hivyo atakuwa amekula milo miwili, mtu huyo hafanyi mazoezi, moja kwa moja ataanza kuongezeka uzito,” amesema.

Amesema asubuhi kuna mtu atakunywa supu na chapati akimaliza anakunywa soda, akieleza ulaji huo haufai.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi