Connect with us

Kitaifa

Samia atetea miswada ya uchaguzi, aahidi kuisaini

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema miswada ya sheria za uchaguzi iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge itawezesha kuwepo kwa mazingira ya uchaguzi ulio huru na uchaguzi.

Miswada hiyo ambayo sasa inasubiri kusainiwa na Rais Samia ili iwe sheria ni pamoja na ule wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, wa Sheria Tume Huru ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Akizungumza leo Februari 7, 2024 katika sherehe za mwaka mpya kwa mabalozi zilizofanyika Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Samia amesema Serikali itahakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu unaakuwa huru na wa haki.

“Kikosi kazi kilileta mapendekezo yake mwaka uliopita na mapendekezo yake yalijikita katika kuongeza uwazi katika mfumo wa uchaguzi ukiwemo uteuzi wa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi,” amesema.

Amesema Serikali ilikubaliana na mapendekezo hayo likiwemo la kuibadilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Mapendekezo pia yalitaa kubadilishwa jina la tume ya uchaguzi ili liendane na maboresho hayo na sasa tuna jina jipya la Tume Huru ya Uchaguzi.

Hata hivyo, amesema baadhi ya mambo yaliyopingana na Katiba yatachukuliwa wakati wa mapitio ya Katiba wakati utakapofika.

“Ili kuyapa mapendekezo hayo nguvu ya kisheria, tulitengeneza miswada mitatu na hivi karibuni, Bunge lilijadili miswada hiyo na Februari 2, 2024 ilipitishwa na nitaisaini miswada hiyo kuwa sheria wakati ukifika.

“Kwa mabadiliko haya yatahakikisha uchaguzi unakuwa katika mazingira ya uhuru na haki katika mfumo wa kitaasisi unaokubalika na tutahakikisha amani na usalama vitakuwepo wakati wote,” amesema.

Amesema watakubali fursa za majadiliano yenye kujenga ya Serikali ya nchi wanazowakilisha mabalozi hao kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano, tunu za Taifa, utawala wa nchi, usawa na umoja wa Taifa.

Mbali na suala hilo, Rais Samia amesema mwaka 2024 utakuwa na maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na pia utakuwa ni miaka 60 kwa ushirikiano na wa kidiplomasia na nchi nyingi.

Kuhusu uchumi, amesema Tanzania kama nchi nyingine imechukua hatua kukabiliana na changamoto za uchumi, yakiwamo mabadiliko ya tabia nchi na maambukizi ya magonjwa.

“Kwa mwaka 2024 Tanzania itaweka kipaumbele cha uzalishaji wa umeme kwa kushirikiana na nchi nyingine. Tumefanya na Uganda mwaka uliopita katika mradi wa Kikagati-Murongo na mwaka huu tutamaliza mradi wa Rusumo unaohusisha nchi za Rwanda, Burundi na Tanzania,” amesema.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema tangu Rais Samia alipoingia madarakani amepokea marais mbalimbali waliofanya ziara za kikazi nchini, huku yeye akifanya nyingine zilizowezesha kuingia makubaliano 78 ya ushirikiano wa kimataifa.

“Napenda kueleza kuwa idadi ya makubaliano (MoU) yamekuwa yakifikiwa kwa wastani wa 14 kwa mwaka tangu tulipopata uhuru.

“Kwa mwaka huu hadi Februari hii makubaliano yamefikia 16, hii inaonyesha mwelekeo mpya katika uhusiano wa kimataifa,” amesema.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi