Connect with us

Kitaifa

Matumaini ya mawasiliano daraja la Somanga yaanza kurejea

Baada ya Daraja la Somanga kukatika na kukata mawasiliano ya Barabara ya Somangafungu tangu jana Machi 24, 2024, bado wananchi wanaotumia barabara hiyo wameendelea kusota kwa kusubiri ukarabati wake unaoendelea.

Baadhi ya wasafiri na wakazi wa maeneo hayo  waliozungumza na Mwananchi Digital wanasema hali hiyo imechangia kuongezeka kwa gharama hususan za mahitaji muhimu ya kujikimu.

Hata hivyo wanasema kadiri muda unavyokwenda, ndivyo matumaini ya kurejea kwa mawasiliano hayo yakiongezeka.

“Hili daraja limetuathiri, mimi nilitakiwa kufika Dar jana, lakini hali ndiyo hii unayoiona na nilitakiwa kuingia kazini. Hatuwezi kulalamika sana lakini kutokana na miundo mbinu yetu ilivyo kaa, hatuna namna,” amesema msafiri mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Danny.

Anasema tangu kukatika kwa mawasiliano hayo jana, gharama za vitu katika eneo hilo zimepanda.

“Kwa mfano sasa hivi tumeingia kwenye matumizi ya dharura ambayo hayakuwa kwenye bajeti na wengine wanawagonjwa,” anasema Danny.

Daraja hilo linaunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Lindi Mtwara na Ruvuma.
Hata hivyo Mwananchi Digital imeshuhudia baadhi ya vifaa kwa ajili ya ukarabati wa daraja hilo vikiendelea kushushwa na kazi ya ukarabati ikiendelea kwa kasi.
Jana Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alisema Serikali inafanya jitihada za kuyarejesha mawasiliano hayo kabla ya mchana wa leo.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi