Connect with us

Kitaifa

Takukuru yabaini safari hewa, udanganyifu vituo vya mafuta

Dodoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imechunguza na kukamilisha majalada 900 yakiwemo 21 yaliyohusu rushwa kubwa zilizohusisha ubadhilifu na hasara kwa Serikali.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni amesema hayo leo Alhamisi, Machi 28, 2024 wakati akiwasilisha taarifa ya taasisi hiyo kwa mwaka 2022/2023 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Katika hizo, imesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilikusanya Sh8.9 bilioni kwa njia ya mashine ya ukusanyaji wa fedha ya Pos lakini fedha hizo hazikupelekwa benki.

Badala yake, amesema watuhumiwa walighushi nyaraka za kuonyesha kuwa fedha hizo zilipelekwa benki.

Vilevile, amesema Takukuru ilichunguza ubadhilifu na ufujaji wa Sh4 bilioni zilizotokana na makusanyo ya Mamlaka ya Hifadhi la Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Uhifadhi wa Bonde la Ngorongoro na Bodi ya Utalii,” amesema.

Akifafanua, Hamduni amesema walifanya uchunguzi wa safari hewa nje ya nchi ambazo zilisababisha hasara Sh1.3 bilioni kwa Mamlaka ya Uhifadhi wa Bonde la Ngorongoro.

Ubadhirifu Uda, Udart

Hamduni amesema pia walichunguza ubadhirifu wa Sh14 bilioni kwa Shirika la Usafirishaji wa Dar es Salaam (UDA), uliofanywa na iliyokuwa menejimenti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart).

Amesema walifanya uchunguzi kuhusu ukodishaji wa maghala ya Uda kinyume cha utaratibu na hivyo kuisababishia Serikali hasara ya Sh20.5 bilioni.

Pia amesema walifanya uchunguzi wa upotevu wa vipuri vya Kampuni ya Uendeshaji ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), ulioisababishia Serikali hasara ya Sh3.29 bilioni.

Hamduni amesema walifanya uchunguzi wa ukiukwaji wa taratibu za ununuzi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwenye Bandari ya Dar es Salaam wakati wa ununuzi wa mfumo wa Enterprise Resource Plan uliofanywa na Kampuni ya Zimbabwe.

Amesema ukiukwaji huo ulisababishia Serikali hasara ya Sh4 bilioni.

Amesema uchunguzi mwingine ulioufanyika ni katika Bandari ya Kigoma ambapo Sh1.6 bilioni zilichepushwa na kufanyiwa ubadhirifu kwa watuhumiwa kughushi saini wakishirikiana na wafanyakazi wa benki.

Hamduni amesema pia walifanya uchunguzi wa uchepushaji wa Sh3 bilioni zilizotolewa na Shirika la Marketing Infrastructure Value Addition and Rural Support Program.

Amesema shirika hilo lilitoa fedha hizo kwa ajili ya kuwezesha kuwainua wananchi vijijini na zililipwa kupitia benki ya KCBL.

Pia amesema walifanya uchunguzi wa Sh4.9 bilioni zilizotolewa na Benki ya Maendeleo ya TIB kwa wafanyabiashara mbalimbali ikiwemo Kampuni ya Heritage Empire Limited bila kuwa na vigezo.

Taarifa za CAG

Hamduni amesema pia walifanyia kazi taarifa zilizotokana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuwa baada ya kuzipitia na kuzifanyia uchambuzi walifungua majalada 375 ambayo yalionyesha viashiria vya rushwa na jinai.

Hata hivyo, amesema majalada 156 yalifungwa kwa kukosa ushahidi wa uwepo wa rushwa au jinai jingine.

Amesema katika majalada 73 watendaji wa Serikali walibainika kukiuka taratibu lakini hawakupata ushahidi wa kijinai.

Taarifa mbio za Mwenge   

Hamduni amesema walifanya uchunguzi wa taarifa zilizotokana na Kiongozi wa Mbio za Mwenge ambapo mwaka jana miradi 20 ilikataliwa kuzinduliwa.

“Kati ya majalada hayo yaliyofunguliwa, 12 uchunguzi wake ulikamilika, moja mtuhumiwa alifikishwa mahakamani na alipatikana na hatia. Jalada moja lilihamishiwa Polisi. Majalada mengine yapo kwa Mwendesha Mashtaka na manane uchunguzi unaendelea,” amesema.

Vituo vya mafuta bila vibali

Hamduni amesema uchambuzi ulihusisha vituo vya mafuta 38 na asilimia 79 ya vituo vilivyofikiwa vilizingatia sheria kwa kuwa na vibali vya ujenzi kutoka halmashauri vilipo.

Ameisema asilimia 21 ya vituo hivyo havikuwa na leseni huku kukiwepo ongezeko la maombi ya ubadilishaji wa matumizi ya ardhi kuwa vituo vya mafuta.

Amesema walibaini ongezeko la vituo vya mafuta katikati ya makazi ya watu na hivyo kusababisha hofu ya usalama kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.

Yapokea kero 6,306

Katika hatua nyingine, Hamduni amesema takukuru imepokea kero 6,306 za wananchi ambazo kama hazifanyiwa kazi zinaweza kusababisha vitendo vya rushwa ama manung’uniko.

aagizo ya Rais Samia yanayohusu kuzuia rushwa, walibuni na kutekeleza programu ya Takukuru rafiki, inayohusisha mikutano ya wanufaika katika ngazi ya kata ambao wanatambua kero katika utoaji huduma au utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema kero zinazotambuliwa huwasilishwa kwa watoa huduma ili waweze kuzipatia ufumbuzi akitahadharisha kuwa endapo hatua hazitachukuliwa, kero hizo zinaweza kusababisha vitendo vya rushwa au manung’uniko ya wananchi katika maeneo husika.

Kupitia mradi huo, kero 6,306 ziliibuliwa na kati ya hizo 3,513 zilitatuliwa.

Hatua hiyo, imepongezwa na Rais Samia katika hotuba yake fupi baada ya kupokea ripoti hiyo, akisema itasaidia kupunguza kero za wananchi na kufanya Serikali kuwajibika ipasavyo.

Yaokoa Sh87.6 bilioni

Hamduni amesema kupitia operesheni za uchunguzi Takukuru imeokoa Sh87.59 bilioni katika kipindi cha mwaka 2022/2023.

Miongoni mwa hizo ni Dola za Marekani milioni 33 sawa Sh76.34 bilioni kupitia uchunguzi wa mkongo wa Taifa.

Alisema imebainika kuwa umoja wa watoa huduma za mawasiliano ulijenga miundombinu ya mawasiliano kinyume na makubaliano na hivyo kuikosesha Serikali mapato kutokana na huduma zao kutopita katika mkongo wa Taifa.

Amesema kupitia mkataba wa makubaliano kati ya umoja wa watoa huduma za mawasiliano na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia, umoja huo ulikubali kulipa Dola za Marekani milioni 20 taslimu katika kipindi cha miaka mitano.

Amesema fedha hizo zitalipwa pamoja na riba ya asilimia 3.5 kila mwaka ili kulinda thamani ya fedha na Dola za Marekani milioni 13 zitalipwa kwa njia ya uwekezaji kati yake na Serikali kupitia wizara husika.

Hamduni amesema Takukuru pia iliokoa Dola za Marekani milioni 2.971 sawa na Sh7 bilioni ambazo zilitokana na mkataba ulioingiwa mwaka 2007 kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya Pangea Minerals.

Amesema pamoja na masharti mengine, mkataba ulikuwa unataka kufunguliwa kwa akaunti ya pamoja (escrow) kwa ajili ya kuweka fedha za kuboresha miundombinu ya umeme katika mgodi wa Buzwagi, zinazolipwa kupitia ankara za bili za umeme za mwezi.

Hamduni amesema Kampuni ya Pangea ilikuwa na jukumu la kukata kiasi cha fedha walichokubaliana na Tanesco na kukiweka katika akaunti hiyo maalumu.

Amesema ingawa hawafungua akaunti hiyo, kampuni hiyo ilikata Dola za Marekani 2.97 milioni kwa ajili ya maboresho ya miundombinu ya umeme na kuzitumia kinyume na makubaliano.

“Baada ya Takukuru kubaini upotevu wa fedha hizo za Serikali, ilianzisha uchunguzi ambao ulisababisha fedha hizo kupatikana,”amesema.

Aidha, Hamduni amesema Takukuru ilifanikiwa kuokoa Sh4.0 bilioni ambazo zilikuwa za halmashauri lakini zilichepushwa nafedha hizo zilirudishwa kwenye akaunti za halmashauri na sekretarieti za mikoa.

Hamduni amesema pia Takukuru ilifanya uchunguzi katika vyama vya ushirika ambapo waliweza kuokoa Sh248.8 milioni ambazo zilirejeshwa kwenye vyama vya ushirika.

Uwazi umesaidia

Akizungumzia taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na Utetezi wa Vijana la Bridge For Change, Ocheck Msuva amesema uwazi na uwajibikaji ndio sababu kubwa ya kuendelea kuona ubadhilifu katika fedha za umma nchini.

“Wananchi lazima watambue ili kuleta utendaji dhabiti si jukumu la Rais pekee yake kuleta uwajibikaji nchini, uwajibikaji unaanzia kwenye serikali za mitaa kwa watu kushiriki katika vikao ili kujua yanayoendelea kwenye mitaa na maeneo yao,” alisema.

Alisema wananchi wanatakiwa kuongeza uwajibikaji, asasi za kiraia zifanye kazi na wananchi kwa karibu pamoja na kubuni miradi ambayo ina tija.

Amesema jambo jingine linalotakiwa kufanywa katika kupambana na rushwa ni kuendelea kuboresha sheria zilizopo ili kuzuia mianya inayoruhusu rushwa na ubadhilifu wa fedha za umma.

“Kama Sheria ya Manunuzi ya Umma imekuaje vitu vimeenda kununuliwa, vikaletwa na vikawa sawa na vikaendelea kutumika na fedha zikalipwa zote. Yaani huo mchakato wa kuidhinisha ulifanyikaje. Inakuaje watu wapate hasara halafu watumie ruzuku kama faida,” amehoji.

Amesema sheria inatakiwa kubainisha kuwa fedha zinazotolewa kwa taasisi za Serikali kama ruzuku zisitumike kama faida bali ziingizwe katika sehemu ya uwekezaji kwa ajili ya kuboresha taasisi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, (Udom), Paul Loisulie amesema hiyo ni hatua mpya ya kuongeza uaminifu kwa tasisi hiyo kwa kitendo chao cha kusikiliza kero za wananchi.

“Hii itategemea wanazitumiaje hizo taarifa, kuna kero nyingine ni za watu kufitiniana, wanapaswa kuwa makini wakati wanapopokea kero kutoka kwa wananchi kwa kujiuliza je, zinaleta haki,” amesema.

Aidha, Loisulie amesema kitendo cha kubaini ubadhilifu licha ya Takukuru kuwepo, kinaonyesha bado vitendo vya rushwa vipo nchini na hivyo Serikali inabidi kubuni njia zaidi za kupambana na tatizo hilo.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi