Connect with us

Kitaifa

Sababu wananchi Dar kujijengea barabara

Dar es Salaam. Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Kinzudi Kata ya Goba Wilaya ya Ubungo jijini hapa wameanza kampeni ya kuchangishana fedha zitakazofikia Sh180 milioni, kwa ajili ya kujenga  barabara na mitaro ili kukabiliana na adha wanayopitia msimu wa mvua.

Wakati ujenzi huo ukiwa umeanza, hadi sasa wamechangisha Sh22 milioni, wakisema wameisubiri Serikali kwa zaidi ya miaka 10 bila mafanikio.

Hata hivyo, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Mkoa wa Dar es Salaam, Geoffrey Mkinga alipoulizwa kuhusu ujenzi huo, amesema anafahamu suala hilo na wametenga bajeti ya kuwaongezea.

“Serikali kupitia Tarura tumetenga kwenye bajeti Sh239 milioni kwa ajili ya kwenda kuunga mkono juhudi zao kwa kuitengeneza barabara hiyo kwa kilomita zote mbili,” amesema.

Akizungumza ujenzi huo, mkazi wa eneo hilo aliyechaguliwa na wakazi hao juzi Machi 19, 2024, Mhandisi Edson Misana amesema barabara hiyo inayoitwa Awadhi ina urefu wa kilomita mbili inatoka Goba na inakuja kutokea Salasala.

“Sisi wananchi wa eneo hili tunaitumia njia hii kwenda kwenye shughuli zetu na kurudi makazi yao, hatuna njia nyingine mbadala na kipindi hiki cha mvua gari ikikwama usafiri unaacha njiani, unaenda nyumbani kwa miguu maana hata pikipiki haipiti,” amesema.

Mwananchi limefika katika mtaa huo na kukuta bango lenye kichwa cha habari, “Wakazi wa Barabara yay a Awadh-KKKT Kinzudi (KM2).”

Misana amesema waliandika bango hilo lililojengwa mita 100 kutoka usawa wa barabara hiyo ili kutoa taarifa na kuhamasisha wakazi wa eneo hilo kuchanga michango yao katika kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo.

 “Baada ya kuweka bango hili matokeo yamekuwa mazuri, kwani tumepata Sh3 milioni, ina maana mwamko umekuwa mkubwa kila mmoja anajua anatakiwa kuchangia kufanikisha ujenzi,” amesema.

Baada ya hapo, amesema waliendelea kukusanya fedha zilizofikia Sh22 milioni na wameshatumia Sh14 milioni kati ya walizochanga na wanaendelea kununua vifaa vinavyohitajika kama saruji kokoto na vingine.

“Bajeti yetu hadi kufanikisha ujenzi si chini ya Sh180 milioni, kwa nguvu za wananchi hatuwezi kufanikisha mara moja na ukiangalia katika bango letu tunasema kabisa wataendelea kuchangisha hadi Mei mwaka huu,” amesema.

Amesema baada ya hapo watakaa na kutathimini kwa kazi iliyofanyika na kinachohitajika, lakini iwapo Tarura watakuja kuwashika mkono kiwango kitakachokuwa kimechangwa watakihamishia sehemu nyingine.

Amesema watu wanajitoa kutoa michango kulingana na walivyojaliwa kipato lakini waliweka kiwango cha kuanzia ni Sh400, 000 hadi 500,000 na kwenye kundi lao la M-koba walioahidi kuchanga wapo 105.

Amesema wamejipanga kwa wale wanaochimba mitaro wanalipwa kwa siku sawa na wale wanaomwaga zege kujenga mitaro hiyo kuhakikisha maji yasiharibu barabara.

Namna ya kuchangia

Amesema kuna wanaotoa fedha taslimu na mfumo mwingine fedha inatumwa moja kwa kwa moja katika akaunti ya M-koba jina ‘Wadau Awadh Road.”

Amesema wajumbe wa nyumba 10 walishirikishwa kuongea na wakazi waliopakana na barabara ili kuwaomba kujitolea eneo kwa upanuzi wanjia na kutatua migogoro midogo inayojitokeza.

Mwenyekiti wa usimamizi wa ujenzi huo kwa niaba ya wananchi wa eneo hilo, Joseph Mboya amesema barabara hiyo hutumiwa na wakazi wengi ikiwamo magari ya watoto wa shule.

“Tuliona kusubiria bajeti ya Serikali tunaweza kuchelewa kufanya mambo yetu mengine na kuna wakati tuna wabeba watoto hadi barabarani wakapande gari waende shule,” amesema.

Amesema kutokana na shida hiyo wakazi wa eneo hilo waliwatafuta wadau kwa kuzingatia kazi zao wanazojijua kuwasaidia na waliojitoa kuchanga kiasi cha fedha na wengine walitoa vifaa.

“Baadaye tuliwafuata wataalamu watupe ramani na namna ya kujenga walitushauri kujenga kidogo kidogo na tumeanza kushughulika na maeneo korofi zaidi,” amesema.

Amesema jitihada za kujenga barabara hiyo si mara ya kwanza mwaka uliopita walichangishana na kuweka kifusi lakini mvua ziliponyeka zilisambaratisha barabara yote.

“Tulishangisha Sh15 milioni tukabebelea kifusi kuweka sehemu zote korofi na Tarura walikuja tena kutuunga mkono kumwaga kokote magari mawili vyote vilisomwa kwa sababu barabara haikuwa na mitaro ya kupitisha maji,” amesema.

Hata hivyo, Mboya amesema kuna baadhi ya watu wakiambiwa kuchangia wanaona kama si sehemu ya kazi yao huku wakieleza wanakatwa kodi, hivyo wanataka Serikali itekeleze wajibu huo wa kuwafikishia huduma.

“Inakatisha tamaa kwa wengine wanaochangia kwa sababu si wote wanaochanga wana uwezo lakini wanajibana,” amesema.

Amesema changamoto nyingine siasa zimekuwa nyingi kuna wanaodhani kwa kuwa wanaelekea kwenye chaguzi zijazo walio mstari wa mbele kupigia debe ujenzi huo wanadhani baadhi wanatafuta umaarufu ili wagombee.

“Kumbe sisi tunapambana ili tupate amani tupite bila shida,” amesema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi