Kitaifa
Majaliwa ataka ushirikiano zaidi NAM
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa nchi na Serikali Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) wahakikishe wanashiriki katika kila tukio la umoja huo ukiwamo ushirikiano katika ulinzi na usalama pamoja na kukabili mabadiliko ya tabianchi.
Majaliwa amesema hayo jana Ijumaa, Januari 19, 2024 wakati akihutubia katika mkutano wa 19 wa wakuu wa NAM ulioanza Januari 15 utakaomilika Januari 20, 2024 akiwa anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
“Tumezungumzia hali ya mabadiliko ya tabianchi na namna tunavyopata athari kwenye maeneo yetu na umuhimu wa kuweka mkakati wa namna ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi kwenye maeneo yetu,” amenukuliwa akisema Majaliwa katika taarifa iliyotolea na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Taarifa hiyo imeeleza masuala mengine ambayo Majaliwa aliyawekea msisitizo katika mkutano huo, kuwa ni kutoa wito kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), kuangalia ajenda za NAM na kushirikiana na umoja huo katika kuzitekeleza.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano huo wa siku mbili unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Ruwenzori, Speke Resort Kampala Uganda, umemkabidhi Rais wa nchi hiyo uenyekiti wa NAM.
“Mkutano wa NAM hufanyika kila baada ya miaka mitatu na mkutano wa mwisho wa 18 ulifanyika jijini Baku nchini Azerbaljan Oktoba, 2019. Mkutano huo haukuweza kufanyika tangu mwaka 2019 kutokana na janga la Uviko-19 lililoikumba dunia.
“Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kwenye masuala ya biashara, uwekezaji, kutokomeza umaskini, mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama katika mipaka, sekta ya afya, mandeleo endelevu, na uchumi wa kidijiti,” inaeleza taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa jana alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe kuhusu kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili ikiwamo uwekezaji kwenye sekta ya madini na biashara.
“Bado Taifa limeendelea na kauli mbiu yetu ya kuboresha diplomasia ya uchumi na tumewakaribisha Sri Lanka kuja kuwekeza kwenye sekta ya madini, viwanda na kilimo. Sri Lanka ni wanunuzi waziri wa madini ya vito, kahawa, chai, korosho na mazao ya mbogamboga,” amesema Majaliwa.
Rais wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe amesema nchi yake ipo tayari kuwekeza nchini na amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wapo tayari kufungua ubalozi Tanzania ili kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kurahisisha shughuli za uwekezaji na biashara.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje Na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na viongozi hao ni urahisi wa wananchi wa Sri Lanka kutembelea Tanzania na Watanzania kutembelea Sri Lanka.
Waziri January amesema, “mkutano huu umefungua fursa ya kuanzishwa kwa tume ya pamoja ya mashirikiano, Waziri Mkuu na Rais wa Sri Lanka wametuelekeza sisi Mawaziri wa Mambo ya Nje tukae na kutengenezwa tume hiyo kwa ajili ya kuratibu mashirikiano baina ya nchi zote mbili.”
Pia, Waziri January amesema miongoni mwa mafanikio ya mkutano huo ni nchi hiyo kukubali kufungua ofisi ya ubalozi nchini, ikiwa ni jitihada za kuongeza uwakilishi katika nchi za Afrika.