Kitaifa
Kitakachofanyika uwekezaji sekta binafsi reli ya Tazara
Dar es Salaam. Dhana ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi imeanza kutekelezwa nchini kufuatia kampuni binafsi kuingiza treni kwenye reli ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) zitakazosafirisha mizigo kati ya Bandari ya Dar es Salaam na nchi za DRC na Zambia.
Hili linakuja ikiwa imepita miezi mitano baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ziara ya kimkakati nchini Zambia na miongoni mwa mambo yaliyozungumziwa, ni kuifanyia maboresho reli hiyo ili kuongeza kiwango cha mizigo kinachosafirishwa katika reli hiyo.
Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860, ikianza kazi yake mwaka 1976, ilikusudiwa iwe na uwezo wa kusafirisha mizigo tani milioni tano kwa mwaka lakini hadi Juni mwaka jana ilielezwa ilikuwa ikisafirisha chini ya tani milioni moja.
Septemba mwaka jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alifanya ziara Tazara kujionea ufanisi wa reli hiyo na kusema Serikali inafanya jitihada za kuiboresha ili kuongeza uwezo wa idadi ya mizigo itakayosafirishwa na reli hiyo.
Alisema malengo ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kubeba tani za mizigo zaidi ya milioni 30 na si kama ilivyo wakati huo ambapo shirika hilo linasuasua.
Ukurasa mpya Tazara
Jana Machi 20, 2024, ilishuhudiwa kampuni binafsi ya Bravo ikiingia makubaliano na Tazara yanayohusisha kuingiza treni mbili za mizigo zenye mabehewa 20 kila moja ambapo kila behewa litakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa tani 50 (sawa na malori mawili)
Makubaliano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa azimio la mageuzi ya kiuchumi kwenye sekta ya usafirishaji kupitia reli ikiwa Tanzania ni miongoni mwa mataifa yenye uhitaji mkubwa wa usafirishaji wa bidhaa zinazoingia nchini kupitia bandari.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Bravo Group of Companies, Angelina Ngalula alisema kampuni yake itakuwa ikisafirisha bidhaa za madini safari nne kwa mwezi ambayo ni sawa na tani 8,000 kwa mwezi.
Angelina alibainisha uwekezaji huo katika reli unalenga kupanua na kujenga ukuaji wa uchumi na fursa za kibiashara ndani ya kanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) yenye nchi 16.Nchi hizo ni, Angola, Botswana, Comoros, DR Congo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Zimbambwe, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
Alisema baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo hatua inayosubiriwa ni ukaguzi na usajili kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ardhi na Usafirishaji (Latra) Baada ya taratibu kukamilika huduma hiyo itaanza kutolewa.
“Tulishinda zabuni hii mwaka 2021 na lengo lilikuwa ni kuleta magari mengi, lakini tulishindwa kuanza operesheni kutokana na miundombinu mibovu ya reli hii, kwa hiyo tuliwaambia tusubiri mpaka wafanye marekebisho katika baadhi ya maeneo, sisi tuko tayari kuongeza uwekezaji kadiri miundombinu itakavyofanyiwa maboresho.
“Kwa sasa tutaanza na treni 2 ambazo zitakua zinapishana, treni moja itakuwa na behewa 20 na kila behewa litabeba tani 50 ambapo jumla tani 1,000 sawa na malori 40 zitabebwa kwa pamoja, na kwa ujumla treni hizi mbili ni sawa na malori makubwa 80,” alisema Angelina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF)
Aliwatoa hofu wamiliki wa malori na bandari kuwa uwekezaji huo hautaua biashara yao badala yake inalenga zaidi kuimarisha sekta ya usafirishaji na kusisitiza kuwa malori bado yataendelea kuhitajika.
Alisema kusafirisha mizigo kwa njia ya reli kunapunguza gharama kwa asilimia 70, pia kunasaidia kupunguza msongamano wa makontena bandarini.
“Tumeamua kuingia kwenye reli wateja wetu wanadai suluhisho endelevu la usafiri, tunafanya kazi na kampuni kubwa katika sekta ya madini ambazo zinatekeleza mpango wa kupunguza uchafuzi wa mazingira…,’’ alisema
unaosababishwa na hewa ukaa na sisi tunataka kuwa sehemu ya mkakati huu,
“Tunaendelea kuishukuru serikali kwa kuona kwamba sekta binafsi inaweza kufanya biashara Tazara na kuruhusu uwekezaji huu, hivyo tutumie miundombinu hii kuinua uchumi wa Tanzania na kuvutia mizigo mingi kupita katika bandari yetu.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tazara, Bruno Ching’andu alisema mchakato wa kuanzisha mradi huo ulizingatia taratibu zote muhimu na anaona unalenga jema la kukuza biashara inayofanyika katika reli hiyo.
“Niipongeze kampuni hii ya ndani kwa kuona fursa ya kuwekeza kwenye reli, kwa upande wetu hatuoni kama ni ushindani bali inakuja kuchangamsha biashara na ushirikiano unaoendelea ili kuongeza mvuto wa reli kwa wawekezaji wenye uwezo.
Walichokisema Tatoa, TPSF
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Rahim Dossa, alipongeza hatua ya kampuni hiyo kutumia usafiri wa reli akieleza itaongeza kiwango cha mzigo unaopitia bandari ya Dar es Salaam hatua itakayokuwa na matokeo chanya kwenye uchumi.
Akizungumzia makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Kampuni ya PMN Group Limited, Dk Judith Spendi, alisema kwa sasa Tanzania inakabiliwa na changamoto ya dola na uwezekano wa makubaliano hayo kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo kwa kuwezesha usafirishaji wa bidhaa na hivyo kuleta mapato yanayohitajika kwa kiasi kikubwa.
“Kama mtu anayehusika sana katika biashara ya usafirishaji, ninaelewa jukumu muhimu la bandari, reli, na malori katika kuwezesha biashara. Kuhamisha usafirishaji wa mizigo kwa reli inaweza kuwa kupunguza tatizo la uhaba wa dola kwa asilimia 60 na tunazidi kuwavutia wawekezaji,” alisema
Naye Mjumbe wa bodi ya TPSF, Octavian Mshiu alipongeza kampuni ya Bravo kwa uwekezaji huo na kuwataka wafanyabiashara wengine kufanya uwekezaji wenye tija na manufaa kama huo.
“Ni hatua kubwa na tuna kila sababu ya kujivunia uwekezaji huu mkubwa, hivi ndivyo tunatakiwa kufanya Serikali imeonesha imani kubwa kwa Sekta Binafsi inashirikiana na sisi hivyo tunapaswa kuilipa kwa kufanya uwekezaji na kuvuta zaidi wawekezaji,” alisema Mshiu.