Kimataifa
Mambo muhimu ziara ya Samia Vatican kuonana na Papa Francis
Jumapili, Februari 11, 2024, saa 3:30 asubuhi kwa saa za Vatican, saa 5:30 asubuhi Tanzania, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis I, atahudhuria misa takatifu, Kanisa la Mtakatifu Peter (St Peter’s Basilica). Kisha, siku hiyohiyo, atampokea Rais Samia Suluhu Hassan.
Papa Francis amemwalika Rais Samia, ambaye amepokea mwaliko. Itakuwa ziara ya siku mbili, yaani Februari 11 na 12. Siku inayofuata (Febrauri 13), Rais huyo wa kwanza mwanamke kwa nchi za Afrika Mashariki, atawasili Norway kwa ziara nyingine ya siku mbili.
Haijawekwa wazi ni mazungumzo gani yanakwenda kuchukua nafasi ndani ya Jumba la Mitume la Sixtus V (Apostolic Palace), ambalo ndiyo makazi rasmi ya Papa. Rais Samia anatarajiwa kukirimiwa na Papa kwenye kasri lake na kufanya mazungumzo mahsusi.
Siku hiyo, Februari 11, 2024, yatakuwa maadhimisho ya miaka 95 ya uhuru wa Dola ya Vatican. Februari 11, 1929, aliyekuwa Mfalme wa Italia, Victor Emmanuel III na Papa Pius XI, walisaini Mkataba wa Lateran, ulioitambua Vatican kuwa ni Kiti Kitakatifu (The Holy See). Mkataba huo ulihalalisha Vatican kuwa nchi huru na inayojitegemea, ndani ya Jiji la Roma. Mkuu wa Dola ya Vatican ni Papa.
Mapinduzi ya Papa, Februari 9, 1849, kufutwa kwa Dola za Papa (Papal States), kisha wanasiasa watatu, Carlo Armellini, Giuseppe Mazzini na Aurelio Saffi, wakaanzisha Jamhuri ya Roma, ambayo iliongozwa kwa ushirikiano wa utatu (The Triumvirate). Utatu huo ulibeba sera ya uhuru wa kuabudu na kufuta adhabu ya kifo. Ikiwa ni dola ya kwanza kufuta adhabu hiyo.
Kilichofuata, Serikali ya Ufaransa ilisambaratisha Jamhuri ya Roma, kisha kuirejesha The Holy See, Julai 3, 1849. Pamoja na hivyo, utata uliendelea kuikumba Roma, kuhusu uhalali na mamlaka ya Papa. Februari 11, 1929, utata ulimalizika kwa Vatican kutambulika kama Kiti Kitakatifu, ikawa dola huru rasmi.
Muhtasari huo unaonesha kuwa Rais Samia, anazuru Vatican katika siku muhimu kihistoria kwa Kanisa Katoliki. Vatican imo kwenye orodha ya dola ndogo (microstates). Ina watu 764 tu, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka jana (2023). Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, ni kiongozi wa juu wa mwisho Tanzania kuzuru Vatican, alipoalikwa na Papa Benedict XVI mwaka 2007.
Ziara inahusu nini?
Maswali yanaanzia hapa. Je, ziara inahusu hali ya amani Afrika Mashariki? Januari na Februari 2023, Papa Francis, alifanya ziara kwenye nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Sudan Kusini, ambazo zina machafuko makubwa na ambayo yamedumu kwa muda mrefu.
Tukio lililobeba hisia za watu duniani ni lile la Papa akiwa Sudan Kusini, alipopiga magoti na kubusu miguu ya Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir na Makamu wa Rais, Riek Machar, ikiwa ni ishara ya kuwaangukia ili waache vita na wajenge taifa moja.
Umepita mwaka mmoja tangu Papa afanye ziara DRC na Sudani Kusini. DRC hali imeendelea kuwa mbaya, wakati Sudani Kusini bado ni shaka tupu. Je, Papa amemwita Rais Samia kujadili amani ya Afrika Mashariki? DRC na Sudani Kusini ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo Tanzania ni mwasisi wake. Mwaka 2023, Somalia, taifa lingine lenye machafuko ya kisiasa na ghasia za kigaidi, lilikubaliwa uanachama wa EAC.
Katika miezi ya karibuni, Papa Francis amekuwa akitoa matamshi tata kuhusu uhusiano wa kimapenzi wa jinsia moja, vilevile ndoa za jinsia moja. Awali, aliuambia ulimwengu kwamba mapenzi ya jinsi moja siyo uhalifu, ila ni dhambi kwa Mungu. Kauli hiyo ilitafsiriwa kuwa Papa alitaka dunia iachane na sheria zenye kutafsiri mapenzi ya jinsia moja kama uhalifu, badala yake lishughulikiwe kiroho.
Desemba 18, 2023, Papa Francis, alitoa ruhusa kwa mapadri kuwabariki wapenzi wa jinsi moja kuwa wanandoa kamili. Ruhusa hiyo ilitoka kupitia azimio la Papa, aliloliita “Fiducia Supplicans”, lililofafanua kuwa hayo ni maendeleo halisi, lakini halibatilishi mafundisho na msimamo wa Kanisa Katoliki, kuhusu ndoa.
Mkazo ni kuwa Kanisa Katoliki linasimamia ndoa yenye kukutanisha mwanamume na mwanamke. Wanaume wawili (wapenzi) au wanawake wawili (wapenzi), ni mwiko kwa Kanisa kuwafungisha ndoa. Hata hivyo, Papa ameruhusu wapenzi wa jinsi moja ambao tayari wanaishi pamoja, wanapokwenda kanisani kuomba kubarikiwa, basi wabarikiwe.
Mwongozo huo wa Papa Francis, umepingwa kila kona Afrika. Askofu wa Jimbo Katoliki, Geita, Flavian Kassala, katika misa ya Krismasi, Desemba 25, 2023, alisema “bora abariki jiwe” mtu akajengee nyumba, kuliko kubariki mambo ambayo yapo kinyume na maadili.
Januari 29, 2024, gazeti la Italia “La Stampa”, lilichapisha mahojiano ambayo lilifanya na Papa Francis. Kupitia mazungumzo hayo, Papa alisema, anaelewa msimamo wa maaskofu kutoka Afrika kuhusu ndoa za jinsi moja kuwa ni jambo baya. Akasema Afrika kwenye suala la mapenzi ya jinsi moja ni kesi maalumu.
Hata hivyo, Papa alitetea ruhusa yake kwa mapadri kubariki wapenzi wa jinsi moja, akisema azimio la Fiducia Supplicans, shabaha yake ni “kujumuisha” badala ya
“kutawanya”. Alieleza kuwa anaamini utafika wakati kila mtu ndani ya Kanisa Katoliki, ataunga mkono sera hiyo mpya ya Vatican.
Rais Samia anapokwenda Vatican kufanya mazungumzo na Papa, suala la mapenzi ya jinsi moja linakwenda kuwa agenda? Je, Papa anajaribu kushawishi sera mpya ya Vatican iingie Tanzania? Inafahamika kuwa Tanzania, kitamaduni na kisheria, mapenzi ya jinsi moja ni uhalifu mkubwa na adhabu yake ni ka
li.
Maswali zaidi
Novemba 2023, viongozi wa dunia walikutana Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), katika Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (Cop-28). Papa alikuwa mmoja wa waliohudhuria kongamano hilo. Akiwa Dubai, Papa alifanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi ambao walikuwa kwenye ratiba yake.
Haikuwezekana kuzungumza na kila kiongozi. Taarifa ya Vatican ilieleza kuwa Papa angeendelea na mazungumzo na viongozi wa ulimwengu kuhusu mazingira hata baada ya kumalizika Cop-28. Je, ziara ya Rais Samia ni kiporo cha Cop-28, kwa hiyo agenda inayokwenda kuwakutanisha ni mazingira?
Lipo suala la uendeshaji na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam. Tanzania imesaini na Dubai, Mkataba wa Ushirikiano wa Kiserikali (Iga), ambao umeruhusu Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kufanya majadiliano, kukubaliana, kisha kusaini mikataba ya utekelezaji na kampuni ya DP World, inayomilikiwa na Dubai.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), lilipinga mkataba wa Iga kuwa haukuwa na masilahi kwa Watanzania. Hata hivyo, Serikali ilisonga mbele na Iga.
Tayari TPA na DP World wameshasaini mikataba ya utekelezaji. Hali hiyo imekuwa ikitengeneza minong’ono kwamba Kanisa Katoliki haliivi na Serikali.
Je, mwaliko wa Rais Samia Vatican unahusu mazungumzo ya uhusiano wa Kanisa Katoliki na Serikali ya Tanzania? Kihistoria, uhusiano wa Kanisa Katoliki na Tanzania ni wa karne nyingi. Mwishoni mwa Karne ya 15 (mwaka 1499), Wamisionari wa Agostini, waliwasili Tanzania wakiambatana na mpelelezi wa Ureno, Vasco da Gama.
Baada ya Vita ya Napoleon, mwishoni mwa Karne ya 18 na mwanzoni mwa Karne ya 19, ilizaliwa jumuiya ya Watawa wa Mary Immaculate, Marseilles, Ufaransa mwaka 1816, ambayo ilifika mpaka Tanzania kufanya uinjilishaji. Karne hiyohiyo ya 19, Mababa wa Roho Mtakatifu (The Holy Ghost Fathers), waliwasili Tanzania kupitia Zanzibar mwaka 1963, kwa misheni maalumu ya Papa Gregory XVI. Kisha, Shirika la Mababa Weupe (White Fathers), liliingia Tanganyika mwaka 1878.
Kanisa Katoliki liliendelea kujitawanya, kisha Wajerumani wakajenga Kanisa la Mtakatifu Peter, Dar es Salaam, lililoanza kutoa huduma mwaka 1905. Tanzania imo ndani ya nchi 15 za kwanza kabisa Afrika ambazo Vatican ilianzisha uhusiano nazo wa kidiplomasia. Kwa mara ya kwanza, Vatican ilituma mwakilishi wa Papa (Vatican Diplomatic Corp) Tanzania mwaka 1968. Kutoka wakati huo hadi sasa (Februari 2024), Tanzania imeshakuwa na wawakilishi 10 kutoka Vatican.
Kardinali wa kwanza Mwafrika, Laurean Rugambwa, alitoka Tanzania. Muhimu pia, Kanisa Katoliki limejenga na kuendesha shule 240 za chekechea, 147 za msingi, 245 za sekondari, vyuo vya ufundi 110, vyuo vikuu vitano, vilevile hospitali, vituo vya afya na zahanati, jumla yake ni 473. Mchanganuo huo unathibitisha kuwa Kanisa Katoliki ni mdau muhimu wa maendeleo Tanzania, pia ni sehemu ya historia ya nchi.