Kitaifa
RC Dar atangaza Januari 23, 24 siku ya usafi
Chalamila ametangaza uamuzi huo leo Jumamosi, Januari 13, 2024 aliposhiriki ibada ya kuwekwa Wakfu Mwangalizi wa Jimbo la Babtist la Dar es Salaam, Makamu, Katibu, Katibu Msaidizi, Mhasibu na Mhasibu Msaidizi.
Katika salamu zake za mkoa, amesema shughuli hiyo ya usafi itafanyika hadi saa 12 jioni na kutokana na hilo, amewatoa hofu wananchi watakapoona vyombo hivyo vya dola mtaani wasiogope kwa kuwa watakuwa wanashiriki kufanya usafi.
“Kutakuwa kuna wanajeshi wengi zaidi ya 5,000, polisi zaidi ya 3,000, Zima moto, watu wa usalama barabani na Kikosi cha Kuzuia Fujo (FFU), JKT na watu wa uhamiaji, kwa hiyo narudia tena mkiwaona msiogope.
“Hivyo kama kuna watu wanadhamiria kufanya fujo watakutana nao barabarani, hivyo terehe 23 na 24 Januari kutakuwa na jopo kubwa la ulinzi na usalama watakaofanya usafi wa Jiji la Dar es Salaam,” amesema Chalamila.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amewataka viongozi wa dini kuwa mabalozi wazuri katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Kipindupindu kwa kuwa Serikali imeshatangaza mikoa sita kuwa na mllipuko huo.
Chalamila ametanza shughuli hiyo ya usafi siku hizo wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kufanyika kwa maandamano ya amani Januari 24, 2024 katika jijini la Dar es Salaam.
Maandamano hayo yametangazwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mbele ya waandishi wa habari na wanachama wa chama hicho kanda ya Pwani yakilenga kuishinikiza Serikali kuiondoa bungeni miswada mitatu ya sheria za uchaguzi.