Kitaifa
Siri shule kongwe za Serikali kupata ufaulu wa juu
Dar es Salaam. Wanafunzi wawili kati ya watatu katika shule 12 kongwe za Serikali amefaulu kwa kupata daraja la kwanza, uchambuzi wa Mwananchi umebaini.
Haya yanatokea, wakati ufaulu ukiongezeka kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka 2023 yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) jana, huku shule hizo zikiwa miongoni mwa zilizofanya vizuri, asilimia 68 ya wanafunzi wakipata daraja la kwanza, asilimia 20 wakipata daraja la pili.
Kwa mujibu wa matokeo hayo hakuna mwanafunzi aliyepata daraja sifuri kwenye shule hizo na ni asilimia 12 pekee walipata daraja la nne.
Shule hizo ni pamoja na Ilboru ambayo wanafunzi wote 131 wamepata daraja la kwanza, Mzumbe ambayo wanafunzi 107 wamepata daraja la kwanza na watano pekee wakipata daraja la pili na hakukua na daraja la tatu, nne wala sifuri.
Nyingine ni Shule ya wavulana Tabora yenye wanafunzi 115 wenye daraja la kwanza na watatu wenye daraja la pili ikiwa haina wanafunzi kwenye madaraja ya chini.
Shule nyingine ni Pugu yenye daraja la kwanza takribani nusu kati ya 127 huku shule ya Jangwani ikiwa na daraja la kwanza 125 kati ya 225.
Msalato ina wanafunzi 102 waliopata daraja la kwanza kati ya wanafunzi 118, huku Kilakala daraja hilo wakiwa ni 98 kati ya 114.
Kwa upande wa Tanga Technical yenye wanafunzi 200, daraja la kwanza ni zaidi ya nusu huku Shule ya wasichana Tabora daraja la kwanza ni asilimia 83 kati ya wanafunzi wote na Zanaki 57 kati ya 172.
Akizungumza na Mwananchi leo Januari 26, 2024 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mdau wa elimu, Dk Zubeda Mussa amesema asilimia kubwa ya shule hizo ni za vipaji hivyo ni rahisi wanafunzi kupata ufaulu wa juu.
“Mara nyingi shule hizi zinachukua wanafunzi waliofanya vizuri darasa la saba, lakini pia idadi ya wanafunzi sio kubwa ikilinganishwa na za kata ambako unakuta mwalimu mmoja anafundisha hadi mikondo sita,” amesema Dk Zubeda.
Amesema ni rahisi kwa mwanafunzi kusoma kwa bidii anapokuwa kwenye shule kama hizo kutokana na historia na utamaduni wake kwenye kufaulisha wanafunzi.
“Changamoto ziko kwenye shule za kata, unakuta mwalimu mmoja ana vipindi 36 kwa wiki hususani mwalimu wa hesabu, hapo labda mwanafunzi afaulu kwa muujiza,” amesema.
Dk Zubeda ameongeza kuwa Serikali inapaswa kuajiri vijana wenye taaluma ya ualimu hususani wa hesabu ili kupunguza mzigo wa walimu wachache waliopo na kuongeza ufanisi utakaosaidia kupanda kwa ufaulu.
“Serikali isikwepe kuajiri vijana bali ifanye juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba shule za kata nazo zinainuka kwenye ufaulu, kama hakuna jitihada za makusudi hakuna kitu kitakachobadilika,” amesema.
Akizungumzia suala hilo, Msaidizi wa Mkuu wa Shule Taaluma Feza Boys, Shaban Mbonde amesema maboresho yanayofanywa katika shule za umma yamezifanya shule za binafsi ikiwemo yao kukuna kichwa zaidi na kuongeza ubunifu, ili kuweza kustahamili katika utoaji huduma za elimu
“Hivi karibuni Serikali imekuwa ikifanya jitihada katika kuboresha elimu katika shule za umma, lakini sisi kama wadau wa elimu binafsi tunapambana ili tuendelee kufanya vizuri zaidi ili kuziba pengo ambalo Serikali imeshindwa kulifikia.
“Katika kufanikisha hili, Serikali italeta shule nzuri, ushindani lakini sisi kama Feza hata wale wenye vipaji wakipangiwa serikalini wanaobaki wakija kwetu watafanya vizuri,” amesema.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa wanafunzi 76 wa shule hiyo wamepata daraja la kwanza na kati yake 47 wamepata daraja la kwanza la pointi saba.
Akitaja siri ya ufaulu huo, Msaidizi wa Mkuu wa shule ya Fedha kidato cha Nne, Richard Maina amesema matumizi ya mfumo wa ‘1 to 1’ (Mwalimu kwa mwanafunzi) ndiyo umewabeba.
“Unachukua mwanafunzi mmoja mmoja unakaa naye unamfundisha hadi kuhakikisha anaelewa, hii imesaidia kuongeza ufaulu, baada ya masomo pia kuna programu za kufanya mapitio ya mitihani ya nyuma na marudio hivyo inapofika wakati wa mtihani wanakuwa na uelewa,” amesema Maina.
Kwa upande wake Neema Kitundu ambaye ni mdau wa elimu amesema uongozi thabiti katika shule hizo ni moja ya sababu za wanafunzi kufaulu katika madaraja ya juu.
“Wanafunzi kujitambua ni swala la msingi. Na hii ipo kwenye shule kama hizo kutokana na historia. Mwanafunzi akifahamu nini kilichompeleka shule lazima atasoma kwa bidii na kupigania ndoto yake,” amesema Neema.
Neema ameongeza kuwa kwa asilimia kubwa ya shule hizo zina miundombinu bora ya kufundishia na kujifunzia suala ambalo linasababisha kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.