Kitaifa
Polisi: Tutaowakamata kesho wenye namba 3D, kuwafikisha mahakamani
Dar es Salaam. Baada ya Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuanza operesheni kwa watu walioweka namba zilizoongezwa ukubwa ‘3D’ kwa kuwatoza faini, hatua itakayofuata kuanzia kesho Jumamosi, Machi 16, 2024 ni kuwakamata, kuwaweka mahabusu na kuwafikisha mahakamani.
Operesheni hiyo imeanza leo Ijumaa, Machi 15, 2024 nchi nzima baada ya siku 14 zilizotolewa na Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Nga’nzi kwa wale wote wanaoweka namba za 3D kuhakikisha wanazitoa kuzitoa kwa hiari.
Jeshi hilo lilipiga marufuku matumizi ya namba 3D wakieleza sababu mbalimbali ikiwewo kutokuwa namba rasmi katika nchi ya Tanzania, badala yake likaelekeza wamiliki wa magari kutumia namba za 2D zilizoidhinishwa na msajili wa magari kupitia mawakala.
Sababu nyingine ni kwamba namba hizo haziko kwenye mfumo wa Tanzania, kwa kuwa hazina ubora unaotakiwa, zinatengenezwa na watu wasioidhinishwa kuwa mawakala wa namna za magari.
Leo Ijumaa, Machi 15, 2024 askari wa usalama barabarani wameanza operssheni za kubandua namba hizo pamoja na kuwaandikia faini wale wote waliokuwa wakikamatwa. Wapo walioomba muda zaidi uongezwe hata mwezi mmoja.
“Nilikuwa nimesafiri nimerudi jana (juzi) na leo ndio natoka lakini hata ukiwaekeza askari, hawalewi,” amesema mmoja wa dereva ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Fadhil Mohamed, dereva wa teksi mtandao amesema yeye amepewa gari na tajiri yake ikiwa na namba hizo, lakini faini anaandikiwa yeye si sahihi.
Amesema bado kuliwa na nafasi ya kuwaongezea muda angalau miezi miwili au mitatu, hakikupaswa kuwa jambo la haraka hivyo ni kuwaumiza wananchi.
“Huku ni kuumizana unapewa gari yenye namba hizo halafu unakamatwa na kuandikiwa hii sio sawa, tulipaswa kuongezewa muda hata wa mwezi mmoja au miwili,” amesema Mohamed.
Hata hivyo, Kamanda Nga’nzi akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa amesema operesheni hiyo ndio imeanza kwa kuwaandikia faini na kubandua ujazo kwenye namba kuanzia leo kitakachofuata ni kuwakamata na kuwaweka ndani na Jumatatu kufikishwa mahakamani.
Amesema malalamiko ya baadhi ya madereva hayana msingi, kwa kuwa walipewa muda kwa mara ya kwanza na kuongezewa muda mwingine, lakini kinachofanyika ni kukaidi.
“Operesheni inaendelea na kuanzia kesho atakayekamatwa atapelekwa mahabusu na Jumatatu kupelekwa mahakamani, kutengeneza namba hakuchukui muda kinachoonekana ni ukaidi,” amesema Kamanda Nga’nzi.
Kuhusu idadi ya magari yaliyokamatwa leo, Kamanda Ng’anzi amesema ni mapema kutoa taarifa kwa kuwa operesheni ndio imeanza, lakini kutakuwa na utaratibu wa kutoa taariafa.
“Operesheni hii inaendeshwa kwenye kila mkoa na inasimamiwa na RTO (makamanda wa mikoa) na ndio wenye taarifa za maeneo yao tutaweka utaratibu wakutoa taarifa,”amesema.
Mwananchi limetembelea barabara kadhaa na kukuta askari wa kikosi cha usalama barabarani wakiwa wamejipanga huku wakikagua magari hayo yaliyokiuka amri ya kubadilisha namba hizo.
Pamoja na baadhi ya madereva kujitetea muda waliopewa kuwa mchache, lakini askari walionekana wakiwaandikia faini, huku wengine wakibandua ujazo ulioongezewa.
Kwa mujibu wa askari waliokuwa wakitekeleza opereshemi hiyo kwa masharti ya kutojitambulisha kwa kwa kuwa sio wasemaji walieleza kuwa walianza saa 11 alfajiri baada ya kupokea maelekezo.
“Operesheni hii itakuwa endelevu kutokana na maelekezo tuliyopewa na tukishabandua namba hivi kesho tukimkamata ni kosa lingine la kuendesha gari bila kuwa na namba,”amesema askari huyo kwa sharti la kutojitambulisha.
Hivi Karibuni, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini alisema namba za 3D hazitengenezwi na wakala aliyepata kibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), huku akibainisha ukubwa herufi hizo unaleta ugumu wa kusomeka katika umbali usiopungua mita 100.