Kitaifa
Mramba: Muda wowote mgawo wa umeme utakoma
Dar es Salaam. Hatima ya kukoma kwa mgawo wa umeme nchini ipo ndani ya muda mchache ujao, baada ya matarajio ya kuingizwa kwa megawati 235 katika gridi ya Taifa.
Matumaini ya kukoma kwa mgawo huo, yanatokana na kile kilichoelezwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba kwamba muda wowote kuanzia sasa, mtambo kutoka Bwawa la Jilius Nyerere (JNHPP) utawashwa.
Hatua ya kuwashwa kwa mtambo huo inafuatia majaribio kadhaa uliyowahi kufanyiwa na kwamba utakapowashwa, utapunguza kwa zaidi ya asilimia 80 ya changamoto ya mgawo wa umeme.
Mgawo wa umeme ulianza Septemba mwaka jana, ukitokana na upungufu wa uwezo wa uzalishaji wa nishati hiyo kutoka kwenye vyanzo mbalimbali yakiwemo maji.
Tangu kuanza kwa mgawo huo, kumekuwa na ahadi lukuki za viongozi juu ya kukoma kwake, ikiwemo iliyowahi kutolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.
Kapinga aliahidi mgawo huo unatarajiwa kukoma Februari 17, 2024 na baadaye aliibuka na kueleza utakoma Machi, mwaka huu.
Wingi wa ahadi hizo ndiyo uliopoteza matumaini ya wananchi juu ya kukoma kwa mgawo huo, wakihofu pengine ahadi wanazopewa zitabaki kuwa hewa.
Hata hivyo, Septemba 25, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alimpa miezi sita bosi mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo-Hanga kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana nchini. Miezi hiyo sita inakwisha Machi 25 mwaka huu.
Matumaini ya kutamatika kwa mgawo huo yametolewa jijini Dar es Salaam leo Alhamisi, Februari 22, 2024 na Mramba alipozungumza katika mkutano wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu na wahariri wa vyombo vya habari, uliofanyika Ikulu.
Mramba amesema matarajio ya kukamilika kwa mgawo ni bwawa la JNHPP ambalo kwa sasa kuna mitambo miwili iliyopo katika hatua za mwisho za kukamilika kwake.
Kati ya mitambo hiyo, amesema wa kwanza umeshafanyiwa majaribio na kilichobaki ni kuingiza umeme wake kwenye gridi ya Taifa.
“Ninaposema muda wowote namaanisha muda wowote kwa sababu wataalamu wanaendelea na kazi kuhakikisha wanaingiza megawati 235 za umeme huo kwenye gridi ya Taifa,” amesema.
Kwa kuwa mahitaji ya nishati hiyo kwa sasa ni takriban megawati 300 hadi 400, kiwango hicho cha umeme kitakachoingizwa kitapunguza angalau asilimia 80 ya matatizo ya umeme yaliyopo.
“Kwa kuwasha tu ule mtambo, zaidi ya asilimia 80 ya matatizo yatakuwa yamekwisha. Taratibu za mtambo huu ziko mwishoni kabisa, unaweza ukajikuta umeamka asubuhi kesho ukashangaa mgawo haupo au keshokutwa, lakini niseme tu tupo katika hatua za mwisho,” amesema.
Kuhusu mtambo wa pili, alisema umeshafanyiwa majaribio ya awali na kinachotarajiwa kufanyika ni majaribio ya awamu ya pili wiki hii kisha itafuata awamu nyingine.
“Kwa kawaida majaribio ya namna hii yanachukua wiki mbili kwa hiyo tumekadiria kufikia katikati mwa Machi mtambo wa pili na wenyewe utakuwa umekamilika,” alisema.
Amesisitiza kilichoelezwa na Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ni sahihi kwamba mitambo hiyo itakayoingiza jumla ya megawati 470 ipo katika hatua za mwisho.
“Watu wana hofu na hawaamini, lakini niwaondolee hofu, JNHPP sasa hivi lina maji mengi na mwaka huu umekuwa wa maajabu kwa sababu katika wiki tatu zilizopita kiasi cha maji yanayoingia kwenye mabwawa yamevunja rekodi,” amesema.
Hata hivyo, mtendaji mkuu huyo wa wizara hiyo alisema matatizo ya umeme nchini yapo katika eneo la uzalishaji na usambazaji na si usafirishaji.
Kinachotokea kwenye uzalishaji, alisema ni kukosekana uwezo wa kuzalisha umeme unaoendana na mahitaji ya nchi na jambo hilo ndilo linalosababisha mgawo.
“Mahitaji ni makubwa, lakini kiwango kinachozalishwa ni kidogo huo ndiyo mgawo unavyotokea,” alisema.
Kwa upande wa usambazaji, alisema matatizo hutokea pale ambapo umeme unazalisha wa kutosha, lakini miundombinu inakuwa na tatizo na hivyo kusababisha wananchi wasiupate.
“Unakuta umeme unaozalishwa unatosha lakini transfoma ina hitolafu au nguzo imeanguka, haya ndiyo matatizo kwenye usambazaji, lakini haya hayasababishi mgawo ni kukatika kwa kawaida,” amesema Mramba.
Hata hivyo, alisisitiza kukatika huko kwa sababu ya hitilafu ya miundombinu ni jambo linalotarajiwa kuwepo hata baada ya kukoma kwa mgawo wa umeme.
“Kwa hali ya mifumo ya usambazaji ilivyo, hatutarajii kwa kweli hizo changamoto za kukatika kwa umeme hapa na pale zitakuwa zimeisha kabisa,” amesema.
Aliijenga hoja hiyo akitolea mfano wa matukio ya wizi wa mafuta ya transfoma katika Wilaya za Temeke, Mbagala na Kigamboni.
“Transfoma inavyoungua inakuwa imeunganishwa na wateja takriban 100 kwa hiyo inapoungua wateja hawa watakuwa gizani hadi transfoma mpya itakapoenda kuwekwa,” alisema.
Alieleza changamoto nyingine zitakazosababisha kukatika kwa huduma hiyo ni mvua inayosababisha nguzo kuloa maji na kusababisha shoti.
“Wakati wa mvua kwa sababu ya kuwepo kwa maji mengi na kwa sababu yanaweza kusababisha hitilafu, hizo ndizo changamoto zinazoweza kuwepo,” alisema.
Alieleza kukatika kwa kawaida kila mtu anaelewa na litakapotatuliwa suala la mgawo hayo mengine yatakomeshwa taratibu.