Makala
Athari za kutibu ugonjwa wa macho kwa njia asili
Dar es Salaam. Kukamulia maziwa ya mama kwenye jicho, kuliosha kwa maji yenye chumvi au kwa chai ya rangi, si miongoni mwa tiba za maambukizo ya ugonjwa wa macho mekundu ‘Red Eyes’ kama wengi wanavyodhani, wataalamu wanafafanua.
Hakuna tiba
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo anasema bado hakuna tiba maalum ya maambukizi hayo, badala yake dalili zake zinakadiriwa kuisha kwa muda wa wiki mbili hadi sita kwa baadhi ya watu.
“Wagonjwa wanashauriwa kufika katika kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupimwa na kupatiwa dawa ya kupunguza madhara kulingana na ishara zinazoonwa na daktari,” anasema.
Profesa Rugajjo anasema kuna namna lukuki zitakazowezesha kuzuia ugonjwa huo, ikiwemo kuepuka kugusa macho na iwapo utafanya hivyo unapaswa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Anasema vile vinavyogusa macho yako unapaswa ama kuvitupa au kuvisafisha kwa maji ya moto na sabuni, lakini haupaswi kuchangia vipodozi, taulo za karatasi, nguo na dawa za macho.
“Funika mdomo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya, pia tumia taulo tofauti na leso kwa kila mwanafamilia,” anasema.
Mtu anaambukizwa ugonjwa huo, kwa kugusa machozi au tongotongo kutoka kwenye macho yenye ugonjwa huo.
Anasema kugusana mikono na mtu mwenye maambukizo hayo ni sababu nyingine ya kuambukizwa ugonjwa huo na kwamba, dalili zake huanza kujitokeza kuanzia siku tano hadi 14 baada ya kupata vimelea.
Hata hivyo, anasema wanafunzi wanaougua wanashauriwa kukaa nyumbani hadi dalili zinapoisha kwa kuwa ni ngumu kuzuia maambukizo yasisambae kwenye mazingira ya shule.
Profesa Rugajjo anasema unapoona jicho linakuwa jekundu, linawasha na kuchomachoma, macho yanavimba, yanaogopa mwanga, yanatoa matongotongo meupe na ya njano ujue una dalili za ugonjwa huo.
“Uwezo wa kuona unakuwa kama kuna ukungu na unasikia maumivu ya macho hizi zote ni dalili za Red Eyes,” anasema. Kwa ujumla wake, anasema ugonjwa huo unasababishwa na kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho ‘Viral Keratoconjunctivitis’ na husambaa kwa kasi kubwa.
Kwa asilimia 80 mlipuko huo, anasema unasababishwa na kirusi cha ‘Adenovirus’.
Angalizo
Iwapo umebainika kuwa na ugonjwa huo, anasema ni vema kuepuka kutumia dawa zisizo rasmi na ambazo hazikuandikwa na daktari kwa wakati huo.
“Usitumie dawa za macho anazotumia mgonjwa mwingine au alizoandikiwa yeye awali alipokuwa na tatizo la jicho ili kuepuka madhara kwa kuwa dawa za macho ni tofauti kwa matumizi,” anasema.