Kitaifa
Usimamizi mbovu miradi ya maendeleo Dk Nchimbi atoa maagizo
Rukwa. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amezitaka taasisi za Serikali zinazotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, kuhakikisha inazingatia ubora na viwango ili thamani halisi ya fedha ionekane.
Dk Nchimbi ameeleza hayo leo Jumatatu Aprili 15, 2024 alipokuwa akikagua ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa mkoa wa Rukwa uliopo manispaa ya Sumbawanga.
Katika ukaguzi huo, Dk Nchimbi aliambatana na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla na Katibu wa Oganaizesheni, Issa Ussi Gavu.
“Tunapojenga vitu ambavyo vinatarajia vikae miaka 40 halafu vinadumu kwa miaka mitatu huko ni kukosa uzalendo wa hali ya juu, na wakati mwingine ni rushwa za ‘kipumbavu’ watu wanaacha masilahi ya Taifa wanazingatia ya kwao.”
“Tunatoa wito kwa wataalamu wetu wote kuhakikisha wanazingatia masilahi ya Taifa wanaposimamia hii miradi inayotumia fedha nyingi za umma, ili ijengwe kwa ubora na thamani halisi ya fedha inayotumika ionekane,” amesema Dk Nchimbi.
Mbali na hilo, Dk Nchimbi amewataka watendaji wa Serikali kuzingatia suala la mikataba kama wamekubaliana miaka kadhaa basi iwe hiyo.
Katibu mkuu huyo, amefafanua kuwa uamuzi wa Serikali kujenga uwanja wa ndege Mkoa wa Rukwa unalenga kutatua changamoto za usafiri kwa wananchi wa mkoa huo.
Amewataka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Rukwa kuhakikisha wanaongeza kasi katika usimamizi wa ujenzi wa uwanja, akisema wananchi wanausubiri kwa hamu.
Awali Meneja wa Tanroads mkoani humo, Mhandisi Mgeni Mwanga amesema ukarabati na upanuzi wa ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Machi mwaka 2025.
Amesema wameanza kuweka tabaka la chini katika eneo la kuruka na kutua ndege na ujenzi wa jengo la abiria litakalochukua watu 100,000 kwa mwaka.
“Gharama ya mradi huu ni Sh60.1 bilioni utekelezaji hadi sasa umefikia asilimia 8.8, lakini mpango ulikuwa asilimia 15 hadi sasa, kwa hiyo mkandarasi yupo nyuma kwa asilimia 6 hivi,” amesema Mwanga.
Naye Makalla amesema mchakato wa ujenzi huo ulikuwa unasuasua, lakini Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kuuvalia njuga kwa kuhakikisha unakamilika ili kurahisisha shughuli za usafiri mkoani humo.
“Tumeshawaambia Tanroads wakamilishe kwa wakati maana CCM tuna jambo letu mwakani, tunataka Rukwa tuje na magari na ndege wakati wote.”
“Iwe jukumu la kila mwanaCCM kueleza haya mambo mazuri kuanzia ngazi ya tawi nataka mtembea kifua mbele Serikali inafanya kazi kubwa ya kuboresha huduma za kijamii,” amesema Makalla.
Kwa upande wake, Gavu amesema dhamira ya CCM ni kuwatumikia wananchi, hivyo waliopata nafasi kupitia chama hicho wahakikishe wanajitoa kwa wananchi katika utekelezaji majukumu yao.