Kitaifa
Ndege nyingine mpya aina ya Boeing B737-9 Max kuwasili nchini kesho
Dar es Salaam. Ndege mpya ya abiria aina ya Boeing B737-9 Max ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) inatarajiwa kuwasili nchini huku Watanzania na viongozi mbalimbali wakialikwa kwenda kushuhudia mapokezi hayo.
Ndege hiyo inatarajiwa kuwasili kesho kuanzia saa 4:00 Asubuhi Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)Dar es Salaam.
Akizungumzia ujio wa ndege hiyo inayotokea Marekani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kuwasili kwa ndege hiyo ni mwendelezo wa Serikali katika jitihada za kuboresha sekta ya uchukuzi ili kukuza uchumi wa nchi.
“Ujio wa ndege hii ni alama ya ushindi kwa Taifa, na fahari kubwa, hivyo nichukue fursa hii kuwaalika Wakazi wa Dar es Salaam na Watanzania wote kuja kushiriki mapokezi ya ndege hii kuanzia saa 10:00 asubuhi Terminal One katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,” amesema.
Chalamila amezungumzia maandalizi ya mapokezi hayo kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akisema aina hiyo ya ndege ni ya pili kuwasili nchini tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi 19, 2021.
“Tulipokea ndege ya kwanza ilikuwa ya abiria, ikaja ya mizigo na sasa hivi ni ndege ya tatu ya abiria lakini ni ya pili kwa aina ya Max,” amesema Chalamila.
Pia, amesema katika ushindani wa mataifa yoyote duniani silaha moja wapo wanayotumia ni kuboresha sekta ya anga kutokana na umuhimu wake.
“Kwa kutambua hilo Serikali imekuwa ikiweka jitihada ya kufanya mapinduzi katika sekta ya uchukuzi. Kuna maboresho ya reli yanaendelea pamoja maeneo mengine ya sekta ya usafiri kwa mantiki hiyo naalika viongozi wengine wa Serikali, chama, dini, mashirika ya umma na binafsi kushiriki kupokea ndege hii ambayo ni uhodari na alama ya ushindi iliyofanywa na Serikali,” amesema Chalamila.
Kuongezeka kwa ndege hiyo kunalifanya shirika hilo kufikisha ndege 14 kati ya hizo moja ni ya mizigo na zinazobakia zinabeba abiria.
Hii ndiyo Boeing 737-9 Max, tofauti yake na zilizopo
Pengine unaweza kujiuliza ndege hiyo ina uwezo gani na sifa zake nyingine ni zipi ikilinganishwa na ndege ambazo tayari zipo katika shirika la ndege la Tanzania (ATCL).
Uwezo wake wa kupakia abiria ni wastani wa abiria 220 kulingana na mpangilio wa ndani huku ikisafiri hadi umbali wa kilometa 6,110 bila kulazimika kutua.
Ndege hiyo ambayo toleo lake la kwanza lilitoka mwaka 2017 inatumia injini ya LEAP-1B ambayo inatengenezwa na CFM International ya Marekani. Gharama yake inatajwa kuwa Dola za Marekani milioni 128.9 hadi 135 (Sh323.79 bilioni hadi Sh339.12 bilioni).
Urefu wake ni mita 42.16 na upana wa mabawa yake ni mita 35.9 inaendeshwa na marubani wawili na wahudumu wa ndani ya ndege wanne. Tanzania ambayo imenunua jumla ya ndege mbili inakuwa nchi ya nne bara ni Afrika kumiliki ndege hiyo baada ya Nigeria (18), Ethiopia (17) na Afrika Kusini (5).
Jumla ya oda za Max 9 tangu mwaka 2017 ni zaidi ya 5000 hadi Agosti 31, 2023 hata hivyo zilizokwisha kufikishwa kwa wanunuzi ni zaidi ya 1200.
Kwa mwaka huu tayari wamewafikishia wateja wao ndege 344 nyingi zikiwa ni Max 9.
Ukiachana na ndege za ATR-72 na Bombardier Q400 zinazotumia injini za mapanga katika anga la Tanzania, ndege za ndani za abiria zitumiazo injini ya ‘Jet’ ni Airbus A220-300 na Boeing 787-9 (Dreamliner) zote zinazoendeshwa na ATCL.
Tofauti kubwa ya Max 9 na A220 ni uwezo wa abiria kwa kuwa ni A220 uwezo wake wa juu ni kupakia abiria 160 wakati Max 9 uwezo wake wa juu ukiwa ni abiria 220.
Umbali wa kuruka bila kusimama Max ni kilometa 6,570 huku A220 ikiwa ni 6,112 huku uwezo wa kupaa ukiwa na mzigo ni tani 67.5 kwa A220 na tani 88.3 kwa Max 9.
Spidi ni kilometa 840 kwa saa A220 huku ya Max 9 ikiwa pungufu kwa kilometa moja kwa saa (839). Bei ya A220-300 inatajwa kuwa Dola milioni 91.5 (Sh233.7 bilioni).
Ukizilinganisha ndege hizo mbili na Dreamliner imeziacha mbali, kwanza uwezo wake wa kupakia abiria ni 242 na ina uwezo wa kuruka ikiwa na uzani wa tani 227.9 huku uwezo wake wa juu ukiwa ni spidi ya kilometa 954 kwa saa.