Connect with us

Kitaifa

Naibu Waziri awashukia watoto wa vigogo kuomba ajira kwa ‘memo’

Dar es Salaam. Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, amewanyooshea kidole wazazi kutokana na mmomonyoko wa maadili kwenye jamii, akisema wasaidizi wa ndani ndio wameachiwa jukumu la malezi.

Amesema hata hivyo,  shida kubwa ya maadili ipo kwa watoto wa viongozi ambao hata nafasi za ajira zinapotoka,  hawataki kushindana wengine, bali  wanaziomba nafasi hizo kwa barua ya maelekezo ‘memo’.

Katambi ameyazungumza hayo leo Jumatano Machi 6, 2024 kwenye hafla ya kuhitimisha mafunzo ya mwanamke kiongozi awamu ya tisa yaliyoratibiwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

Mafunzo hayo yamehusisha wahitimu 497, yakilenga kuwajengea uwezo wanawake kumudu nafasi za juu za uongozi.

Akimkaribisha mgeni rasmi ambaye ni  Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, Katambi amesema Taifa linakosa viongozi kutokana na mmomonyoko wa maadili akidokeza wazazi wanatingwa na mambo yao badala ya kujali makuzi na malezi ya familia.

“Usiwaachie wasaidizi wa ndani kuwa wazazi,wanawake mliopo hapa ujuzi na maarifa mliopewa, fedha tunazotafuta nyumba na magari  hazina maana. Takwimu nilizonazo watoto wengi wa viongozi wanaharibikiwa sana hata nafasi za ajira zikitoka hawataki kujituma wanakwenda kusema baba amenituma,” amesema.

Amesema watoto wamekuwa wakilawitiwa kutokana na ‘ubize’ wa wazazi kutokana na kuwaachia wasaidizi wa ndani kila kitu.

Akihitimisha mafunzo hayo, Dk Gwajima amesema ni muhimu kuwekeza kwa wanawake, kwani kwa kufanya hivyo, kutaongeza kasi ya maendeleo, kukuza ustawi wa jamii na kujenga familia bora kwa maslahi ya Taifa.

“Wanawake tushikamane, ninyi mliopo maeneo ya kazi, muwanyanyue na wengine, muwasaidie, msiwe visababishi vya misongo ya mawazo kwa wengine,” amesema.

Dk Gwajima amesema Serikali itaendelea kushirikiana na ATE kuhakikisha kunakuwa na  ushiriki rafiki  wa wanawake katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, ili kukuza uchumi wa nchi na wananchi wote.

Kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia,  ametoa wito kwa jamii kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo na kutumia vizuri mitandao ya kijamii ili kuwalinda wanawake na watoto, akisisitiza mitandao itumike kuleta tija kwa jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba amewataka wanawake waliopewa mafunzo ya uongozi kutumia maarifa waliyopewa kuleta mabadiliko na kuwabadilisha wengine.

Akidokeza suala la usawa kijinsia, amesema kampuni zote zilizosimamia usawa wa kijinsia zimepata faida.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi