Connect with us

Kitaifa

Mbunge asisitiza wabakaji, walawiti wahasiwe

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kilimanjaro, Shally Raymond amesisitiza pendekezo la muda mrefu la baadhi ya wabunge la kuhasiwa wanaume wanaopatikana na hatia ya ubakaji ama ulawiti kwa watoto.

Mbunge Shally Raymond amesema hayo leo Jumatatu ya Aprili 29, 2024 wakati akichangia mjadala bungeni wa taarifa ya mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Amesema tatizo la wabakaji limekuwa la muda mrefu na wabunge nao kwa muda mrefu wamekuwa wakiiomba Serikali ilete bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria, kwa ajili ya kutunga adhabu ya kuhasiwa kwa wanaume wanaopatikana na hatia.

Kwa mujibu wa Raymond ameshangaa ni kwa nini mapendekezo hayo ya wabunge yamekuwa hayatekelezwi kwa kuletwa muswada bungeni.

Ni hoja ya muda mrefu

Mwaka 2020, mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu Katimba (Kwa sasa ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Elimu, aliishauri Serikali kuweka adhabu kali kwa wabakaji ikiwemo kuhasiwa.

Akizungumza bungeni Februari 4, 2020, Zainabu alisema, masharti ya kuthibitisha ubakaji yamekuwa magumu hasa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18, ni vema utaratibu huo ukaangaliwa vizuri.

Pia, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Arumeru Magharibi, Dk Thea Ntara aliwahi kupendekeza kuwa wanaume wanaopatikana na hatia ya ubakaji ama ulawiti kwa watoto wahasiwe.

Wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi kwa mwaka wa Fedha wa 2022/23, baadhi ya wabunge walipendekeza wabakaji wahasiwe.

Mmoja wa wabunge hao, Subira Mgalu (Viti Maalumu), alisema takwimu matukio ya kulawiti ambapo watoto wa kiume zaidi ya 3,000 kati ya 3,260 sawa na asilimia 64 wamelawitiwa inatisha.

“Mpaka tunatamani kama adhabu iongezwe au tuseme wanaume wahasiwe hii yote ni kuona namna gani tunaweza kuondoa ukatili huu wa ulawiti na ubakaji wa watoto,” alisema.

Pia, miaka ya nyuma mbunge Esther Nyawazwa akiungwa mkono na wabunge wengine alitaka adhabu kali kwa wabakaji na wanaolawiti watoto. “Ili kukomesha visa kama hivyo tunahitaji hukumu kali kupita kiasi, mfano adhabu ya kifo,” alisema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi