Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa, Tanzania inakabiliwa na changamoto mbili za ukuaji wa uchumi ikiwamo kushindwa kutafsiri namna ya kupunguza umaskini na tatizo la ongezeko la watu linalotokana na kuzaliana.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Benki ya Dunia (WB).
Taarifa hiyo inasema wakati hali ya Pato la Taifa (GDP) ikitarajiwa kukua kwa asilimia 5.6 mwaka 2024 na fursa endelevu kwa karibu asilimia 6, Watanzania wengi bado wanakabiliwa na umaskini.
Benki hiyo imebainisha hayo jijini Dar es Salaam jana katika uzinduzi wa toleo la 20 la Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Tanzania.
Takwimu za benki hiyo ya dunia zinaonyesha karibu Watanzania milioni tatu wameingia kwenye umaskini wakati na baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19.
Inasema mwaka 2018, takriban Watanzania milioni 14 walikuwa wakiishi katika umaskini, lakini kufikia mwaka 2022, idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia milioni 17.
Pia, watu zaidi ya 300,000 walishuka chini ya mstari wa umaskini ilipofika Desemba 2023 hali iliyofanya ifikishe jumla ya watu milioni 17.3.
Hata hivyo, wakati WB ikisema hayo, pia inakadiria idadi ya Watanzania itaongezeka zaidi kila baada ya miaka 23 huku kukiwa na uwezekano wa kufikia karibu watu milioni 140 ifikapo mwaka 2050.
Mkurugenzi Mkazi wa WB, Nathan Belete alisema ongezeko hilo litaongeza mahitaji ya elimu na huduma za afya zaidi ya uwezo wa uchumi.
Alisema hali hiyo inaweza kusababisha changamoto katika kubuni nafasi za kazi.
“Kwa mfano katika sekta ya elimu, makadirio yanaonyesha ifikapo mwaka 2061, gharama ya elimu kwa umma zitapanda kutoka asilimia 3.3 ya Pato la Taifa hadi asilimia 4.1 chini ya hali ya juu ya uzazi, lakini inaweza kushuka hadi asilimia 2.9 katika mazingira ya chini ya uzazi,” alisema Belete.
Belete alipendekeza njia ambayo Tanzania inaweza kupata manufaa kutokana na idadi ya watu ni kukuza uchumi.
Alisema kukua huko kunaweza kutokea wakati nchi inapitia maboresho ya haraka ya matokeo ya afya yanayoambatana na kupungua kwa watu kuzaliana.
Belete alisema maboresho mengine ni kuimarisha juhudi za kupanua upatikanaji na ukamilishaji wa elimu ya sekondari kwa wasichana na kuongeza huduma za uzazi wa mpango.
“Serikali inahitaji kuendelea kuboresha afua za maisha ya watoto pamoja na kupunguza viwango vya udumavu ili kuwapa wazazi imani ya kuzaa watoto wachache,” alisema.
Belete pia, alishauri kuendelea kuwalinda wasichana waliobalehe wasibebe ujauzito hovyo na kukuza uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake na wasichana.
Akizungumza katika mkutano huo, Kiongozi wa Maendeleo ya Binadamu wa WB, Aneesa Arur alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi nane zinazotarajiwa kuchangia nusu ya ongezeko la watu duniani.
“Ili Tanzania ifaidike na mgao wa kidemografia ambao ni ukuaji wa uchumi unaotokana na hali tatu za awali, inapaswa kutupia jicho kushuka kwa kasi ya vifo na kufuatiwa na kupungua kwa kasi ya uzazi,” alisema Arur.
“Sharti la pili ni uwekezaji katika mtaji wa binadamu ili kuunda nguvu kazi yenye afya, elimu ya juu, ujuzi na mwisho ni kuundwa kwa kazi nzuri na fursa za kiuchumi kwa nguvu kazi hii yenye ujuzi.”
Awali, akifungua mkutano huo, Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imeweka kipaumbele kwa sera zinazolenga vijana na vijijini.
Alisema uwekezaji wa watu ndiyo msingi wa ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Elimu bado ni muhimu ili kwenda mbele zaidi, kwa sababu inahusiana na kiwango cha chini cha uzazi. Hii inakwenda sambamba na elimu ya uzazi wa mpango na afya ya uzazi,” alisema Profesa Kitila.
Alisema Serikali pia inazingatia utolewaji wa elimu juu ya mabadiliko ya uchumi vijijini kwa kuwa, ndiyo kipaumbele cha kwanza katika kupitia marekebisho mapya ya sera na mitalaa ya elimu.
“Hii ni pamoja na mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT), mpango wa vijana kwa ajili ya kilimo na biashara ya kilimo,” alisema Profesa Kitila.
Kwa mujibu wa WB inayoungwa mkono na tathmini ya uchumi mkubwa unaotia matumaini ya kuongeza bajeti katika sekta ya kilimo, inayoajiri robo tatu ya watu wanaokabiliwa na umaskini, inatarajiwa kutakuwa na nafuu ya kiwango cha umaskini katika muda wa kati.
“Licha ya mtazamo huu chanya, kuna hatari za nje na za ndani. Uwezekano wa mdororo wa kiuchumi duniani ndio hatari kuu ya nje, wakati utekelezaji wa sehemu ya mageuzi ya kimuundo, hasa yale yanayohusiana na kukuza sekta kibinafsi, ndio hatari kuu ya ndani,” alisema Belete.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hatari nyingine kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo na utalii.
“Ili kupunguza hatari hizi, watunga sera lazima waharakishe mageuzi ya kimuundo kama sehemu ya juhudi endelevu za kuvutia uwekezaji mkubwa wa kibinafsi na kuchochea ukuaji thabiti unaojumuisha sekta binafsi,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kwa muda mrefu, moja ya changamoto kuu za Tanzania ni kushindwa kukamilisha mageuzi yake ya kiuchumi ya kimuundo, yanayohitaji kuweka mazingira mazuri ya biashara.
Inaeleza kuwa, kwa kufanya hivyo, itasaidia katika ukuaji wa sekta ya viwanda na huduma pamoja na itaongeza tija kwenye kilimo.