Connect with us

Makala

Kauli za vijana kwa nini hawaoi, hawaolewi

Dar/Mikoani. “Siwezi kuoa kama sina vitu vya thamani ndani, hata wanawake wa sasa ni ngumu kukubali kuolewa na mwanamume asiye na kitu,” hii ni kauli ya Nashon Fabian (36), mkazi wa Dar es Salaam.

Amesema kwa umri wake si kama hataki kuoa, lakini hawezi kuingia kwenye ndoa kama hana kitanda, jokofu, kabati na vitu vingine vya thamani.

Fabian haamini katika kutafuta mali pamoja na mwanamke atakayemuoa, akidai kwa sasa hakuna mwanamke anayeweza kumvumilia mwanamume asiye na kitu.

Hata hivyo, kauli yake imepingwa na baadhi ya wanawake wanaosema wanaume wengi kwa sasa wanaishi maisha ya kuigiza.

Witness Leonard (22), mkazi wa mkaoni Kilimanjaro, amesema wasichana wengi wanashindwa kuolewa na wanaoolewa wanaachika mapema kwa kuwa wanaume wengi si wa kweli, wanaishi maisha ya uongo, kinyume cha uhalisia.

“Sasa hivi hakuna upendo wa kweli, baadhi ya wanaume hawana upendo wa dhati. Anaweza kukudanganya kwa kukuahidi ama hiki au kile, lakini mwisho wa siku akishakuoa anakuacha unapambana na maisha mwenyewe,” amesema.

Witness amesema, “Anakuwa hana muda na wewe, ndiyo maana hivi sasa wanawake wengi tunapambana kuwa na maisha yetu bila kuwa tegemezi.”

Zuwena Rashid, mkazi wa Ngokolo mkoani Shinyanga amesema wengi wanaogopa kuingia kwenye ndoa kwa kuwatazama walioolewa ambao baadhi ndoa zao huvunjika baada ya muda mfupi.

“Wanaona ni bora wabaki ‘single’ na wengi hasa sisi wanawake tunaona kuolewa ni kwenda kuteseka, huishia kuzaa na kuwapa wazee majukumu ya kulea wajukuu,” amesema na kuongeza:

“Vijana wa kiume siku hizi hawapendi kujishughulisha, matokeo yake wanashindwa kuoa kwa kuona hawatamudu kuendesha familia.”

Mbali ya hayo, wanaume wamesema nguvu ya kiuchumi ni kikwazo kikuu kwa wengi kushindwa kuoa.

“Ingawa wapo wenye kila kitu, lakini kwa utashi wao tu hawataki kuingia kwenye ndoa wakihisi maisha ya ubachela ni mazuri, lakini wengi wetu ni kuogopa majukumu,” amesema Idrisa Rajabu, mkazi wa jijini Dodoma.

Mustapha Juma, kwa upande wake amesema inaaminika ndoa ni jukumu la mwanamume, hivyo anapaswa kuingia akiwa na nguvu kiuchumi na kijamii.

“Uchumi nikimaanisha kama nina uhakika wa kupata Sh10,000 kwa siku basi iwe hivyo kila siku au kipato kipande ili nisije kutetereka kumtunza mke wangu, na watoto nitakapokuwa baba,” amesema na kuongeza:

“Kama naona siviwezi, ya nini nijiongezee majukumu? Lakini pia unamuona binti wa watu ambaye ametoka kwao kuna maisha bora, anakuja kwako hata friji huna, huko ni kumtesa tu ingawa pia kwa kizazi cha sasa ni ngumu kukuvumilia.”

Amesema ili aoe angalau awe na uhakika wa kipato kwa asilimia 70, na 30 inayobaki watatafuta na mkewe. Bila hilo kutimia amesema hawezi kuoa.

Charles Edward (24), mkazi wa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro amesema sababu ya vijana kushindwa kuoa ni kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

“Hali ya uchumi sasa hivi imekuwa ni tatizo kidogo, vijana wengi hatuna ajira ili tuweze kuanzisha familia, maana mwisho wa siku unaweza kuoa mtoto wa watu ateseke, lakini anaweza kukukimbia pia kwa sababu sina cha kumpa,” amesema.

Adam Msafiri wa mkoani Shinyanga, amesema, “Zamani suala la kuoa lilikuwa linasimamiwa na familia, wazee ndiyo walikuwa wanalipa mahari tofauti na sasa kijana anawajibika kutafuta mwenyewe na bado aandae harusi ndiyo maana wanakwepa majukumu.”

Ibrahim Rojara, mkazi wa Shinyanga, amesema waliozaliwa miaka ya 1990 wanashindwa kuoa kutokana na kuona matukio mengi ya ndoa kuvunjika na ukatili wa kijinsia kuongezeka, ikiwamo wanandoa kuuana.

“Vilevile vijana wengi wa kike wanajirahisisha, hivyo kijana wa kiume akimhitaji inakuwa rahisi kumpata na wengine wanakwenda kununua ‘madada poa’ hivyo kufanya kuwa ngumu kuoa.

Seleman Mutabazi, mkazi wa Morogoro (48), amesema  anatamani kuoa hata kesho, lakini hali ya maisha inamkwamisha.

“Kuna kutoa mahari, lakini ndoa si harusi tu, kuna namna unatakiwa uishi na mkeo hapo ndipo wengi wanashindwa sababu ya kutokuwa na kipato cha uhakika, vijana wengi hawana ajira,” amesema.

Amesema, “Wale wanaolazimisha kuingia vivyo hivyo ndiyo hao tunasikia ndoa zao zimevunjika haraka, maisha huyaokoti kama embe kwamba unaoa ili kuyajaribu lazima ujipange kama mume.”

Kauli za vijana hao ni kutokana na alichosema Rais Samia Suluhu Hassan Januari 21, 2024  aliposhiriki ibada maalumu ya kumuingiza kazini Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa, katika viwanja vya Kanisa Kuu la Azania Front, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Rais amesema taasisi ya familia inakabiliwa na changamoto mbalimbali, akinukuu Ripoti ya Utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya ya mwaka 2020/2022 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu NBS inayoonyesha zaidi ya nusu ya Watanzania waliopo kwenye umri wa kuoa au kuolewa hawajaingia kwenye ndoa.

“Kwa wakazi wa mijini wastani wa asilimia 62 wapo tu mabachela wanazunguka tu mtaani, ndiyo maana tunazungumzia mambo ya ubakaji hauishi huko mtaani, hata vijijini takwimu zinaonyesha asilimia 55.5 ni mabachela,” amesema.

Rais Samia amesema hata wanaoingia kwenye ndoa, wana changamoto mbalimbali zinazosababisha migogoro ya ndoa, akitoa mfano wa takwimu za mwaka 2023/2024 walipokea mashauri 39,571.

Amesema nusu ya mwaka 2024/2025 wameshapokea mashauri 28,773 asilimia kubwa ya migogoro ya ndoa ikihusisha ndoa za vijana au ndoa changa.

Kauli za viongozi wa dini

Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo amesema japokuwa vijana wengi wa sasa wanadai hali duni ya uchumi, lakini si kweli.

“Ndoa haitegemei uwezo wa kifedha, kama hali yako ni ya duni, utakutana na duni mwenzako mtaoana, kama ni ya kifedha utakutana na wa kifedha mwenzako mtaoana, kinachokwamisha vijana wa sasa kuoa ni malezi na imani yao katika maisha.

“Hivi sasa kina dada wengi wanatembea hovyo, mtu anaona nimuoe wa nini? Wakati anachokitaka anakipata kirahisi,” amesema.

Amesema malezi na imani tofauti kuhusu maisha ndiyo vinachangiza vijana wengi waliofikia umri wa kuoa kutofanya hivyo.

“Zamani kutokana na malezi na mazingira fursa za kukutana na mwanamke zilikuwa ndogo, mtu anapofikia umri wa kuoa na uhitaji anaoa,” amesema.

Mchungaji Danny Sendoro wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, amesema wanandoa wengi kwa nyakati hizi hawana mfano mzuri wa kuwashawishi waliopo nje kuingia.

“Wengi wa wanawake na wanaume waliopo kwenye ndoa ni wazinifu kama wengine, hakuna nidhamu, uadilifu na usafi wa kumshawishi mtu ambaye hajaingia aione ni taasisi bora kwa wengi,” amesema.

Amesema hali ya uchumi au umri si kigezo cha ama kuoa au kuolewa, isipokuwa ni utayari wa kiroho, kisaikiolojia na kijamii wa kumfanya mtu kuoa.

“Mtu kuona yeye akioa au kuolewa anaweza kuwa mfano mzuri, na mwisho ni nguvu ya uchumi kati ya mwanamke na mwanamume itakayowafanya wafurahie ndoa, hii si utajiri bali namna ya kuweza kujitegemea na kupata mkate,” amesema.

Amesema moja ya vitu vinavyosababisha ndoa nyingi kuvunjika ni misukosuko ya uchumi.

“Mnapokuwa hamna pesa ndipo kunakuwa na muda wa kutosha wa kuwa na wivu, chuki, hasira, visasi na vitu kama hivyo,” amesema.

Amesema ili kutoka huko, kunahitajika kuimarisha upya msingi wa taasisi hiyo na wale waliopo kwenye ndoa watulie, huku watu wakipambana kuboresha vipato vyao.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi