Kitaifa
Mahakama yaamuru nyumba ya mtoto wa Mbowe ipigwe mnada
Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi imeamuru kukamatwa na kupigwa mnada nyumba ya mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe iliyoko Mikocheni, ili kulipa deni la Sh62.7 milioni anazodaiwa na waliokuwa waandishi na wahariri wa gazeti hilo.
Sambamba na amri hiyo iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mary Mrio, pia imemteua dalali wa kutekeleza amri hiyo, Jesca Massawe kutoka kampuni ya udalali ya MM Auctioneer & Debt Collectors.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo kufuatia maombi yaliyowasilishwa na waandishi hao, Maregesi Paul na wenzake tisa ili kutekeleza tuzo yao waliyopewa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), katika shauri la mgogoro wa kikazi walilolifungua dhidi ya mwajiri wao huyo.
Akizungumza na Mwananchi, Paul amesema wakati amri hiyo inatolewa, Dudley ambaye ni mtoto wa Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema, hakuwepo mahakamani licha ya kwamba alikuwa ameahidi kuwa angefika na fedha za kuwalipa.
Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia amri hiyo, Dudley hakupatikana kwa simu yake ya mkononi ambayo haikuwa hewa, na dalali huyo namba yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.
Hata hivyo, Naibu Msajili huyo, amelithibitishia Mwananchi kuhusu kuwepo kwa amri hiyo akisema ni kweli imetolewa na Mahakama dhidi ya mdaiwa huyo.
“Ni taarifa za kweli kwamba walikuja (washinda tuzo/wanahabari hao) kuomba ikamatwe (nyumba hiyo) baada ya yeye (mshindwa tuzo/Dudley) kushindwa kuwalipa na tukatoa hiyo amri,” amesema Naibu Msajili Mrio.
Awali, wanahabari hao, Paul na wenzake hao tisa walifungua shauri hilo la mgogoro wa kikazi namba 28461 la mwaka 2023, CMA Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, baada mwajiri wao huyo kuvunja mikataba yao ya ajira.
Katika shauri hilo, wadai walikuwa wakiomba kulipwa malimbikizo ya mishahara yao jumla ya Sh114 milioni.
Hata hivyo, CMA katika uamuzi wake uliotolewa na Mwenyekiti wa CMA, Bonasia Mollel Julai 17 mwaka 2023, iliamuru wadai walipwe Sh62.7 milioni baada ya pande zote kukaa pamoja na kujadiliana na kufikia makubaliano.
Paul amelieleza Mwananchi kuwa kufuatia makubaliano hayo Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30, 2023 na awamu ya mwisho Februari mwaka.
Hata hivyo, amesema mwajiri huyo hakutekeleza ahadi hiyo ndipo wakawasilisha mahakamani maombi ya utekelezaji wa tuzo hiyo.
Paul amesema shauri lilikuwa limepangwa Februari 9, 2024 lakini mjibu maombi, alipigia simu akieleza yuko Moshi kwenye msiba na kwamba niombe shauri liahirishwe kwa wiki moja na kwamba angefika na fedha za kuwalipa.
“Jana tulipomtafuta (mahakamani) asubuhi hakupatikana na mpaka leo hapatikani, tukamwambia Mheshimiwa huyu mdaiwa hapatikani, tukaubaliana tupange leo na leo pia tumemtafuta hapatikani. Kwa hiyo, tukaomba sisi tuendelee.”
Amesema wameieleza Mahakama kwamba kwa kuwa mdaiwa wao amekaidi kuwalipa wameona njia sahihi wakamate nyumba yake namba 9 iliyopo Mtaa wa Feza, Mikocheni B, barabara ya Chipaka.
Paul amesema kuwa Mahakama baada ya kusikiliza hoja zao imekubaliana nao na kutoa amri ya kukamata nyumba hiyo na kumteua dalali huyo kutekeleza amri hiyo.
Baada ya uamuzi huo, Mahakama iliahirisha shauri hilo mpaka Machi 4, 2024 kwa ajili ya kupata taarifa ya utekelezaji wa amri hiyo.