Kitaifa
Serikali kupitia upya faini bajaji za mizigo
Dodoma. Serikali imesema maboresho ya faini zinazotozwa kwa pikipiki za magurudumu matatu ‘bajaji’ zinazobeba mizigo yatakamilika kabla ya mwaka ujao wa fedha.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Aprili 17, 2024 na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alipojibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Ng’wasi Kamani.
Kamani ameuliza iwapo Serikali haioni haja ya kupunguza faini za bajaji za mizigo kwa makosa ya kukosa leseni ya usafirishaji kutoka Sh250, 000 hadi Sh25, 000.
Kihenzile amesema Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kupitia Wizara ya Uchukuzi, imeshafanya mapitio ya Kanuni za leseni za Usafirishaji (magari ya mizigo) za mwaka 2020.
“Miongoni mwa maboresho yaliyofanywa ni pamoja na kupunguza faini za pikipiki za magurudumu matatu,” amesema.
Naibu waziri amesema rasimu ya mapendekezo ipo katika hatua za majadiliano ya wadau.
Amesema Latra itaandaa mikutano ya wazi kwa lengo la kujadili na kupitisha viwango vya faini vitakavyokubalika.
“Nitoe rai kwa watumiaji wa vyombo vya barabarani kuzingatia sheria kuepuka kulipa faini zisizo za lazima,” amesema.
Katika maswali ya nyongeza, mbunge huyo amesema bajaji za mizigo hivi sasa ziko katika kiwango sawa na malori ya mizigo wakati haviendani lakini vyombo hivyo vinatozwa faini zilizo sawa.
“Ni lini kanuni au mchakato huu utakamilika ili tubadilishe sheria hizi na watu wa bajaji kupigwa faini zinazoendana na thamani ya vyombo vyao?” amehoji.
Kihenzile amesema watakapofika katika majadiliano watapima kulingana na hali halisi ya wakati kama iwe Sh25, 000 au kiasi kingine kitakachoonekana kinafaa kwa wakati huo.
“Tunaamini maboresho haya yanaweza kukamilika kabla ya mwaka huu wa fedha na hivyo ianze kutumika,” amesema.