Kitaifa
Serikali yaongeza kasi uwekezaji Bandari Dar
Dar es Salaam. Kujengwa kwa matenki 15 vya kuhifadhia na kushushia mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya ndege (Jet 1) katika Bandari ya Dar es Salaam, kunatajwa kuwa moja ya njia itakayosaidia kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa na mafuta.
Kujengwa kwa visima hivyo pia kunatajwa kupunguza siku ambazo meli husubiri kabla ya kushusha mzigo kutoka kati ya 11 hadi 12 kufikia siku kati ya tatu hadi nne.
Hayo yalielezwa leo Februari 26 2024 katika hafla ya utiaji saini mkataba kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na kampuni kutoka China zilizoshinda zabuni hiyo inayogharimu zaidi ya Sh678.6 bilioni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Mkandarasi aliyeshinda zabuni hiyo ni muunganiko wa kampuni mbili za China Railway Major Bridge Engineering Group na Wuhuan Engineering.
Mkataba huu ni muendelezo wa maboresho yanayofanywa katika bandari, ili kuongeza ufanisi wake ikiwa ni baada ya ile mitatu iliyosainiwa kati ya TPA na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World.
Hili limefanyika ikiwa ni siku saba baadaye tangu Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuziita kampuni kutoka Misri kuja kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji wa gati namba 13 hadi 15.
Akizungumza katika halfa hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa amesema mkandarasi huyo anatarajia kujenga matenki yenye mita za ujazo 420,000 pamoja na miundombinu ya upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za mafuta ndani ya miezi 24, jambo litakalofanya meli sasa kutumia siku tatu mpaka nne kushusha mzigo na hapo ndipo ahueni itaanza kuonekana.
“Kwa siku meli ilikuwa ikitozwa dola 25,000 za Marekani kutokana na kusubiri (zaidi ya Sh63.75 milioni) kwa wastani wa siku nane ni sawa na Sh510 milioni, hii ilikuwa ikienda kama mzigo kwa wananchi, kupungua kwa siku hizi itapunguza bei ya mafuta kwa mwananchi wa kawaida,” amesema Mbossa.
Amesema matenki hayo pia yatasaidia kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kwani mafuta yote yatapokelewa na kupimwa vizuri chini ya TPA kabla ya kusambazwa.
“Hii itaimarisha udhibiti wa mapato ya Serikali kwa kuzuia mianya ya ukwepaji kodi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na bidhaa za mafuta zinazoingia nchini,” amesema Mbossa.
Hilo kutaifanya kuihakikishia Serikali hifadhi ya mafuta ya kutosha na itaondoa changamoto ya sasa ambapo uwezo wa kuhifadhi mafuta nchini ni wa siku 15 kupitia matenki ya kampuni binafsi.
Kuhusu mfumuko wa bei, Mbossa amesema matenki hayo utaleta ahueni kwa wananchi kwa kudhibiti ongezeko la bei linalosababishwa na kupanda kwa mafuta.
“Mradi huu pia utachochea mashirika yanayoshughulika na mafuta kuanzisha kituo cha usambazaji mafuta (Hub) kwenda nchi za jirani kama Uganda, Rwanda, Burundi, Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo na kuifanya Tanzania kuwa kituo cha soko la biashara ya mafuta,” amesema Mbossa.
Kwa sasa, Dar es Salaam inapokea mafuta kupitia sehemu mbili, Bora ‘Single point Mooring’ (SPM) yenye uwezo wa kuchukua meli yenye tani 120,000 huku Kurasini Oil Jetty (KOJ) ikiwa na uwezo wa tani 40,000.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameitaka TPA kuhakikisha mkandarasi aliyepewa mradi huo anasimamiwa na kuumaliza ndani ya wakati, ili thamani ya fedha ipatikane kwa mujibu wa mkataba.
“Lakini huu sasa ni muda ambao bodi inatakiwa kuanza kujipanga kwa ajili ya kujenga gati kubwa ya kushushia mafuta katika eneo la Kigamboni,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Suleimani Kakoso aliitaka Serikali kuja na mkakati mwingine wa kuongeza gati zitakazosaidia kupokea meli za dharula hasa kipindi hiki ambacho bandari inapokea meli nyingi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Deus Sangu amesema fedha nyingi zimekuwa zikipotea kutokana na ucheleweshaji miradi huku akisema katika mwaka wa fedha uliopita mashirika ya umma pekee zaidi ya Sh400 bilioni zililipwa kama riba kwa wakandarasi kwa sababu ya ucheleweshaji wa miradi.