Kitaifa
Ripoti 21 za CAG zatua bungeni
Dodoma. Ripoti 21 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), za ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka 2022/2023 zimewasilishwa bungeni.
Kukabidhi ripoti hizo kunakuja baada ya CAG, Charles Kichere kuikabidhi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Machi 28, 2024 Ikulu, Chamwino jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za leo Jumatatu Aprili 15,2024 iliyotolewa na Bunge, ripoti zilizokabidhiwa ni ukaguzi wa taarifa za fedha za Serikali kuu kwa mwaka wa fedha, ukaguzi wa taarifa za fedha za mamlaka za Serikali za mitaa na ukaguzi wa taarifa za fedha za miradi ya maendeleo.
Ripoti nyingine ni za ukaguzi wa taarifa za fedha za mashirika ya umma, ufanisi na ukaguzi maalumu, mifumo ya Tehama, upatikanaji wa huduma za afya ya akili pamoja na ufanisi kuhusu udhibiti wa vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya vya umma.
Nyingine ni za ufanisi kuhusu udhibiti wa mazao ya biashara, udhibiti wa usambazaji wa mbolea kwa wakulima, udhibiti wa elimu ya ufundi nchini, usimamizi wa urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na ufuatiliaji.
Ripoti nyingine ni ufanisi kuhusu udhibiti na tathmini ya umahiri wa watumishi katika sekta za umma, utekelezaji wa programu za urekebu kwa wafungwa, usimamizi wa mipango miji na usimamizi na ufuatiliaji wa watoa huduma za bima nchini.
Ripoti ya ukaguzi usimamizi wa fukwe, uwezeshaji wa wachimbaji wadogo wa madini, usimamizi wa rasilimali za uvuvi, usimamizi wa uingizaji wa mafuta nchini, taarifa kuhusu ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya kaguzi za ufanisi yaliyotolewa mwaka 2020.
Pamoja na mambo mengine akikabidhi ripoti hiyo kwa Rais Samia, Kichere alisema wamebaini mashirika matano ambayo yamepata hasara ya mabilioni ya shilingi.
Mashirika hayo ni Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Shirika la Reli Tanzania (TRC), Kampuni ya Uwekezaji (Tanoil) na Shirika la Posta Tanzania.
Rais Samia aliahidi kwenda kuzifanyia kazi dosari zilizobainishwa na CAG na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ili zisijirudie.