Kitaifa
Serikali yasaka mwarobaini uhaba wa pombe Zanzibar
Unguja. Serikali imekiri kuwapo uhaba wa pombe Zanzibar na kwamba changamoto hiyo inatafutiwa ufumbuzi.
Katibu wa umoja wa wafanyabiashara ya pombe eneo la Amani, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Frank John Kahamu amesema licha ya kuanza kuona jitihada zinazochukuliwa na Serikali, bado hali haijakaa sawa.
Amesema suala la vinywaji ni shida na vimekuwa adimu, hivyo kuathiri biashara.
Kwa mujibu wa katibu huyo, eneo hilo la Amani pekee kuna watu zaidi ya 3,000 wanaotegemea vinjwaji hiyo ama kwa kujiajiri au kuajiriwa.
Amesema hali haijakaa vizuri, kwani kuna baadhi ya vinywaji vinakosekana na vingine havitoshelezi mahitaji.
Frank amesema wameambiwa tatizo hilo linashughulikiwa na wamejaribu kuongeza wakala, ili kuongeza kasi ya kuingiza vinywaji hivyo kutosheleza soko.
“Hili nalo tunaona kama limesaidia kidogo na matokeo yake tunayaona japokuwa bado mahitaji yapo mengi, ili kurejea katika hali ya kawaida,” amesema katibu huyo.
Amesema bei za bia zipo juu, kwani kwa rejareja wanauza kati ya Sh3,000 mpaka Sh4,000 kutegemeana na aina ya pombe .
Kuhusu bei za jumla, amesema kreti ya bia zinazozalishwa nchini wananunua kati ya Sh55,000 na Sh65,000 kwa maeneo ya shamba (vijijini), wakati awali kreti ilikuwa inauzwa kati ya Sh42,000 na Sh43,000 kutegemea na aina ya pombe.
Frank amesema kwa upande wa pombe kali za maboksi zipo zilizopanda kutoka Sh90,000 hadi Sh100,000, huku zilizokuwa zinanunuliwa kati ya Sh100,000 na Sh105,000 zimepanda hadi Sh110,000.
“Huyu mama (wakala) tunaona kama ameshusha kidogo, kwa hiyo tunadhani kadri tunavyoendelea mambo yatabadilika zaidi na kuwa katika hali ya kawaida, kikubwa kuendelea kuongeza jitihada zaidi ili biashara ifanyike kwa amani,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Februari 18, 2024 bila kutaka kuingia undani wa suala hilo kwa madai ya tamaduni za Kizanzibari, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amesema Serikali inalitambua tatizo hilo, hivyo linashughulikiwa na Machi mwishoni litakuwa limepatiwa ufumbuzi.
“Sekta ya utalii ni nyeti, lakini kutokana na hulka, silka na tamaduzi za Kizanzibari kuna vitu ambavyo vikawepo, lakini havizungumzwi kwa umma na kuacha soko lenyewe lizungumze. Hata mimi ukiniuliza huwa sipendi kuviongelea kwa sababu ya kuheshimu zile mila na tamaduni zetu,” amesema Soraga.
Hata hivyo, amesema wanafahamu kuna changamoto na Serikali inazifanyia kazi.
“Tungependa waandishi wa habari kuheshimu ile process (mchakato) inafanyika na kuna priorities (vipaumbele) nyingi za wananchi zinazowagusa moja kwa moja ambazo zinaumiza kichwa sana kuliko haya.
“Tunapoanza kuzungumzia ishu ambazo kimsingi hata katika tamaduni zetu si jambo linalosemwa sana kidogo inakuwa shida, wananchi wangependa kujua zaidi kuhusu masuala ya sukari, mchele na vyakula ambavyo kimsingi vinawagusa moja kwa moja katika maisha yao,” amesema.
Soraga ambaye ana siku 18 tangu ateuliwe kushika wadhifa huo amesema: “Nikiwa msimamizi wa sekta jambo hili tunalifahamu, hatua mbalimbali zinachukuliwa kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo, tunaamini kufikia ndani ya miezi miwili, mitatu yaani kufikia mwisho wa Machi litakuwa limerejea kwenye hali ya kawaida.”
Kuhusu sekta ya utalii kuathirika, Soraga amesema bado hawajaona athari kwa sababu bado ni kipindi cha mpito, labda pengine baada ya miezi mitatu mbeleni ndipo wanaweza kubaini.
“Kwa ujumla bado ndege zinaendelea kuingia Zanzibar kwa wingi hakuna ratiba ya ndege ambayo imebadilika,” amesema.
Hivi karibuni Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) ilikutana na kampuni tatu— Bevco, Kifaru na Zan zilizopewa leseni kuingiza vileo Zanzibar kujadiliana kuhusu changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa ZRA, Yussup Juma Mwenda, baada ya kukutana na kampuni hizo, walikubaliana moja ya sababu za magendo ni kutokuwapo vinywaji vya kutosha kisiwani humo.
Amesema ZRA waliwaeleza moja ya maeneo ambayo wanakusanya kodi ya kutosha ni mnyororo wa utalii na eneo la vinywaji lina manufaa makubwa.
Kama alivyosema Soraga, pia Mwenda amesema hawajaona athari katika ukusanyaji wa mapato.
Baada ya kukutana na ZRA, kampuni hizo zilisema zina uwezo tofauti na inavyosemwa, hivyo baada ya muda mfupi hali itarejea kama kawaida.
Nocole Verjus, Mkurugenzi Mtendaji wa Bevco amesema wana uwezo wa kusambaza vinywaji kwa asilimia 100 na sasa wameanza kuagiza makontena, hivyo baada ya Februari hali itakaa sawa.
Francis William, kutoka kampuni ya Kifaru amesema wamejipanga kuhakikisha wanasambaza vinywaji maeneo yote, kwani wamepata leseni hivi karibuni na wana uwezo wa kutosha, hivyo watafuata utaratibu ili kusitokee mianya ya kuisababisha Serikali ikose mapato.
Ilivyokuwa
Tatizo la uhaba wa pombe kisiwani hapa liliibuka Januari 23 baada ya aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Muhammed Said kukutana na wadau wa sekta ya utalii kuzungumzia hali hiyo.
Katika mkutano huo uliofanyikakatika ukumbi wa wizara hiyo Welesi, Simai alisema sekta ya utalii imeanza kupata changamoto kwa sababu ya hoteli kukosa vileo, akiilalamikia bodi ya vileo kubadilisha mawakala waliokuwa wanaingiza vileo Zanzibar na kuwapa mawakala wengine bila hata kuishirikisha wizara.
“Tumeona maamuzi ya Bodi ya Vileo Zanzibar imewaondosha wale waliokuwa wanahusika kama ZMMI, Schoch na One Stop nimeanza kuona athari, hoteli nyingi zimeanza kukosa huduma baada ya bodi ya vileo kufanya uamuzi huo,” alisema.
Hata hivyo, baada ya siku mbili, Janauri 25, 2024 Simai alimuandikia barua Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kujiuzulu nafasi yake kwa kile alichoeleza mazingira ya kazi si rafiki.
Siku moja baada ya kujiuzulu, Januari 27, 2024 Dk Mwinyi alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na kumbadilisha Soraga kutoka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kuziba nafasi Simai.
Mwinyi na masilahi
Wakati akimuapisha Soraga na wenzake aliowateua Ikulu Zanzibar, Februari mosi, mwaka huu, Dk Mwinyi aligusia masuala ya kujiuzulu kwa Simai akisema ni vyema akasema ukweli kilichomfanya ajiuzulu.
Pia alitaja masuala ya masilahi binafsi kugubikwa katika sakata la kujiuzulu Simai ambaye amebaki na nafasi ya uwakilishi wa Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Sheria ya vileo Zanzibar
Zanzibar ina sheria kuhusu vileo inayoeleza si kila mahali inaruhiswa kuuza pombe na kuna wakati bodi ya wadhamini wa Jumuiya ya Maimam Zanzibar (Jumaza), ilifungua kesi mahakamani kuishtaki bodi ya vileo Zanzibar na Mwanansheria Mkuu wa Zanzibar kwa kukiuka sheria ya vileo.
Jumaza ilidai bodi ya vileo imekiuka sheria namba tisa ya mwaka 2020 kifungu cha 33 (1) kinachosema bodi inatakiwa kutoa vibali kwa kuingiza pombe Zanzibar kwa kampuni zisizozidi tatu, lakini tayari ilikuwa imetoa vibali kampuni nane.
Hata hivyo, baadaye bodi hiyo ilivunjwa na kuundwa bodi nyingine iliyopo hadi sasa.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, Bodi hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kutoa leseni kwa kampuni za uingizaji vileo kisiwani Zanzibar, kwa hoteli, baa, maduka maghala na vibali vya kusambaza vileo katika matukio muhimu.
Kwa mujibu wa kifungu cha 33 (1), kampuni zinazotakiwa kupewa vibali vya kuingiza pombe ni tatu na anayepewa kibali lazima awe Mzanzibari, mlipakodi, awe na ghala na gari la kusambazia bidhaa hiyo.