Kitaifa
Shule binafsi zapigwa marufuku uenguaji wasiofanya vizuri
Dodoma. Serikali imepiga marufuku kwa wamiliki wa shule binafsi wanaowaondoa wanafunzi wenye alama za chini pindi wafanyapo mitihani yao ya kidato cha pili na darasa la nne.
Hayo yamezungumzwa leo Januari 9, 2024 Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda wakati alipotembelea Shule ya Mfano Iyumbu Dodoma.
Mkenda amewataka wamiliki waache tabia ya kuwafukuza wanafunzi ili shule zao zionekane zinafaulisha kwa kuwa zinabaki na watoto wenye uelewa mkubwa pekee na kuwaondoa ambao uelewa wao unaonekana ni mdogo.
“Matokeo ya Mtihani darasa la nne na kidato cha pili yametoka, Shule iliyompokea mtoto na kupokea ada tusisikie imemuondoa mtoto ili wabakie wenye akili tu,” ameongeza Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amesema kuwa Shule bora ni ile inayowasidia watoto ambao uwezo mdogo hadi kuwawezesha kuwa na uwezo mkubwa.
Aidha Mkenda amezitaka shule nazo zijitolee kuwafundisha wanafunzi bila kuwabagua kama wanavyojitolea wazazi kuwapeleka watoto wao kwenye shule bora licha ya gharama kubwa
A amewakumbusha viongozi wa shule kuacha tabia ya kuweka michango ya lazima inayomzuia mtoto kwenda shuleni kama mzazi hajalipa.